Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Nami naomba kuchangia hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri jinsi gani tunaweza kuboresha upatikana wa huduma za afya kwa Watanzania, mengi tutayajibu katika mjadala wa bajeti yetu ya Wizara ya Afya na leo niseme jambo moja ambalo lilielezwa kwenye mjadala huu nalo ni kuhusu umuhimu wa Bohari ya Dawa (MSD) kununua dawa kutoka kwa wazalishaji.
Mheshimiwa Spika, Rais wa Awamu ya Tano Mwenyezi Mungu amrehemu uko alipo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alipoingia madarakani kati ya jambo moja alilolieleza ni kututaka Wizara ya Afya kupitia MSD kununua dawa moja kwa moja kutoka viwandani au kwa wazalishaji.
Mheshimiwa Spika, tulikuja Bungeni kuleta mapendekezo kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kufanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi (Procurement Act) mwaka 2016. Kwanza tukafanya kipengele cha kuruhusu manunuzi ya dharura kwa sababu dawa ni bidhaa za kuokoa maisha. Jambo la pili kukaingizwa section 65A ambacho kinasema a procuring entity or the agency shall for the purpose of obtaining value for money in terms of price, quality and delivery. Procure goods or services directly from the manufacturer, dealer, wholesaler or service provider. Kwa hiyo, huu ndiyo msimamo wa sheria.
Mheshimiwa Spika, MSD hazuiwi na sheria kununua moja kwa moja kutoka viwandani au kwa wazalishaji, lengo kushusha gharama ya dawa. Sheria imeweka mipaka siyo tu gharama, quality (ubora) wa dawa, efficacy (ufanisi) wa dawa na upatikanaji wa dawa.
Mheshimiwa Spika, kanuni za manunuzi ya umma kwa sababu suala hili ni nyeti likaweka utaratibu maalum wa kuwezesha manunuzi ya dawa, vifaa na vifaatiba Kanuni ya kuanzia 139 hadi Kanuni ya 147 na inarudia vilevile kwamba tunayo fursa ya kununua moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, hili nafurahi tulilitekeleza.
Mheshimiwa Spika, 2017 nilipata heshima pia ya kuwa Waziri wa Afya. Tuliingia mikataba 73 na wazalishaji 46 wa dawa kutoka Uganda, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, China, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Bangladesh, India, Kenya na Tanzania. Tuka-identify aina za dawa 178 lakini pia vifaatiba 195 na vitendanishi 178. Kwa hiyo, hili suala siyo geni limeshafanyika. Lengo ni kushusha gharama ya dawa.
Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano. Baada ya utaratibu huu kuanza kutumika mfano dawa ya chanjo ya homa ya ini, hepatitis ‘B’ vaccine kabla ya kununua viwandani ilikuwa inauzwa elfu 22,000 sasa ikashuka mpaka elfu 5,300. Dawa ya sindano ya diclofenac kwa ajili ya maumivu vichupa 10 ilikuwa inauzwa Shilingi 2,000 ikashuka mpaka 800/= Dawa ya kupambana na maambukizi ya bakteria Amoxicillin miligramu 265 yenye vidonge 15 kwa supplier ilikuwa inauzwa 9,800/= ikashuka mpaka 4,000, mashuka yalikuwa yanauzwa elfu 22,000 yakashuka mpaka elfu 11,100.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili jambo na ndiyo muelekeo wa Wizara Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla ili kushusha gharama za dawa, dawa zitanunuliwa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.
Mheshimiwa Spika, wakati tunatafuta unafuu wa dawa hatuta-compromise ubora wa dawa lakini pia na usalama wa dawa. Tunafahamu hata leo ukienda kariakoo utapata shati la Shilingi 10,000 lakini kuna shati hilo hilo linauzwa Shilingi 30,000. Shati la Shilingi 10,000 linaweza likakaa siku moja la Shilingi 30,000 likadumu hata mwaka mmoja au miaka miwili. Hili ni jambo lazima pia tuli-take into consideration. Kwa hiyo, ninachotaka kumaliza Sheria ya Manunuzi ya Umma haijaweka kikwazo kwa dawa kutonunuliwa moja kwa moja viwandani.
SPIKA: Haya ahsante sana.
WAZIRI WA AFYA: Tunalifanyia kazi lakini ninachotaka kusema...
SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na sisi tutaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa salama na zenye ubora. Ahsante sana. (Makofi)