Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nianze kwa kumpongeza Waziri ambaye ametuletea mpango. Mpango wake ni mzuri sana na unaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao tunaujadili sasa hivi hapa ni kamnofu/kakipande kamoja ka miaka mitano tuliopitisha kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilipopitisha ulikuja mpango mrefu wa miaka mitano. Sasa hapa tunajadili kakipande tu kale ka miaka mitano ndio maana tunaona miradi mingi iliyoko humu ni ile ile ambayo inakuwepo, miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema miradi mingi tuliyonayo, tuna Bwawa la Nyerere, tuna reli ya umeme, tuna bandari zinajengwa na tuna miradi mingi ya kimkakati inajengwa. Kama kweli tuko tayari, nchi hii watu walihangaika sana kutafuta uhuru na bahati nzuri viongozi wetu watangulizi wa nchi hii walianza kwa kutengeneza utaifa na sio kutengeneza uchumi. Nchi nyingine zilianza kutengeneza uchumi bila kutengeneza utaifa. Sisi tumetengeneza utaifa upo na leo tunafahamiana vizuri sana. Kwa hiyo, kutengeneza uchumi na kupanga mipango sisi sio shida kwa nchi hii ya Tanzania, shida yetu ni kusimamia mipango, ndio shida tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza, kama miaka mitano iliyopita tumepanga mipango ya miradi ya kimkakati ,hatukuimaliza na leo ni mpango wa tatu tunaenda unaisha mwaka 2025. Bwawa la Nyerere litakuwepo, labda reli itakuwepo, labda bandari kwenye mkakati itakuwepo, hivi hii mipango itakwisha lini? Kwa hiyo, nafikiri kwamba Mawaziri wote na hasa Waziri mwenye mpango mwenyewe tuhakikishe kwamba miradi mikubwa tuliyopanga inaisha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema jambo moja tu, hii nchi hata tungepata Rais ananuka mafuta, hakuna. Kwa sababu watu wetu tunaowategemea huko chini hawapo. Sasa nchi hii imebaki kila Rais anayekuja Rais anafanya nini? Je, ninyi mmefanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna chama kikubwa cha CCM, tuna viongozi mahiri, tuna vijana tumewafundisha, ni makada na wazalendo, kwa nini hawafanyi mambo Rais amewaagiza? Leo kuna miradi inaliwa tu sasa tunasema tunatafuta hela, ipi sasa? Maana miradi yote ninayoiona ni ile ile na kusema kweli ndiyo tulivyopanga na huwezi kuleta mpango mpya. Cha msingi ni kukusanya fedha ili miradi iende kutengenezwa. Hicho ndicho cha msingi tulicho nacho. Tukusanye fedha miradi itengenezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani nilikuwa nasikia jambo wanasema, bwana Bwawa la Nyerere lina hela ambayo imekuwa ringfence. Sasa sijui Kiswahili cha ringfence ni nini? Kwamba kuna fedha ipo kiasi kwamba hatuhitaji fedha nyingine kutengeneza hilo bwawa. Tutakuwa tunatoa humu tunajenga. Kuna hela za ringfence ya SGR zinakuwepo na mimi najiuliza kama ipo au haipo kwa nini tusikope sasa hiyo fedha tukaifungia, tukasema hiyo fedha imalize huu mradi? Kwa nini tusifanye hivyo? Mara tunaambiwa fedha tunakusanya tunalipa, mara tunaambiwa fedha tunakopa, tuambiwe wazi sasa fedha za mradi wa Bwawa la Nyerere ziko wapi? Ziko tayari au tunazikusanya? Fedha za bwawa, reli na miradi mingine ya kimkakati. Mimi nafikiri hili ndilo jambo la msingi tulifanye.
Kwa hiyo, naishauri Serikali tuhakikishe tunakusanya mapato na tuyatumie ipasavyo, vinginevyo itakuwa ni mchezo wa kuigiza. Nchi yetu iko salama kabisa, tatizo ni namna ya kusimamia miradi yetu iende, tatizo ni namna ya kusimamia fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza jambo moja, jana nimesikia wanasema Mto Ruaha hakuna hata tone la maji. Mimi nimewahi kutembelea ule mto, sehemu kubwa ya ule mto hakuna kina kirefu. Sasa najiuliza hivi tukipeleka pale tukawa kila mita 500 au kilometa 15 tunachimba kina kirefu kwenye huo huo mto tunachimba mpaka tukaumaliza, hivi maji yakiisha si yatabaki mle ndani? Tumekuwa na mvua zinanyesha kila siku kwenye nchi hii, lakini maji yote yanatoroka yanaenda ziwani. Sasa najiuliza hivi tunafanyaje? kama hatuna uwezo wa kukinga maji kukabiliana na suala la climatic change tutafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya Bunda, Mheshimiwa Mwigulu mpango huu ni msingi wa bajeti ijayo. Sasa najiuliza hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe ungekuwa Mbunge wa Jimbo la Bunda ungefanyaje? Kama leo ndoo ya maji ni shilingi 1,000 mpaka 2,500 wakati kutoka ziwani ni kilometa 25. Leo maji yanakuja mpaka Dar es Salaam, mnasema maji yaje Dodoma, yaende Tabora, Shinyanga sijui yaende wapi, lakini Bunda kilometa 25 hatuna maji. Wanachi wangu, wananchi wa Mama Samia wanachota maji kwa ndoo shilingi 1,000 hadi 2500. Hivi wewe ungekuwa Mbunge wa Bunda ungefanyaje? Hivi wakikwambia hauwatetei hawana maji unafanyaje? Kwa hiyo, nakuomba kwenye mpango ujao wa bajeti uhakikishe kwamba maji yanaenda kwa babu zako, usiwaache kwenye hii hali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)