Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi leo kuwa wa kwanza kuchangia bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwanza kwa kuishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa Tabora tulikuwa na ufunguzi wa mradi mkubwa wa reli iendayo mwendo kasi (SGR). Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutujali wananchi katika miradi ambayo ni mingi sana kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye ofisi yake hii kwa jinsi ambavyo anachapa kazi na Watendaji wake. Nitakuwa na machache ya kusema, kwenye suala la kuwawezesha vijana kuna miradi ile ya vitalu nyumba na wengine wamewahi kuongelea hapa. Vile vitalu nyumba gharama yake ni kubwa, vitalu nyumba vya kawaida vinafika mpaka Milioni 12 ambavyo vijana wa kawaida hata wakimaliza kujengewa ule ujuzi hawana uwezo wa kumudu kununua vile vitalu nyumba. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iangalie hawa vijana watawezeshwa kwa nchi nzima namna gani wanaweza kupata vile vitalu nyumba kwa bei ambayo ni affordable, hawa vijana kila wakimaliza mafunzo wasikae tu bila kazi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulizungumzia suala pia la bajeti ya wenzetu upande wa DPP, wenzangu wengi waliongelea, kwenye ukomo wa bajeti tuliomba waongezewe hata Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya kuwezesha hizo Ofisi za DPP ziweze kufanyakazi, kwa sababu kwa kweli mashtaka mengi yanakawia kusikilizwa ni kwa sababu ofisi nyingi Mikoani hazina hawa wenzetu wa ofisi ya DPP. Kwa hiyo, mara nyingi wanatumika Askari wale wale wafanye upelelezi, Askari hao hao na waendeshe mashtaka. Sasa nimewahi kusema hawa Askari wakati mwingine wakifika vituoni wanapangiwa kazi zingine, inakuwa siyo rahisi wakafanyakazi za aina mbili. Kwa hiyo, Ofisi ya DPP kwa kweli inahitajika kuwa na usaidizi wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa sijatenda haki kama sintalisema hili ambalo nimelikuta jana Tabora. Nimekwenda Tabora kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la SGR nimekuta bomoa bomoa ambayo siyo ya kawaida, kwa kweli wananchi wa Tabora Manispaa Mheshimiwa Waziri Mkuu wamebomolewa sana vibanda vyao, hatukatai mimi siungi mkono Miji yetu kuwa michafu, siungi mkono kabisa, Serikali kuisafisha Miji yetu inafanya vizuri ninaunga mkono kabisa kuweka Miji yetu katika hali ya usafi. Kitu ambacho kinanisikitisha ni namna mazoezi yenyewe yanavyoendeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Tabora Manispaa, kwanza wale wa kubomoa wameenda usiku, asubuhi wananchi wale wajasiriamali na wengine wanaamka wanakuta vibanda vimebomolewa, yanatumika matingatinga usiku lakini hata kipindi chenyewe, sasa hivi watu wako kwenye mfungo wa Ramadhani, watu wako kwenye Kwaresma wanamalizia, hivi kulikuwa na haraka gani hawa wananchi wakiwa katika hali hii Mheshimiwa Waziri Mkuu, bado tuna majibu ambayo tunatakiwa kuwajibu ugumu wa maisha unaoendelea kipindi hiki na Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea hilo suala, maisha yamepanda tunafahamu vita ya Russia, tunafahamu hiyo Ukraine tunajua kinachoendelea, maisha yamepanda, sasa wananchi wanapobomolewa bila hata kusubiri basi huu mfungo basi upite. Hili limekuwa na haraka gani katika kipindi hiki? Watoto wao wanaowategemea hawa wajasiriamali wamekosa nini sikukuu wote zitakuwa ni mbaya kwao, hawa watoto wamekosa nini?

Mheshimiwa Spika, nafikiri hii approach Mheshimiwa Waziri Mkuu tuiangalie kwamba hawa tunawasaidiaje, mbona tunawasaidia hata wahalifu?

Mheshimiwa Spika, niliuliza Mtaalam mmoja wa Manispaa alinijibu kwamba walishirikishwa walikuwa wabishi kwa hiyo tumeamua tena tuwabomolee usiku, kwani kumshirikisha mtu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni nini? Wangapi wanashirikishwa hapa wanaambiwa msiue, msizini, msifanye hiki na wanaendelea kama kawaida, lakini tunawawekea mpaka Mawakili kuwatetea. Kwa mfano, kesi za mauaji bado zipo tunawawekea Mawakili, kwa nini hawa akina Mama Lishe tusiwatetee? Tuangalie approach ya namna gani tunaweza tukafanya, hawa ni Watanzania wenzetu, nchi hii ni ya kwetu sote, tuangalie approach ambayo haitakuwa ya kuwaumiza kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake sisi wengine tofauti na Watendaji wa Serikali hawa waliokuwa wananiambia jana wao ni Watendaji wa Serikali tena mmoja ni Mteule wa Rais, mimi siyo Mteule mimi wanaonifanya niwepo hapa ni wale wananchi lazima niwasemee. Kwa hiyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hatukatai kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Tabora Manispaa walioomba wanafika zaidi ya Elfu Moja, maeneo yametengwa yako kama 500, ni kama nusu tu, hawa wengine wanapelekwa wapi? Matokeo yake sasa kila siku tutakuwa ni kuombwa mitaji tu, Wabunge hawa ndiyo wanaoombwa mitaji, maana yake wale sasa kwa kuwabomolea hawana tena mitaji.

Mheshimiwa Spika, kwenye huu mradi ambao unaendelea nchi nzima huu wa SGR kwenye ripoti ya watu wa reli watajenga sehemu mbalimbali majengo na hasa kwenye vituo vikubwa yatakuwepo majengo ya biashara, mpaka shopping malls zitakuwepo mle, ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu imekuwa ni kawaida hata kwenye Halmashauri kunapotengwa maeneo ya nyumba za kufanyia biashara au vibanda vya kufanyia biashara, wanaanza wao wenyewe Watumishi wa Serikali kuanza kujigawia vile vibanda.

Mheshimiwa Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye huu mradi mkubwa hawa wananchi ambao mradi huo wa reli wa SGR utapita basi, wapewe kipaumbele kwenye maeneo ya vile vyumba ambavyo vitakuwepo kwa ajili ya biashara ili vijana wetu nao wapate ajira, kuliko hawa wenzetu wenyewe wa Serikali kuanza kuandika majina mbalimbali na kuchukua vile vibanda halafu wao ndiyo wanafanya biashara.

Mheshimiwa Waziri Mkuu nirudie kusema kwamba ofisi yako inafanyakazi nzuri na nchi yetu kwa kweli kwa kiwango kikubwa inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)