Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nichukue nafasi hii kwanza kutamka rasmi naunga mkono mapendekezo ya Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchangiaji wangu utajikita katika suala zima la viwanda, lakini pia nitazungumzia masuala ya Zanzibar kama wengine walivyozungumza japo tunaandaa Mpango Kazi. Napenda utambue kwamba kitambulisho changu cha Uzanzibar ni Na.010242768 ambacho ni halali na kitambulisho changu cha Tanzania ni Na.196650102-12114-0001-17. Nimeona nijitambulishe nafasi hiyo ya Uzanzibari kwa sababu kuna watu Zanzibar wanaijua kwa ramani lakini wanaisema kama vile wanakaa kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Zanzibar tuliiachia Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar ambayo imetoa maelekezo na mpambano ni tarehe 20 Machi, 2016. Huwezi ukakaa unasema wewe unaendekeza demokrasia, unaijua na unataka haki itendeke wakati unawaaambia wananchi wako wasiende kupiga kura. Demokrasia ya kweli inachagua viongozi wanaowataka wao siyo kwa kiongozi mmoja kutamka watu wangu msipige kura, hiyo demokrasia ya wapi? (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia Zanzibar ni shwari na salama atakaye aje. Zanzibar ingekuwa siyo shwari Wabunge tusingekuwa hapa. Wabunge wote tungekuwa tumeshaenda Zanzibar kwa ajili ya hekaheka ya Zanzibar lakini Wabunge kutoka Zanzibar tuko hapa hii inaashiria jinsi gani Zanzibar iko shwari. (Makofi)
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa
wakiongea bila mpangilio)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kukumbusha, humu ndani hakuna Amiri Jeshi Mkuu anayeweza kutangaza hali ya hatari. Nakumbuka tarehe 29 Oktoba, 1978, Nduli Iddi Amini alivyoingia Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu ndiye alitangaza kwamba tuna hali ya hatari nchi yetu iko kwenye vita. Sasa humu ndani ni nani aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu anayetangaza Zanzibar si shwari? (Makofi/Kicheko)
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa
wakiongea bila mpangilio)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa siku zijazo, kwa kuwa Wabunge tunatoka kwenye kampeni tukija hapa labda kidogo akili zina-change itabidi tupimwe kwanza akili ndiyo tuingie Bungeni. (Makofi/Kicheko)
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa
wakiongea bila mpangilio)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu mpaka sasa hivi wanaongea wanafikiri wako kwenye kampeni, wamesahau kwamba kampeni zimekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie Mpango na kama nilivyosema nauunga mkono. Tunavyo viwanda ambavyo vinahitaji kufufuliwa, naomba viwanda vile vifufuliwe vikiwepo vya korosho na vya nguo. Sambamba na hilo naunga mkono pia utaratibu wa kujenga viwanda vipya, naomba vijengwe katika maeneo husika ambapo malighafi inapatikana. Isije ikawa kama tulivyofanya Kiwanda cha Almasi kinajengwa Iringa wakati almasi haipatikani Iringa. Naomba tuangalie kipaumbele cha namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo naomba vijana wetu wawezeshwe katika kupata elimu ya utaalamu huo ili tusije tukajaza wataalamu kutoka nje na vijana wetu wakakosa ajira. Katika ajira hizo, naomba vijana waangaliwe zaidi siyo kwamba hatutaki uzoefu wa wazee, tunaomba ule uzoefu uende pamoja na uzeefu muda ukifika wastaafu ili vijana wapate nafasi. Kumekuwa na tabia baadhi ya wazee ambao wako kwenye nafasi wanapoanzisha mradi wanaanza kubadilisha majina, anakuwa Project Manager inapokuja kuanza kazi wanatengeneza CV zinazolingana na wao walivyo ili vijana wasipate ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba hali hii ibadilike vijana wapewe ajira na experience wataipata wakiwa kazini, wanayo nafasi ya kujiendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba wafanyakazi walipwe mishahara mizuri ili kuondoa migogoro kwenye viwanda hivyo. Kwa sababu kama kutakuwa na migogoro viwanda vitafungwa vitashindwa kuzalishwa na majipu yatazidi kuonekana. Katika hili nikukumbushe majipu mengi makubwa huwa yanatoa na alama ya sehemu gani ukamue ili kiini kiweze kutoka. Upande wa pili unaong‟ang‟ania CCM tuna majipu kule kuna matambazi, yale majipu makubwa ambayo hayaoneshi mdomo uko wapi? Mimi nikuhakikishie majipu ya namna ile lazima yatumbuliwe na mikasi. Majipu makubwa makubwa kama yale ambayo yanaitwa matambazi mengi yako upande wa pili japo hawataki kuyasema. (Makofi/Kicheko)
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakiongea bila mpangilio)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napenda kuongelea kuhusu sekta binafsi. Naomba sekta binafsi zipewe ushirikiano wa kutosha kwa kuondoa urasimu na ukiritimba ili waweze kufanyiwa maamuzi ya haraka ili vijana wetu wapate ajira na tupate maendeleo ya haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, naomba niseme naunga mkono wale wote waliochangia kuhusu kuboresha miundombinu ya umeme, bandari, barabara, maji, reli na mawasiliano ili tuweze kufikia malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nasisitiza, Zanzibar ni shwari atakaye na aje. (Makofi)