Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangaia katika Mpango huu wa Serikali. Mchango wangu utajikita katika maeneo matatu kama muda utanitosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na suala ambalo Serikali yetu hasa ilani ilitoa kwamba inataka kufikia ajira milioni nane kwa ilani hii tunayoendelea nayo. Hata hivyo jambo hili linakuwa gumu sana kutekelezeka kwa sababu vyuo vyetu vimejikita sana katika kuzalisha watu wa utawala, mambo ya kijamii lakini halijajikita katika kuzalisha watu wa production. Watu wa production ni watu ambao wamesoma mambo ya sayansi. Kwa sababu ukisema kilimo ni sayansi, kufuga ni sayansi, utawala tayari tuna watu wengi sana wa kutosha. Watu wa uhasibu, leo taasisi kubwa kama hii ya Bunge inahitaji Wahasibu labda wawili au watatu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unapotaka kwenda kwenye production, kama unataka kufuga lazima uwe na watu wengi ambao wamesomea na wana uwezo. Ukitaka kulima ardhi hii ni kubwa na inahitaji watu wengi. Kwa hiyo, ningeshauri hivi vyuo vyetu vifike mahali viangalie production vinatoa watu wa aina gani katika vyuo vyao. Ukizingatia kwamba watu hawa wanakopeshwa mkopo na Serikali na inabidi walipe mkopo. Sasa kama ni watu ambao wanaweza kujiariri, ambao wanaweza kuzalisha ni rahisi kuwa-trace na kurudisha mikopo na watu wengine wakaendelea kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka huu mtindo wa ku- copy, sasa hivi ukiangalia UDSM na UDOM karibu course zote ni zile zile tu zinajirudia watu wa jamii, utawala na ndio nyingi. Kwa hiyo ningeomba mwelekeo wa vyuo vyetu uangalie kwamba unazalisha watu wa aina gani na hii itakuwa rahisi hata Serikali inapowakopesha fedha zile zirudi na uchumi wa nchi yetu kuweza kuchangamka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, lazima sasa niguse kwa mwajiri wangu ambaye ni wananchi wa Mkalama. Sasa hivi tunajenga barabara kutoka Manyara – Simiyu, barabara ya kimkakati kabisa. Barabara hii tunapojenga na tayari imetangazwa ni vizuri tukajenga katika mtazamo wa kibiashara pia ili Serikali iweze kukusanya mapato. Zipo baadhi ya barabara ndogo sana ambazo zikiwekwa pamoja na mradi huu ambao ni feeder roads zitasaidia sana kufanya barabara hii ichangamke kuleta mapato. Ikichukua barabara kutoka Iguguno inayopita Mkalama kwenda kuunganisha na barabara hii kule Sibiti na ukichukua barabara inayotoka Iyongero inakwenda kuunganisha na barabara hii kwenda kule Haidom, barabara hizi zinaunga barabara kubwa ya katikati ya nchi inayotoka Dar es Salaam mpaka Mwanza zinaunga na barabara hii ambayo itakuwa ni kubwa katika corridor upande wa kaskazini na huko ndiko kuna mbuga za wanyama na kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utaona kabisa wananchi wanaotoka Nyanda za Juu Kusini watapita hapa katikati kwenye utalii wa ndani na kwenda kuchangamsha uchumi wetu kwenye mbuga za huku. Kwa hiyo utaona barabara hizi zitakuwa zimekaa kiuchumi zaidi na zitaleta faida kwa nchi yetu. Kwa hiyo ushauri wangu, kwa sababu sasa ujenzi wa barabara hii umeshatangazwa na unajengwa kwa EPC+F, basi na barabara hizi wataalam wetu waziunganishe katika barabara hii, hivi vipande viwili vidogo vya barabara nilivyovitaja, viwe kama feeder road ili barabara hii iwe na faida zaidi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nisemee kwenye suala zima la mawasiliano. Mawasiliano ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Kitu kinachonishangaza sana, kaka yangu Mheshimiwa Nape juzi ameleta hapa Muswada wa kulinda habari binafsi, tukampitishia Muswada mzuri kabisa, lakini nataka alete tena Muswada mwingine wa kuhusu kulinda haki zetu. Mashirika haya yamekuwa yakituibia, hivi ni kwa nini bando zina-expire? Simu ni ya kwangu, nimenunua bando kwa fedha yangu, halafu unanilazimisha nitumie kwa muda unaotaka wewe, hii ni kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni sheria, basi iletwe hapa tuibadishe, kwa sababu tunawaibia wananchi. Anatafuta fedha kwa jasho, ananunua simu, anataka awasiliane ananunua bando limsaidie, anaambiwa ndani ya siku saba limeisha. Hivi hii sheria ni ya nchi gani? Kama ni sheria tunaomba ije hapa, kwa sababu tunaibia hawa wananchi na tunaibiwa huku tunaona, kwa nini unipangie kutumia bando langu? Mimi si ndiyo najua umuhimu wa mawasiliano ndiyo maana nikanunua lile bando la wiki moja! Kama nimeamua kulitumia taratibu, wiki moja imeisha nimeweka akiba kwa nini wewe ulikate? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuomba sana kwa hili uwe mkali, utuongoze hili jambo la kuibia wananchi wa Tanzania lifikie mwisho…
T A A R I F A
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa taarifa hiyo. Mimi bado naona kwamba kama utaratibu ni huo bado Bunge lako linahaja ya kutunga Sheria kuwalinda wananchi kuhusuiana na suala zima la matumizi ya bando, kwa sababu hata TANESCO tunanunua umeme kwa Tarif one na huo umeme ukifika unapata unit 75 unapofika mwisho wa Mwezi hujazimaliza zile unit zako zinabaki unaongeza zingine zinaendelea kukusaidia, hata ving’amuzi. Kwa hiyo, ninaomba bado kuna haja ya kuja hapa tutunge Sheria ya kuwalinda wananchi wetu na bando zao, akinunua bando atumie mpaka liishe kama sivyo hiyo huduma waitoe wasiiweke kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu katika suala zima la kumuunga mkono Rais wetu. Mama yetu anao mpango mzuri wa kutaka wakina mama wapikie gesi safi, gesi asilia kwa sababu wanaumia sana na kupikia mkaa na kuni. Vilevile nchi inaisha kwa kukatwa miti kwa sababu ya mkaa. Nchi yetu tumebarikiwa tuna bomba la gesi linalotoka huko limefika Dar Es Salaam, lakini Bomba hili bado halijaenea katika nchi hii. Kwa hiyo, niombe katika mpango bomba hili litoke Dar es Salaam sasa lisambae katika nchi, lielekee Mwanza,Kigoma, Kaskazini, Arusha na kusini huku ili wananchi tuweze kutumia gesi asilia kwenye majumba yetu. Teknolojia ya magari sasa hivi inatumika, Dar Es Salaam sasa hivi magari karibu yote ya uber wanatumia gesi asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilo moja ya gesi inakwenda mara mbili ya lita ya petroli na bei ya kilo moja ni karibu 1500 na huku petroli ni 3000 na kitu. Kwa hiyo katika mpango bomba la gesi liende likasambae hata kwa kipenyo kidogo sio sawa na kipenyo kikubwa sana kilichotoka kule kusini ili lisambae kwenye nchi ili tuweze kutumia gesi na tumuunge mkono Mama yetu kwa kuhakikisha kwamba tunatumia gesi asilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili litachangamsha uchumi kwa sababu miti itapona na tabianchi itabadilika kuwa positive, mvua itaongezeka mabwawa yetu yatajaa maji. Kwa hiyo hili jambo lina faida mtambuka lina faida kubwa sana kusambaza bomba ambalo tayari tunalo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri katika mpango wako fikiria suala la Bomba kwenda Mikoani. Kama Mama anatoa Bilioni 100 kila Mwezi kwenye ruzuku ya mafuta anao uwezo pia wa kutoa fedha kwa aijili ya kujenga bomba ambalo litatuokoa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka tumuunge Mkono Mama yetu katika uchumi kwa kusambaza bomba wananchi wa Tanzania wafaidi bomba hili wakiwa bado hai na vizazi vijavyo pia waje wafaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme hayo kwa uchungu kabisa kwamba yakitekelezeka naamini Watanzania wengi watafurahi. Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)