Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa nafasi hii ya pekee kuendelea kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu. Pia nikupongeze wewe mwenyewe kwa ushindi mnono ulioupata na namna unavyoliendesha Bunge hili kwa hekima na busara na kutambua nafasi za Wabunge wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ya bajeti aliyoitoa. Kwa kweli, iligusa kila mahali, imegusa uhitaji wa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoipambania nchi yake, kwa jinsi ambavyo halali anatafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wake wanafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze sana kwa upande wa Jimbo la Ushetu, katuletea shilingi 3,200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, katuletea Shilingi 1,590,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, katuletea Milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Ulewe. Kweli mama anapambana sana. (Makofi)

Mheshimia Spika, Jimbo la Ushetu, liko sehemu ya Wilaya ya Kahama, na Jimbo la Ushetu lina changamoto kubwa sana ya maji. Nikuambie kutoka Ushetu kwenda Kahama ambako mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria upo ni kama kilomita 12 tu, lakini wananchi hawa na Kata zao hawana maji kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ya Ushetu ni maji, pamoja na kazi nzuri wanayoifanya Wizara ya Maji, nakuendelea kuleta watafiti wa maji katika Jimbo la Ushetu, changamoto iliyopo ni maji hayapatikani na wanapochimba wanakutana na vumbi pale chini. Kwa hiyo, ningeomba maji ya Ziwa Victoria yaweze kuletwa kwa wananchi wa Ushetu.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, nadhani unapotoa taarifa utafuata ile miongozo ya taarifa unayoweza kutoa na siyo kwamba unataka kuchangia, Mheshimiwa Iddi Kassim.

T A A R I F A

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka nimpe taarifa mchangia kwamba mwezi wa kumi mwaka jana Wizara ilitenga kiasi cha Shilingi 99, 225,000 kwa ajili ya upembuzi yakinifu, mpaka sasa tunazungumza ni kwamba bado hata ule mchakato wa kumpata consultant haujakamilika.

SPIKA: Hizo Shilingi Milioni 99 ni kwa ajili ya Jimbo lake la Ushetu?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, la Jimbo la Ushetu.

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, unapokea taarifa hiyo?

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, taarifa hii naipokea kwa mikono miwili na kwa sababu hiyo, kuna watu walikuja pale kipindi cha nyuma pale baada ya kuuliza sana tukaambiwa kwamba ujazo wa maji ya Ziwa Victoria kwa upande hayawezi kupata uelekeo wa Jimbo la Ushetu, ni jambo la kushangaza, lakini maji hayo ya Ziwa Victoria ambayo yamechukuliwa kutoka Kahama yameenda Nzega, yameenda Tabora, yanaendelea kwenda maeneo mengine zaidi ya kilomita 200, yashindweje kuja kwa wananchi wa Ushetu ambao wanahangaika na kununua maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, toka uhuru kuna Kata hazijawahi kupata hata maji ya kisima, mfano Kata ya Bukomela, Kinamapula, Kata ya Ulewe, Kata ya Ubagwe, Kata ya Ulowa, Kata ya Ushetu, Kata ya Mapamba, Kata ya Ukune. Pamoja na hali ngumu ya maisha ya kupanda kwa vitu hawa wananchi wananunua maji dumu moja Shilingi 500. Hebu niambie maji yamepanda bei, mafuta yamepanda bei, mafuta ya kula yamepanda bei, sukari imepanda bei, lakini wananchi hawa bado wanahangaikia maji ya kunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningeomba suala hili Serikali ilifanyie kazi kwa udharura wake, wananchi hawa wanapakana sana na vijiji vilivyoko katika Wilaya ya Kahama, katika Jimbo la Kahama Mjini. Maji ya Ziwa Victoria yapo, wanashindwa kupeleka maji ya Ziwa Victoria kwa wananchi hawa waweze kufaidika? Wanashindwaje kufanya upembuzi yakinifu kwa haraka na fedha zipo kwa ajili ya Jimbo la Ushetu na wananchi wake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuomba sana hili nakujua uchapakazi wako, Mama Samia namjua uchapakazi wake, Waziri Mkuu namjua uchapakazi wake, Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu wake pamoja na watumishi wote wa Wizara ya Maji nawajua uchapakazi wao, naomba suala hili walifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ushetu ni jimbo ambalo pia ni la wakulima kwa kiasi cha asilimia 90, ni kati ya wazalishaji wakubwa sana wa mazao ya mahindi, mpunga pamoja na tumbaku lakini changamoto ni miundombinu.

Mheshimiwa Spika, eneo la Ushetu, lina wafanyabiashara wanaokuja kununua mahindi yao, wananunua mpunga wao hasa katika barabara muhimu sana ambayo tunaomba sana hii barabara itengewe fedha haraka. Barabara inayotoka Masumbwe, kilomita 124.01 inayopita Mwawomba, inayopita Nyankende, inayopita Ulewe, barabara inayopita Ubagwe na inapita Ulowa na inaunganisha Mikoa ya Shinyanga, Geita pamoja na Tabora mpaka eneo la Uyowa. Kwanini barabara hii isianze angalau kutengewa fedha za dharura ifanyiwe matengenezo ya dharura? (Makofi)

MHE NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Nicodemas Maganga.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka tu nimpe taarifa mchangiaji kwamba barabara anayoizungumzia, inaunganisha mikoa mitatu, kwa hiyo, ni ya muhimu sana hiyo barabara maana inatoka Masumbwi, Mkoa wa Geita, inakuja Ushetu ambao ni Mkoa wa Shinyanga, inakuja Mkoa wa Tabora. Kwa hiyo, tunaitegemea sana hiyo barabara Serikali ione kila namna iweze kurekebishwa hiyo barabara.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, niwakumbushe tena masharti ya taarifa. Hapa mbele mtaanza kusikia mtu akiaambiwa hiyo siyo taarifa. Mheshimiwa Cherehani, malizia mchango wako.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru lakini pia taarifa hizi ziendelee kuzipokea kwa sababu wananchi hawa sasa tunaelekea kwenye masoko, masoko ya tumbaku, ambapo magari ya wanunuzi wanahitaji watumie hizo barabara kupeleka tumbaku sokoni. Barabara ya kilomita 47 ambayo inatoka Kata ya Ulewe, inapita Kata ya Bulungwa, inaenda moja kwa moja Kahama Mjini maeneo yetu ambapo wakulima wetu wanafanyia masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kuna kilomita 30 zinazotoka Kata ya Ulowa, kupita Kata ya Ushetu mpaka Uyogo. Barabara hizi magari yanaanguka sana ya wananunuzi, inafika mahali wanunuzi hawa wanaongeza gharama za uendeshaji kwa sababu ya magari yao kukaa muda mrefu kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana eneo hili barabara hizi muhimu kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu na wananchi wote wanaozunguka maeneo hayo ziweze kutengewa fedha za matengenezo ya dharura. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kuzipandisha barabara hizi hadhi, kuzipeleka kuwa ni za TANROAD, ziweze sasa kufanyiwa matengenezo ya dharura, maeneo yote ambayo hayapitiki ili wakulima hawa waweze kusafirisha mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ambalo nataka nijikite kulichangia ni suala la ushirika. Nimpongeza sana Waziri wa Kilimo kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye ushirika. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa pikipiki zaidi ya 6,000 kwa Maafisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba suala hili tulipe kipaumbele sana hasa kwenye upande wa vyama vya ushirika. Tunahitaji wakulima wetu inapopanda bei ya pamba kwenye soko la dunia, inahitaji pia waweze kufaidika wakulima wetu. Wakati mwingine inapopanda bei ya pamba wanashindwa kufaidika wakulima wetu kwa sababu mara nyingi fedha hizi tunazolipa ziweze kulipwa moja kwa moja kwenye akaunti za wakulima wenyewe badala ya kupeleka kwenye AMCOS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu fedha zinapopelekwa kwenye AMCOS unakuta mkulima wa pamba ameshapeleka pamba yake, amelipwa, amepewa receipt, lakini mnunuzi anapokuja kupeleka fedha anakuta pamba iko kwenye godauni imejaa, bei imepanda kutoka 1,400 kwenda mpaka 1,700, mfano 1,750 mkulima afaidike na bei hii. Sasa mkulima angelikuwa analipwa kwenye akaunti moja kwa moja, mnunuzi angekuwa anapeleka fedha moja kwenye akaunti ya mkulima. Kwa hiyo, mkulima angekuwa anafaidika sana na kupanda kwa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba suala hili liangaliwe sana, namuamini sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo najua atalifanyia kazi, ninamwamini sana Waheshimiwa Waziri Mkuu najua atalifanyia kazi na nimpongeza tu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri alizofanya kwenye ushirika, amefanya kazi nzuri sana, amerudisha mali nyingi sana za ushirika, amerudisha mali nyingi, magodauni mengi, viwanda vingi, ningeoma sasa viwanda hivi viweze kufufuliwa wananchi hawa waweze kufaidika na mali ambazo zimerudishwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu mali hizi zimerudishwa lakini bado hazijaanza kuwafaidisha wana ushirika wetu, kwa sababu bado hati nyingi zimeshikiliwa na benki na ningeomba benki zitumie busara sana, kwa sababu wanashikilia hizi hati kwa sababu vyama vinadaiwa lakini wameshikilia hati sasa vyama vinashindwa kujiendesha vyama vinashindwa kutumia hivi viwanda, kwa hiyo mali zinachakaa sasa kwa nini wasikae chini wakubaliane utaratibu wa kulipa madeni yale halafu viwanda hivi vifufuliwe viendelee kufanya kazi badala ya kuendea kuvizuia matokeo yake mali zinachakaa umeshikilia hati, lakini hivi viwanda vinaendelea kuchoka na kupunguza thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo najua hili analiweza lipo ndani ya uwezo wake afuatilie hivi viwanda vyote ambavyo vimeshikiliwa hati zake na mabenki ili wakae wazungumze namna nzuri ya kuweza kufanyakazi na kuanza kurejesha ile mikopo taratibu huku wakiendelea kufanyakazi huku kuendelea kuimarisha viwanda na wakulima wanaendelea kufaidika na ushirika wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kukushukuru sana lakini niendelee kurudisha shukrani zangu pia kwa mawaziri wanafanyakazi nzuri sana, naendelea kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)