Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mtanisamehe sana leo sauti sio nzuri kama ile mliyoizoea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, kitendo cha kutoa trilioni 1.3 ziende kwenye miundombinu, imesaidia sana sana kwa madarasa na sasa tunaamini kweli watoto wakiingia kwenye madarasa yetu yapo na yamekaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo niombe Waziri wa Fedha kwenye Mpango tuone sasa tunaongeza bajeti kwenye research. Kwenye ile mikopo ya wanafunzi tusipoongeza fedha, research zetu zitakuwa za kulipua. Pia tuongeze bajeti kwenye COSTECH wafanye research za uhakika. Nalisema hilo leo nalirudia ni mara ya nne; elimu ni rearch, afya ni rearch, uvuvi ni research na kadhalika. Haya yote tunayozungumza humu ndani bila kujikita kwenye research za uhakika na kutoa
facilities za uhakika kwenye research itakuwa ni kazi bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi mlimsikia Mheshimiwa Rais akizungumzia suala la family planning. Alizungumzia suala la family planning na kusema sasa twende na family planning tupunguze lile zoezi ili tusiwe tunaongezeka kwa mtindo ambao hautasaidia kuleta maendeleo. Alilisema hivyo kwa sababu gani? Tayari takwimu za research ndizo zilisaidia Mheshimiwa Rais akaona kwamba huko tunakokwenda ni kubaya. Kwa hiyo ushauri huo aliutoa kwa sababu ya ripoti hizo za research. Ndio maana nasema research ni muhimu katika kila nyanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kila Wizara hapa wana zile basic research yaani kila Wizara ina kaeneo ka research wana basic research, lakini niwaombe washirikiane na Vyuo Vikuu ili wafanye research za uhakika, ziwe research effective.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachangia kwenye eneo la kilimo. Narudia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita kwamba anaendeleza ule mpango wa kuwapeleka Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wengine wa Wizara Japan katika kusoma ile Program ya Local Government Reforms. Sasa kwenye hiyo program wenzetu kule wanaangalia namna gani kila eneo linaweza likawa na jambo moja la kuwaletea uchumi wananchi mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna program ile inaitwa OVOP, one village one product, sisi tujipange kwenye one district one product au one region one product. Mwekezaji au mfanyabiashara akija Tanzania akisema nataka asali nzuri unamwelekeza sehemu. Vile vile sio asali nzuri mwingine anasema nenda Lindi, nenda Singida, nenda Tabora hiyo haitawezekana. Kwa hiyo tukiwa na program ile tukai-develop hapa kwetu, tukai- copy, ndio italeta ufanisi na yale mafunzo yetu tunayokwenda huko yatakuwa yanaleta tumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mazao hapa wenzangu walishaongea, unakwenda mahali ujue kabisa hapa nakwenda kwa ajili ya kahawa, nakwenda mkoa huu kwa ajili ya alizeti, nakwenda mkoa huu kwa ajili ya mahindi, lakini sitapenda kuzungumza nakwenda mkoa huu kwa ajili ya tumbaku. Hilo nimemwambia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, hilo hapana. Kwa hiyo tujipange hivyo, twende na ile program ili tusaidie. Wawawezeshe sasa, wamerudi kwenye mpango Mheshimiwa Waziri awawezeshe sasa tu-practice ile ili kwa kweli tuwe na zao moja, sio lazima zao la kupanda hata madini mbalimbali, mwekezaji au mfanyabiashara akija ajue nakwenda mahali fulani napata kitu fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika kufanya hivyo niombe katika Mpango, hivi ni lini wakulima hawa wataendelea kulima kwa jembe la mkono? Niombe Mheshimiwa Rais anapotafuta fedha hizi nyingi na zinapoingia katika Mawizara tunakuja hapa tunalalamika fedha nyingi zinapigwa. Hebu tujipange sasa hizo fedha zisipigwe, tuone kama tunaweza kufanya pilot study kwenye mikoa michache, vijiji vinunuliwe matrekta, kijiji kimoja matrekta matatu, tutakuwa tunafanya kitu cha maana. Tunataka uchumi wa mtu mmoja mmoja, lakini hili jembe la mkono Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Mwigulu hatufiki mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujaribu, hivi hatuwezi kila kijiji kikapata trekta tatu? Kwani trekta tatu ni bei gani? Waweke kwenye mpango kwani hawalielewi hili? Hebu waweke kwenye mpango jamani tubadilishe hiki kilimo. Yaani hii mipango tutaiongea lakini itakapokuja wakati wa utendaji kama mtindo ni ule ule wa jembe la mkono, nakwambieni tutakuwa na mipango lakini utekelezaji wake ni zero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kama nilivyosema, tuone kabisa kwamba sasa kwenye mpango huko zao la tumbaku Waziri asiliweke, kama wanataka kuendelea kulima tumbaku, wawachague wale wakulima wakubwa wanaofaidika, wa-deal na hao wakulima wakubwa, wakulima wadogo wa tumbaku hawapati faida yoyote, Mheshimiwa Bashe analijua hilo, hawapati faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale verifiers usipowapa pesa, usipowahonga, tumbaku yako kila siku itakuwa grade ya chini, sasa kuna faida gani? Wawawezeshe wakulima walime mazao yale yanayoweza kuwapa faida, mazao mbadala, tumbaku tuipige vita, tumbaku haiwasaidii wakulima wa chini.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe mzungumzaji taarifa, ni kweli faida inakuwa ndogo kwa sababu hata kwenye masoko kumekuwa na utaratibu wa kufanya central market ambazo zinafanyika mjini badala ya masoko kufanyika kwa wakulima walioko kwenye maghala yao vijijini.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara unapokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili na namwomba anisaidie tuendelee na kampeni ya kuliondoa na kulipunguza kabisa hili zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)