Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi napenda kutumia nafasi hii kupongeza maandalizi ya mpango pamoja na Taarifa ya Kamati ya Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu, mimi ni mwanamichezo nitumie nafasi hii kuwapongeza Wananchi, jana wametuheshimisha, wamefuata nyayo na wameweza kuuthibitishia umma kwamba kumbe hata sisi ugenini tunaweza na hivyo wameenda hatua ya makundi. Nawapongeza sana. (Makofi/vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na pongezi hizi zinzendana na kama siku zote ambavyo nasema michezo ni uchumi, michezo ni biashara; kwa sababu kwa Yanga kuingia
katika makundi sambamba na Simba maana yake ni kwamba, timu hizi zinapocheza kwa mfano hapa Dar-es- Salaam tunaona watu wanafanya biashara, magari yanasafiri yanajaza mafuta tunapata fuel levy, akinamamantilie wanauza chakula, n.k. Kwa hiyo michezo ni biashara tuendelee kuwekeza katika michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuseme hayo napenda kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali, hasa kwa suala la ruzuku ya mbolea. Kwa kweli sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini tulikuwa na kilio kikubwa. Pamoja na changamoto ndogondogo ambazo wananchi wanakabiliananazo huko site lakini kwa kweli ni jambo ambalo linaenda kuinua kilimo chetu, linaenda kuongeza mapato kwa sababu, kutokana na kilimo ambacho ni takriban asilimia 60 wananchi wetu wataongeza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa ujenzi wa barabara ya Mafinga kwenda Mgololo, Iringa kwenda Ruaha National Park na Uwanja wa Ndege wa Iringa. Hivi vyote vikikamilika kwa sisi watu wa Iringa vitaenda kusisimua sana uchumi kwa sababu utalii ukiongezeka sisi watu wa Mafinga, pamoja na kwamba, tutauza mbao na mirunda lakini pia wakulima wetu watauza mbogamboga, wakulima wa parachichi watauza matunda. Ni jambo la kupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na pongezi hizi nitoe tahadhari. Nimeona katika Taarifa ya Kamati, Ukurasa wa 34, kwamba wana mashaka na EPC+ Financing. Sasa na sisi tuliambiwa barabara ya Mafinga – Mgololo itajengwa kwa EPC+Financing kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind up tuweze kupata ufafanuzi kutokana nah ii hoja ya kamati, tunaendaje mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la Tanzania ya Kidijitali. Ukienda katika Ukurasa wa 14 na 15 wa Kamati, uchambuzi unasema kwamba, Kamati imebaini kwamba mapato mengi ya Halmashauri hasa yale yanayokusanywa nje ya mfumo hupotea bila kuingizwa kwenye akaunti za Serikali. Lakini pia Kamati inasema kwamba pamoja na jitihada na kazi inayofanywa na Mfuko wa Mawasiliano imebaini kuwa kuna ugumu wa kuyafikia baadhi ya maeneo kimtandao kutokana na uwezo wa kifedha au kutokana na kwamba, yale maeneo hayana vivutio vya kibiashara kwa hiyo, kampuni za kibinafsi haziwezi kujenga minara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka tuongeze mapato. Kwamba hoja ya kwanza, ili tudhibiti upotevu wa mapato lazima tuwe na mifumo ya kidijitali lakini at the same time hatuwezi kuwanayo kwa wakati kwa sababu, gharama za kujenga minara na hiyo miundombinu ni kubwa mfuko tu peke yake hautoshi. Kwa hiyo, kamati imesema nini? Kamati imeshauri kwamba, pawepo na vivutio maalum vya ki-kodi kwa ajili ya ujenzi wa minara na uendeshaji kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wakati kamati inashauri hivyo nataka nikupe contradiction iliyopo. Kwa mfano kwa wenzetu nchi jirani hapa East Africa, kwa mfano Kenya ukijenga huo mkongo kwa urefu wa kilometa moja Serikali ina-charge dola 50, yaani ukipitisha katika ile road reserve au ile open space ambayo ni ya jiji, wenzetu Uganda wanatoza dola 30, Rwanda kwa sababu wanavutia zaidi wanatoza dola 0, sisi tunatoza dola 1,000 kwa kilometa moja ukitaka kujenga ile fibre.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza ukaona, wakati huku tunapendekeza nafuu ya kikodi kumbe sisi wenyewe bado kuna baadhi ya charges zinaweza kutusaidia kupunguza hizi gharama ambapo mwisho wa siku itasaidia kupunguza hata haya malalamiko ambayo kila siku tunamlilia Mheshimiwa Nape kwamba, “punguza bando, gharama ni kubwa.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile haitoshi, unapopitisha miundombinu ya maji kwa Kilometa moja, unalipa wastani wa Dola 50. Ukipitisha Sewage system Dola 50, ukipitisha wire overhead Dola mbili, ukipitisha cable Dola 50, ukipitisha miundombinu ya gesi na oil Dola 50, lakini ukipitisha fibre unatozwa Dola 1,000. Kwa hiyo, kama unataka tuwezeshe hii mifumo ili kudhibiti upotevu wa mapato na kwenda online na hii Tanzania ya kidijitali, maana yake ziko taratibu, sheria na kanuni, na ni lazima kwanza tuweze kuzipitia hata kabla hatujaanza kufanya unafuu wa kikodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuoneshe faida; kwa mfano, BRELA toka walipoenda digital, makusanyo yao mwanzoni yalikuwa Shilingi bilioni 11 kwa mwaka. Mwaka uliofuatia wakakusanya Shilingi bilioni 18, sasa hivi wanakusanya mpaka Shilingi bilioni 29. Nikufahamishe, leseni hizi za biashara za halmashauri, kimsingi vile vitabu vinatolewa na BRELA. Halmashauri A inaweza kupewa vitabu viwili, ikaenda kutengeneza vitano, ndiyo maana kunakuwa na upotevu ambao Kamati imesema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwisho wa siku ni lazima tuiwezeshe Serikali na Wizara ya Mheshimiwa Nape ili kusudi huu mkongo wa Taifa ujengwe hata kwenye maeneo ambayo hayana vivutio kibiashara, tuweze kuwa na miundombinu ambayo itatuwezesha kukusanya mapato kwa njia ya kidijitali ili hayo mapato yatusaidie kujenga miundombinu ya elimu, madarasa, vituo vya afya na gharama nyingine kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baada ya kusema hayo naona kengele imelia, naunga mkono hoja. (Makofi)