Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa na mimi napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Wizara ya Ulinzi, Mheshimiwa Waziri na jopo lake lote, napenda pia kuwapongeza Mkuu na Wakuu wa Majeshi yote ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ulinzi wa raia na Tanzania kwa jumla ndani na mipaka yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuanza kuchangia sasa hivi ni kuhusu kuvamiwa kwa maeneo ya kambi za Jeshi. Kama ilivyoelezwa na Wajumbe waliotangulia, kambi zetu nyingi zimevamiwa na maeneo ya raia. Nataka kuishauri Wizara yako Mheshimiwa Waziri tuangalie kambi ambazo zimeathirika sana na kuvamiwa na raia, tuombe Serikali tubadilishe maeneo ya kambi tupeleke maeneo mengine ambayo yapo nje zaidi na maeneo ya wananchi. Hayo ni kwa sababu ya kunusuru maisha ya wananchi waliozunguka katika maeneo yale, lakini pia usalama wa jeshi lenyewe, pamoja na vifaa vilivyokuwemo ndani ya kambi za Jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kidogo kuhusu mapato yanayopatikana na shughuli za utendaji katika majeshi. Naomba Wizara yako kwa kupitia Wizara ya Fedha kama kuna mapato yanazalishwa na majeshi yanakwenda Serikalini, basi iwekwe percent kidogo ibakie pale ili waweze kujiendesha kwa shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa limezungumzwa suala la wanajeshi wastaafu kuwa waganga wa kienyeji. Baada ya mtu kustaafu kazi ya aina yoyote, ana uhuru wa kufanya analolitaka; na uganga wa kienyeji ni fani, siyo kila mtu anaweza. Kama mtu ana fani yake, sheria haimbani kuwa mganga wa kienyeji, kuwa mshona cherehani, kuwa mtengeneza baiskeli, kuwa fuundi makenika, anaweza! Huo ni uhuru wa raia kufanya anachokipenda! Katika uganga wa kienyeji huo anapata mapato mengi kuliko mimi ninayefanya kazi Serikalini nilivyokuwa kwa wakati huo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nizungumzie kidogo suala hili la majeshi kwenda Zanzibar, kubakwa kwa demokrasia, kuingilia uchaguzi. Ninachosema, Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni Jeshi la Wananchi wote wa Tanzania kama jina lake lilivyo. Lina uhuru na lina haki ya kikatiba ya kufanya kazi popote ndani ya Jamhuri ya Tanzania kuanzia Kigoma mpaka Kisiwa Panza mpaka Tumbatu na kazi ya ulinzi ni kazi ya jeshi hili. Kwa wale ambao hawakufurahishwa na kitendo kile, mimi nawahesabu ndiyo wale ambao walikuwa wanataka kuhatarisha amani ya nchi. Kwa sisi ambao tulikuwa tunataka tuwe huru, tufanye uchaguzi kwa amani, tulifurahi sana kuwepo kwa jeshi letu la ulinzi wa Tanzania kuja kutulinda. Wananchi walifurahi, walikuwa wako huru, hawana mashaka kama walivyokuwa mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Zanzibar ilikuwa inajulikana, wakati wa uchaguzi hali ilikuwa tete, wananchi wanaogopa hata kwenda kununua sukari nje, wanashindwa. Kila asubuhi kukicha unasikia milipuko Kibanda Maiti; milipuko Darajani; milipuko, kumezungushwa uzio. Hivi ninyi mlikuwa mnataka kufanya nini hasa? (Makofi)
Mimi nauliza kulikuwa kuna nia gani na nchi yetu hata leo imekuwa jeshi kila mahali linazungumzwa. Jeshi nalipongeza wamefanya kazi nzuri, wameilinda Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano ambayo ni wajibu wao na wamelinda raia wa Zanzibar kama ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kulipongeza kwa dhati jeshi letu liendelee na juhudi zake hizo za kulinda amani ya nchi na nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa Zanzibar umefanyika kwa kufuata sheria zote za uchaguzi za Zanzibar. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye Rais wa Zanzibar, ataiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Nawashauri, tunasikia maneno mengi hapa kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, lakini kama kweli walikuwa na nguvu ya umma inayowakubali kwa nini walikataa kuingia kwenye uchaguzi na wao wana mtaji wa kutosha? Kwa nini wamekataa mechi ya marudio? Kama kweli wana mtaji wa kutosha wa wapiga kura, ilikuwa hakuna sababu ya kukataa kuingia kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Zanzibar …
TAARIFA....
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu kazi ya jeshi ni ulinzi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la ajira. Naomba kama yalivyozungumzwa, hawa vijana waliokwenda kupata mafunzo ya JKT ndio wafikiriwe kwanza katika ajira za jeshi. Pia napenda kushauri kwamba hili jeshi letu la JKT ligawe aina ya mafunzo. Kuwe na mitaala ambayo inawahusisha wanafunzi wa vyuo wanapokwenda kupata mafunzo yawe ya aina nyingine na mafunzo ya vijana wanaoandaliwa kuwa wanajeshi au askari yawe ya aina nyingine kwa maana kwamba hapa tutaepuka kuwafundisha mambo yote ya kijeshi vijana ambao baadaye watakwenda kuajiriwa kwenye taasisi nyingine za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu nyumba za askari wetu wa Jeshi, na mimi nasisitiza kwamba awamu hii nyumba zijengwe Unguja. Nashauri kutokana na uhaba wa ardhi wa Kisiwa cha Unguja, basi sijaona ramani zao lakini nashauri nyumba hizi zisiwe nyumba ndogo ndogo badala yake ziwe nyumba za ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa nyumba nyingi na baadaye eneo litakalobaki huko mbele lije litumike kwa nyumba nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu ni kubwa, limekua, tofauti na jeshi la mwaka 1964 na 1967. Kwa hiyo, kwa sababu jeshi letu limekua, lazima kutakuwa na mahitaji mengi na changamoto nyingi. Kwa hiyo, la kufanya tu ni Serikali kuongeza bajeti katika jeshi hili katika Wizara hii na ifikirie zaidi kutatua matatizo mbalimbali ya Wanajeshi wetu na hasa wakati wa kustaafu walipwe viinua mgongo vyao kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.