Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, kupitia njia ya maandishi naomba nichangie makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Awali ya yote niunge mkono mwelekeo wa makadirio ya mapato na matumizi kama yalivyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mipango na mategemeo yalivyobainisha utekelezaji wake kama tulivyodhamiria utasukuma maendeleo ya Taifa letu kwa kasi kubwa zaidi na kwenda hatua nyingine bora zaidi.

Mheshimiwa Spika, tunapoelekeza nguvu na jitihada zetu katika sekta za kiuzalishaji, nichangie suala la migogoro ya ardhi inayohusisha sekta tunazozitegemea zituvushe.

Mheshimiwa Spika, nianze na utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayotegemea sekta za kiuzalishaji; jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa ni kuondoa na kuzuia migogoro kati ya wananchi na wananchi au na wananchi na taasisi za Serikali au wawekezaji. Njia rahisi na ya haki ya kusimamia sekta hii muhimu ni kuzingatia sheria za nchi na kama sheria zina mapungufu basi ziboreshwe.

Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ya kutolea mfano ambayo migogoro inaibuka kila kukicha na usuluhishi wake unachukua miaka bila kupata muafaka ni ile ya Wilayani Muleba. Mgogoro wa ardhi katika Kata ya Rutoro, kata yenye vijiji vinne na vitongoji 16 chimbuko lake ni utendaji usiozingatia sheria za nchi zilizopo. Mwaka 2005/2006 Serikali ilipopima eneo lenye ukubwa wa hekta 50,000 na kutenga vitalu 18 kwa ajili ya kuwakodisha wafugaji vijiji tajwa hapo juu vilikuwepo. Vijiji vilikuwepo vikiwa na watu ambayo ndiyo rasilimali kuu na namba moja ya Taifa, pamoja na kuwepo vijiji hivyo wakati huo vilikuwa vimesajiliwa kisheria. Kijiji cha Rutoro mwaka 1976 kilikuwa Kitongoji cha Kijiji cha Rwigembe wakati Kata ya Ngenge ilianzishwa toka kata mama ya Rushwa. Wakati huo huo vijiji vya Kyobuheke na Misambya vilikuwa vitongoji vilivyosajiliwa chini ya Kijiji cha Ngenge mwaka 1976. Mwaka 1999 Rutoro ilipandishwa hadhi na kuwa kijiji kwa kufuata sheria za nchi. Lakini kwa kufuata sheria za nchi yetu vijiji vinne vya Rutoro, Kyobuheke, Misambya na Byengerere vikasajiliwa na kuunda Kata ya Rutoro.

Mheshimiwa Spika, utaona kuwa hata kwa mtu mgeni wa sheria usimamiaji mbovu wa sheria ndilo chimbuko na kichocheo cha mgogoro wa Rutoro. Kama ilivyo kwa mgogoro wa Rutoro, MWISA II nayo mgogoro wake umeibuka kwa makosa yale yale yaliyofanyika mwaka 2005/2006 Kata ya Rutoro. Mradi wa NARCO kupima vitalu ili kuwagawia wachungaji wa ng’ombe kwenye kata saba zenye vijiji 12 na vitongoji 19 bila kuzingatia sheria ni kuzalisha mgogoro mpya. Utawala bora kwa kuzingatia sheria unaelekeza matumizi bora ya ardhi na uhaulishaji pale inapobidi.

Mheshimiwa Spika, kiu ya NARCO na Wizara mama yake ya kuwa na maeneo mengi ya kufuga inachochea migogoro kutokana na utendaji wake usiozingatia shughuli zenye tija kubwa. Kimsingi NARCO anachofanya ni kuvamia maeneo, kupima, kuwakodisha wachungaji na kudai kodi. Shughuli yenye tija inapashwa kuanza na utendaji unaozingatia sheria, uendelezaji wa maeneo kwa kulenga ufugaji wenye tija au kuwawezesha wawekezaji wazawa ili waendeshe shughuli kwa tija au na kutafuta wawekezaji wenye uwezo mkubwa wa kiuwekezaji ili shughuli iwe na tija kwa manufaa ya wadau wote.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.