Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika mwelekeo wa mpango wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Pia naipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuja na mwongozo huu wa Mpango na Bajeti ambao wameileta mbele yetu. Tatu, naipongeza Kamati ya Bajeti kwa namna walivyoichambua na kuleta maoni yao hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wetu lazima ujielekeze katika kujibu mambo ya msingi yanayotuhusu. Ninafurahi kuona kwamba mpango huu umeandaliwa vizuri. Mwelekeo wa mpango huu ni mzuri na unatupeleka kule tunakotaka. Yapo matatizo ya msingi ambayo sisi sote tunahusika na lazima tutafute mwelekeo wa namna ya kuyatatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni umasikini mkubwa wa wananchi katika utajiri ulio mwingi katika nchi yetu. Nchi yetu ni moja ya nchi tajiri sana, lakini watu wake ni masikini. Kwa hiyo, hili ni lazima mwelekeo wa mpango ukajibu hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni ukosefu na upungufu wa ajira kwa vijana wetu; na la tatu, ni mchango mdogo wa sekta za uzalishaji kwenye pato la Taifa. Jambo la nne, ni tija ndogo katika maeneo mbalimbali; na la tano ni ukuaji mdogo wa sekta ya viwanda na mambo mengine yote. Haya mambo matano ni msingi mkubwa wa utayarishaji wa mpango. Nami naamini kwamba mpango huu unatupeleka katika kujibu na kutafuta ufumbuzi wa haya ambayo yanaikabili nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ukisoma Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2000-2025, ina vipaumbele vitano. Moja ya kipaumbele ni kwamba tunataka kuboresha hali ya maisha ya Watanzania. Sasa hivi maisha ya Watanzania katika uhalisia, hali ni mbaya. Tunataka kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja, na hili tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa; tunataka kujenga utawala bora; tunataka kuwepo kwa jamii iliyoelimika na inayofundishika; na tunataka kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani wa nchi jirani na nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dira yetu inavyosema, mipango yetu, vipaumbele vyetu, Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, vyote vinashabihiana. Vinatulazimisha tukae chini tuweze kutatua haya matatizo ya wananchi. Sasa hali ilivyo sasa hivi, tunazo takwimu nyingi; tunayo nchi yetu ambayo imebarikiwa kuwa na rasilimali za kila namna, lakini tunazunguka katika mzunguko wa umasikini (poverty cycle), tunazunguka mle. Sasa hapa lazima tujikite kuona tunatokaje katika huu mzunguko ili twende kwenye eneo lingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mipango yetu na mambo yote ambayo tumekuwa tukiyafanya, bado tunazunguka. Sasa hivi kuna mjadala mkubwa kwamba nchi yetu ilikuwa imefika kipato cha kati, sasa tumerudi kipato cha chini, lakini sisi kazi yetu ni kuhakikisha kwamba tunatoka hapo tunaenda mpaka kwenye kipato cha juu. Sasa yapo mambo ambayo mimi ningependekeza kwamba tuyaangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumependekeza kwa muda mrefu na bado halijafanyiwa kazi. Kwanza, ni uwepo wa Tume ya Mipango pamoja na Baraza la Tija.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongezae Mheshimiwa Mbunge kwa mchango mzuri. Nimeona ame-refer hili jambo lililosemwa juzi kwamba Tanzania tumeshuka kwenda kwenye kipato cha chini, pamoja na kwamba nimejiandaa kuja kulijibu, lakini niliona ili kumsaidia atiririke vizuri, ni kwamba Tanzania haijashuka kwenda kwenye kipato cha chini na taarifa zilizotolewa na mchangiaji, Mbunge wa Musoma Vijijini siyo sahihi, na nukuu aliyonukuu na yenyewe haikuwa sahihi. Nadhani nitatolea zaidi ufafanuzi nitakapokuwa na-wind-up.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, kwa sababu sina tatizo kabisa katika huo mjadala unaoendelea. Naipokea kabisa kwa sababu tunatakiwa tuwe na takwimu sahihi, na ndiyo msingi wa kupendekeza kwamba tuwe na Tume ya Mipango itakayokuwa na uwezo wa kuchambua hali ya maisha, uchumi wa nchi yetu na kutupa takwimu sahihi. Ile Tume ya Mipango itapanua wigo, itafanya watu wote waweze kushirikishwa wataalam mbalimbali, waweze pia kujadili watupe takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri hii itatusaidia sana kuwepo kwa Tume ya Mipango lakini pia na Baraza la Tija ambalo litasimamia kupanua tija katika uzalishaji, tija katika viwanda vyetu na tija katika maeneo mbalimbali. Hili ni suala ambalo nafikiri ni la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumeona nchi yetu iko strategically located, na ndiyo maana sasa hivi tunazo bandari ambayo tunafikiri zinaweza kuhudumia nchi jirani. Sasa hivi kuna mjadala unaoendelea, watu wengine wanasema tujenge Bandari ya Bagamoyo na wengine wanakataa. Mimi nafikiri Bandari ya Bagamoyo ni inevitable, lazima tuijenge, na Bandari ya Dar es Salaam iendelee, ya Mtwara iendelee na bandari nyingine zitakazowezekana zijengwe. Kwa sababu lengo la hizi bandari ni kuhudumia, na tunataka zile nchi ambazo hazina uwezo wa ku-access ziweze kuhudumiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hili lazima tuweke nguvu. Kwa hiyo, nategemea mpango huu utakapokuja, utakuja na namna ya kuijenga hii Bandari ya Bagamoyo, lakini tusisahau na pale Bandari Kavu Mpemba, Tunduma kwa sababu pale ndiyo lango la SADC. Pale ndiyo nchi za Zambia, Malawi na nchi zote zitakuja kuchukulia mizigo pale. Kwa hiyo, tukijenga Bandari ya Bagamoyo, tunajenga Bandari Kavu pale Tunduma-Mpemba, tutakuwa tayari tumeitendea haki nchi hii. Tutaenda kujibu matatizo haya ya msingi ambayo nimesema yapo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo napenda kupendekeza, ni katika upande wa allocation ya resources. Mheshimiwa Waziri atakapokuja na bajeti, nimeona mwongozo, nimeusoma, lakini nadhani, ili tuondoke katika mzunguko wa umasikini ili tutoke pale, uwekezaji tuje na formula ya namna ya kuwekeza zile rasilimali zetu. Allocation ya resources zile za maendeleo, tuje na formula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza napendekeza, zaidi ya asilimia 30 au 40 ielekezwe kwenye sekta za uzalishaji. Kwa sababu tukielekeza kwenye uzalishaji, huko ndiyo wananchi wengi wapo; tutatatua tatizo la ajira, umasikini na tutahakikisha uzalishaji malighafi zinapatikana na ndiyo viwanda sasa vitaweza kujengwa, tutapata malighafi. Huwezi kufanya hivyo kama hilo halitakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 30 iende kwenye huduma za jamii na asilimia 30 nyingine iende kwenye huduma za biashara na miundombinu. Hiyo formula inaweza ikatusaidia kutoka. Tukiwekeza kwenye huduma za jamii bila kuwekeza kwenye uzalishaji, tutakuwa tunazunguka kwenye poverty line, hatutatoka kule kwenye yale maeneo ambayo mimi ningependekeza tutoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne, kujenga viwanda na kuanzisha mfuko wa kuchochea viwanda. Hatuwezi kujenga viwanda kwa kupiga kelele. Hatuwezi kujenga viwanda kwa kusema tunahamasisha viwanda, lazima tutenge fedha, tujenge viwanda, halafu tutafute waendeshaji wa hivyo viwanda. Yale mazingira yawe yameshatengenezwa, tutakuwa tayari tumetekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi, lakini mengine tutayachangia, nashukuru sana kwa kupata hii nafasi na ninaunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.