Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii. Nafikiri sitakosea kama mwenzangu aliyetangulia.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, naomba ni-declare interest kwamba mimi nimezaliwa katika quarter za Jeshi...
TAARIFA
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.......
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, uko sahihi kwa sababu na wewe umelizungumzia. Naomba ulinde muda wangu. Naendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, nimezaliwa kambini, Jeshi ninalolijua nikikua lilikuwa ni Jeshi makini kwa maana ya kipato. Wazazi wetu walituzaa wengi kwa kuwa walikuwa wakiishi maisha mazuri, walikuwa wakipata mishahara mizuri, tulikuwa tukipata ration kwa wakati na vitu kama hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jioni ya leo naomba nichangie. Tukiangalie bajeti iliyopita, ndugu zetu pesa za maendeleo walichangiwa shilingi bilioni 220 kama sikosei, lakini Serikali iliwapatia shilingi bilioni 40 au 41. Mimi najiuliza, watawezaje kuishi maisha mazuri tuliyoishi zamani kama Bunge imepanga na imepitisha hiyo bajeti na haijaweza kufika kwenye Jeshi waweze kufanya mambo ya maendeleo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia mambo ya maendeleo, tunazungumzia makazi. Wanajeshi wanahitaji nyumba nzuri za kuishi. Ni kweli tumeona, tumetembelea miradi, kuna nyumba zipo zinajengwa, lakini hazitoshelezi. Ninashauri Bunge linapopitisha bajeti tuhakikishe zile pesa zinakwenda kutimiza ahadi tuliyoahidi, wataenda kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Wananchi kama tunavyolisifia, ni Jeshi linalohitaji kuilinda nchi yetu, mipaka ya nchi, lakini pia tunafahamu umuhimu wa chombo hiki; kama tunashindwa kuipatia pesa kwa sababu zozote zile, tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe Wabunge. Shilingi milioni au shilingi bilioni 41, ni miradi gani wafanye, ni miradi gani waache?
Mheshimiwa Naibu Spika, siasa ni nzuri, lakini tusifanye siasa kwenye vyombo vya ulinzi. Tunapozungumzia bajeti; na hii naizungumzia kwa Wizara nzima, nikimaanisha Polisi, Magereza na Jeshi wenyewe. Pesa wanazopata tuhakikishe zikipitishwa kwenye Bunge hili zikafanye kazi sawasawa na tulivyoahidi. Walipata pesa nusu karibu shilingi bilioni 600 hazikwenda kutenda kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafika mahali na wengine wameshasema, hawa ni binadamu, wanaweza wakaingia tamaa kwa sababu wakiishi vibaya hawawezi kusimamia uadilifu waliokuwa nao. Ni kweli tutawasifia, lakini ipo siku wanaweza wakaenda pembeni kwa sababu hatujawajali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba Mkuu wa Majeshi leo yupo. Wanawake walioko Jeshini, najua kwamba kuwa mwanamke siyo kwamba huwezi kufanya vizuri. Ninaamini wapo wanawake wenye vyeo, ila ninatamani na ninamwomba ikibidi wanawake waongezwe vyeo, siku moja tuwe na CDF mwanamke na sisi Tanzania tuonekane tumesonga mbele. Ninaamini vyeo kuanzia chini vipo, naomba mchakato wa kuwapandisha vyeo ufanyike sawa sawa na utashi wa kazi wanazofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu ni mahiri na wenzangu waliotangulia wamezungumzia habari ya Zanzibar. Sitazungumzia huko ila nina swali la kiufahamu; siku za hivi karibuni nimeona viongozi wa kisiasa waliokuwa ni wastaafu wa Jeshi wakiapa kwa kuvaa nguo za Jeshi. Naomba nielezwe ni utaratibu wao au ni kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa mdogo, niliona Mheshimiwa Rais Nyerere wakati wa vita vya Idd Amini akiwa amevaa kombati na nguo za mgambo. Nafahamu kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa Luteni; mpaka anastaafu sijawahi kumwona amevaa nguo za Jeshi. Sijui nimeshau kama ni Kanali au hivyo! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamishwe, inawezekana sifahamu, siku za karibuni Mheshimiwa Rais wetu amevaa nguo za Jeshi. Najua yeye ni Amiri Jeshi Mkuu, hilo nalifahamu, lakini sikuona begani kama amewekwa cheo chochote.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekezwe, utaratibu ukoje? Najua ni Amiri Jeshi Mkuu, lakini begani sikuona cheo chochote. Je, ni sahihi?
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba, vitu vingi ni ufahamu; ni suala la kuelekezwa. Inawezekana ilitakiwa ifanywe na Marais waliopita, lakini hawakutaka, lakini kama ni utaratibu, tuelekezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, Wizara hii inahitaji sana pesa na hasa maeneo ya viwanda. Tunafahamu kwamba Awamu ya Tano mnazungumzia viwanda na jeshi hili lina viwanda; naomba bajeti hii, iongeze pesa kwenye maeneo ya viwanda vya Jeshi. Tukiiongezea pesa tunaomba Serikali badala ya kuagiza vitu vya Kichina, tununue kutoka kwenye Jeshi. Wale wanaopata ten percent wakati huu wasiweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwa kumalizia, Jeshi hili linafanya biashara, mbalimbali na ukusanyaji wa maduhuli. Ushauri wangu, maduhuli haya kwa miaka hii miwili tungeweza kuwaachia iweze kuwasaidia bajeti zao. Nasema hivyo, ninajua Serikali haina hela. Bajeti imeshuka, tukiwaachia maduhuli kwa miaka hii miwili waweze kufanya kazi zao vizuri, itatusaidia kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopitisha bajeti, hatupitishi kishabiki, tunapitisha tukimaanisha ujenzi wa Taifa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, maduhuli ya Jeshi yabaki kwenye Jeshi kwa miaka miwili. Ikipita miaka miwili, tutaendelea na utaratibu mwingine, ahsante.