Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Mpango huu wa Mwaka Mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya tozo ambazo huwa tunatozwa kwenye miradi mbalimbali ya Serikali inayofanywa. Binafsi ninasikitika sana kwa sababu pesa ambazo Wakandarasi wakubwa wa nje na Wakandarasi wa ndani ambao wanakuja kudai Serikali ni pesa nyingi sana. Mpaka sasa zaidi ya Bilioni 12 tumelipa kama Serikali kwa ajili ya faini mbalimbali ambazo hawa Wakandarasi wameipiga Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba Mheshimiwa Waziri, tunapoweka mikataba yetu naamini tunao wanasheria mahiri sana katika Taifa hili ambao wamesomeshwa kwa kodi za wananchi inakuwaje wanachelewesha kuwalipa na kupelekea Taifa Kwenda kulipa pesa nyingi kiasi hiki kwa ajili ya kulipa faini ambazo zinaendelea. Inabidi iundwe Tume maalum ya kuangalia tatizo hili, inawezekana kuna watu wanafanya maksudi na wanafanya hizo deal ili waweze kula hela za Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kwamba tunajua tunahitaji kuendelea kulipana kwa wakati halafu Maafisa Masuuli hawawalipi Wakandarasi hawa mwisho wa siku deni lile linaenda kwa mwananchi wa kawaida ambae ndiye mlipa kodi ambaye pesa yake hii Bilioni 12 ilikuwa na uwezo wa kwenda kuongezea madarasa haya ambayo yanajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema kitu hiki ni kibaya? Miradi inapocheleweshwa na tunakwenda kulipa faini, kwanza inaondoa value for money, miradi ile pia inakuwa haiendi kwa wakati, lakini pia inakuwa chini ya kiwango kwa sababu usimamizi unakuwa si mzuri. Kama mradi ulitakiwa kwisha mwaka huu unapomalizia mwakani hata ufuatiliaji wake, ile monitoring and evaluation haiendi sawa. Mimi ninafikiri sasa ni wakati kama Taifa tuhakikishe maafisa masuuli na wanaohusika kuchelewesha watu kulipwa wachukuliwe hatua kali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ifike hatua sasa Serikali ilete muswada hapa Bungeni ili kupitia Muswada huu itungwe sheria ambayo itafanya yeyote anayechelewesha achukuliwe hatua ili tuweze kusonga mbele kama taifa; na fedha nyingi sana ambazo zinapotea ziweze kurudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mifano ya miradi ambayo tumewalipa hela nyingi sana. Kigongo – Busisi kwa mujibu wa CAG ripoti yake ya mwezi Machi, ukurasa wa 185 anasema tulichelewesha kuwalipa na wao wakatupiga fine ya bilioni 1.5 hizi fedha ni nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ripoti ya CAG huyohuyo kuhusiana na SGR anasema tulipochelewa kuwalipa wale wakandarasi tumeweza kuwalipa kama Taifa pesa zaidi ya bilioni 3.144. Hizi fedha ni nyingi sana kwa Watanzania, zingeweza kusaidia kwanye bajeti ya nchi na tukaendelea na maendeleo kama kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi ya barabara. Kumekuwa na ahadi nyingi sana za barabara. Tunaambiwa tumetoa fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Tumetolewa fedha, kwa mfano kuna barabara inayokwenda Soni – Bumbuli mpaka Korogwe kilometa 74. Hii ilitolewa fedha takribani milioni 924 kwa ajili ya upembuzi yakinifu, lakini ukifika wakati wa bajeti nyingine inakuta bado tuko palepale hatujaanza kuufanyia mradi ule kazi, zile fedha zinakuwa zimelala. Na hiki inawezekana ni kichochoro cha watu kupitishia fedha za kuweza kuliibia Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Mtwara – Newala na Masasi kilometa 221; zimepelekwa fedha za upembuzi yakinifu wakati huohuo inatengwa bajeti na mwaka mwingine ukija bajeti bado iko palepale. Tunaomba ufuatiliaji wa miradi kama huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mfumuko wa bei. Tunapozungumzia mfumuko wa bei kiukweli unamzidishia mwananchi wa kawaida maisha kuwa magumu; chakula na mahitaji ya muhimu ya kimsingi bei imekuwa juu sana. Kama Taifa na Mheshimiwa mwenye Wizara husika tunaomba tumsaidie mwananchi wa kawaida ambaye kimsingi mfumuko wa bei kwa sasa umepanda umekuwa asilimia 7.8 ilhali inahitajika tusivuke asilimia tatu kama Taifa. Mfumuko wa bei unapokuwa juu maisha yanapanda. Tunaomba tusimamie tuhakikishe tunakuwa tuko sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninaunga hoja, lakini tuhakikishe tunasimamia yale ambayo tumekubaliana kama Taifa. Ahsante. (Makofi)