Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii adhimu ili nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa, nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu kama sitampongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Nchi hii Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Tuseme ukweli, mama wa watu; mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, anajitahidi. Ombi langu tu kwa wale ambao amewaamini, wasiendelee kumwangusha, wamsaidie ili aweze kutimiza kusudi lake la kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia mambo mawili tu, kwa kuwa muda siyo rafiki. Jambo la kwanza kabisa, nataka kuwaongelea wananchi wa nchi hii, wale ambao ni wa kawaida, wanyonge, masikini, wakulima na wote ambao wanafanya shughuli zao ndogo ndogo, wanazalisha mambo ambayo yako ndani ya nchi yetu, ni pamoja pia na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa nchi hii wanajitahidi sana na wanajituma sana katika kuzalisha mazao yao ambayo Mwenyezi Mungu amewasaidia wazalishe, na wengine wanatumia mpaka jembe la mkono katika kuzalisha, lakini ambacho nakiona, tunapaswa tuwekeze nguvu kubwa sana kwenye masoko. Kwenye uchumi wanasema, demand inapokuwa high, supply ikawa low au constant inapelelea price kuwa high. Tafsiri yake ni nini? Kama supply itakuwa constant au itakuwa low, demand ikawa high, maana yake wananchi hawa chochote watakachokuwa wanakizalisha kwa sababu wanazalisha katika supply hiyo hiyo, lakini demand inapokuwa kubwa kwenye masoko, itakuwa inaleta motisha ya wao kuendelea kuzalisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo ya mpango, nimesoma ukurasa wa 125 ambao unasema kuhusu huduma za biashara na masoko. Waziri wa Fedha na Mipango anasema, kuimarisha miundo mbinu ya masoko, lakini kipengele cha pili anasema, kuimarisha mfumo wa kilimo cha mikataba na upatikanaji wa mikopo ya kilimo yenye riba nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kipo kipengele ambacho kinazisisitiza balozi zetu kuhakikisha zinatutafutia masoko huko nje. Je, balozi zetu zimesimamaje kuhakikisha zinawatafutia wakulima wa nchi hii masoko ya kutosha ili hata kama supply yetu itakuwa limited, demand iwe high ili wananchi hawa waendelee kupata kwa kiwango kikubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo baadhi ya balozi ambazo tukiwasiliananazo, wanasema changamoto kubwa ambayo wanaipata ni wakulima wetu kushindwa ku-supply kuanzia mwezi wa Kwanza mpaka wa Kumi na Mbili (continuously). Wanashindwa kwa sababu gani? Wanazalisha kwa kiwango cha chini. Kama wanazalisha kwa kiwango cha chini, tafsiri yake ni nini? Hawajawezeshwa. Hapa tunaposema kwenye mikopo yenye riba nafuu, ndipo tunaposema Benki ya Kilimo ihusike na pia Wizara ambazo zimepewa dhamana kwa ajili ya kuziomba benki ambazo zinaweza zikatoa mikopo ya riba nafuu iweze kuwasaidia wakulima wa nchi hii pamoja na wafugaji ambao pia watataka kuwezeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka kusoma kidogo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 15(xv) kinachoongelea miradi ya maji. Mheshimiwa Waziri anasema hivi, “hadi kufikia Juni, 2022 miradi ya maji kwa vijijini ilifikia asilimia 74.5 ukilinganisha na mwaka ya nyuma Juni, 2021 ilikuwa ni asilimia 72.3; na mijini asilimia 86.5 mwaka wa nyuma asilimia 86.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyosoma hapa kwa kweli asilimia 74 ya miradi ya maji ambayo anasema hivi: “kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji ambapo hadi kufikia Juni, 2022 imefikia wastani wa asilimia 74 kutoka mwaka wa nyuma asilimia 72.3.” Tafsiri yake nini? Maana yake ukitembea katika vijiji 100, vijiji 70 vina huduma ya maji. Nilipoona hii ripoti nikajiuliza, kwa hiyo, ni sisi Momba tu ndio tumesahaulika ama! Nikaanza kuuliza baadhi ya Wabunge wenzangu ambao na wenyewe wanatoka kwenye majimbo ya vijijini kama jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza Wabunge zaidi ya 20 hapa, hakuna Mbunge hata mmoja ambaye ameniambia yeye kwenye jimbo lake amefikisha hata asilimia 50 ya upatikanaji wa maji. Swali langu, sisi tunajenga nyumba moja, tuko hapa kuwatumikia Watanzania, hata Mama Samia sera yake anasema anataka kumtua mwanamke ndoo kichwani, nia yake ni ya dhati na nzuri zaidi kwa ajili ya kutaka kuwasaidia akina mama wa nchi hii pamoja watu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhalisia huu siyo wa kweli. Nitolee tu mfano wa jimbo langu, mimi nina vijiji 72. Katika vijiji 72, yaani leo nimeona niwasiliane na Madiwani wote waseme; katika vijiji 72 ziko baadhi ya Kata hazina mradi wa maji kabisa. Sasa nikajiuliza, hiyo asilimia 74 inatoka wapi? Wako pia Wabunge wengine hizo asilimia hazijafika? Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye ukurasa wa saba…
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ni mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, nataka kumpa tu taarifa hayo anayoyasema ni ya kweli kabisa kwamba takwimu hizo zinashangaza na mimi kama Mbunge ninayetokea Dar es salaam upande wa Jimbo la Kibamba, maji ni changamoto, katika kata nyingi hakuna, kwa hiyo ni mchango mzuri na ni kweli kabisa anachokisema. (Makofi)
MWENYEKITI: Nyie wa Dar es Salaam huwa mkisimama na mkaungana na wa vijijini kuna muda hatuwaelewi sana. Hivi na nyie wa Dar es Salaam mna changamoto kweli kama za Momba? (Makofi)
Mheshimiwa malizia sekunde 30.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika vijiji 72 ni vijiji 16 tu ambavyo vina maji na vijiji 56 havina maji. Sasa najiuliza hii takwimu inatoka wapi? Sisi tunajenga nyumba moja, tuwatendee Watanzania haki. Tulienda kuomba kura kwa kutumia ilani hii na kwenye ilani hii ukurasa wa saba, samahani kidogo tu nisome mama yangu. Katika miongoni mwa vitu ambavyo ni vipaumbele ambavyo sisi tulipewa ilani tukanadi kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi inasema hivi; “Kuongeza kasi ya usambazaji wa maji safi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya 85% vijijini na zaidi ya 95% mijini.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naamini kwa sababu wanaona tumeshafika mwaka wa pili na ilani inasema 85%, wameamua waseme 74% hii ili ionekane wametekeleza, hapana sio kweli. Kupitia Bunge hili, namwomba Mheshimiwa Aweso, nataka nikafanye naye ziara kwenye jimbo langu, vijiji 10 ili kweli na vyombo vya habari vimchukue nione kama kweli atakuja na hiyo takwimu ya 76%, kwamba kweli kuna maji. Hapana sio kweli. Ahsante sana. (Makofi)