Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kukushukuru sana lakini kumshukuru sana Mungu kwa kuendelea kutupa afya njema. Bunge lako hii ni awamu nyingine ya bajeti na nitumie nafasi hii kama wenzangu waliopita walivyokwishasema, Wizara hii iko chini ya Mheshimiwa Rais tumpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ya kazi kubwa sana inayofanywa na wasaidizi wake. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake, lakini Katibu Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bunge lako kupitia Wizara hii kama itafanya kazi yake vizuri kwa namna inavyokwenda nina hakika hakuna Mbunge ndani ya Bunge hili atashindwa kurejea hapa kwa sababu hii ndiyo Wizara mama ambayo sote tunaitegemea. Kwa leo naomba nigusie maeneo mawili au matatu.
Mheshimiwa Spika, la kwanza ni eneo la TARURA. Nchi yetu ina barabara nyingi sana ambazo hazijajengwa kwa kiwango kinachostahili. TARURA wamebainisha zaidi ya kilomita 1,044,000 za kiwango cha vumbi ambazo zinatakiwa zijengwe kwa lami. Bajeti tuliyoiona safari hii tunashukuru kwamba imeongezeka kufikia angalau bilioni 800.
Mheshimiwa Spika, lakini ukienda Nyamagana peke yake tuna kilomita zaidi ya 944 ambazo hazijajengwa kwa kiwango cha lami na ni barabara mbaya kabisa. Sasa nadhani umefika wakati kwa Serikali iangalie vizuri Wizara hii ya TAMISEMI na taasisi hii ya TARURA kuhakikisha angalau tunakuwa na mpango wa miaka minne kuongeza fedha angalau zifikie angalau trilioni 1.3 mpaka trilioni 1.4. Kwa kufanya hivyo, ukitazama bajeti ya mwaka huu tumekusudia kujenga kilomita 411 peke yake za lami, lakini kuna miji ina zaidi ya kilomita hizo na mimi nishukuru sana kwa mpango wa TACTIC.
Mheshimiwa Spika, mpango wa TACTIC nafahamu uko kwenye Jiji lako la Mbeya lakini nafahamu uko kwenye Majiji ya Dodoma na maeneo mengine. Mradi huu ni sawa na mradi uliomalizika wa TSP ambao kiukweli umetuachia matokeo makubwa sana na nautarajia sana mradi huu, Mheshimiwa Waziri amesema utaanza mwezi wa Saba baada ya bajeti, nami ninayo barabara ambayo itanufaika na mradi huu, barabara ya kutoka Buhongwa kwenda Rwanima-Kishiri kupita Fumagila mpaka Igoma, lakini barabara hii ni sambamba na ujenzi wa soko la mazao ya majini na nchi kavu.
Mheshimiwa Spika, sasa hii ndiyo miradi ambayo inaweza ikatusaidia, kwanza kupunguza adha na kero kwa wananchi wetu kwa sababu Serikali inafanya mambo mengi mazuri, lakini kama hatutakuwa na barabara bora zenye sifa yote itakuwa ni kazi bure na huko ndiko wananchi wanakopata ghadhabu nyingi. Kwa hiyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na niishukuru sana Wizara yake na wasaidizi wake kwa kuliona hili na kusukuma fedha na makubaliano ya TACTIC yamefikia mwisho ili tuweze kuona sasa matokeo ya miradi hii.
Mheshimiwa Spika, siyo hilo peke yake, nigusie jingine kwenye sekta ya afya. Tumejenga vituo vya afya vingi sana, tumejenga zahanati nyingi sana kabisa na rekodi ukianzia mwaka 2017 awamu ya kwanza ilijenga vituo 44 ambavyo tunashukuru sana kwa sababu vyote vilipata vifaa tiba. Awamu ya Pili karibu 80%, hivi lakini awamu ya tatu na kuendelea vituo vingi sana havijapata vifaa tiba na kupelekea halmashauri zetu kulazimika kutafuta fedha kwa wadau na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Jiji la Mwanza peke yake Nyamagana na niombe sana Wizara ukienda Igoma toka kimekamilika leo ukienda hakina vifaa vya msingi vinavyoweza kutoa huduma, ukienda Fumagila na kule Bulale, sasa haya ni maeneo ambayo tunadhani kwa mpango huu ambao Wizara imekuja nao leo.
Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri wamefikiria vizuri kwa fedha walizozitenga kwa kuongeza kwenye vifaa tiba tufike wakati ikiwezekana bajeti ya ujenzi ipungue, irudi nusu ya tulipo sasa ili fedha nyingi tuielekeze kwenye vifaa.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu, nitoe mfano, mtu kwa mfano unaenda kwenye kituo kilichoko jirani yako karibu kilometa tano, unafika unaambiwa hatuwezi kukufanyia vipimo uende hospitali ya wilaya, unalazimika kutembea zaidi ya kilomita zingine saba, sasa kuna faida gani ya kuendelea kujenga wakati vituo vingi tulivyovijenga, zahanati na vituo vya afya havina vifaa tiba. Maana yake hapa ni kwamba hatujawasaidia wananchi. Nilikuwa naongea na Daktari mmoja anasema kwa mfano ukiwa na kituo halafu hauna tu peke yake ile mashine ya ultra sound, tunataka kupunguza vifo vya mama na mtoto, kama hatuna kifaa hiki hatuna state ya wazazi kuja kujifungua, hatuna vitanda vya akinamama kujifungulia, bado itakuwa ni kazi bure hatutapambana na wimbi la vifo vya mama na mtoto.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niishukuru sana Wizara kwa kuja na mpango huu wa kuendelea kupunguza fedha kwenye ujenzi na kuongeza fedha nyingi zaidi kwenye kupeleka vifaa ili kila mtu na siyo Nyamagana peke yake, ukienda kule Mbeya kwa mfano kwenye hospitali yako ya Igawilo ambayo imepandishwa hadhi kwenda kwenye hospitali kutoka hospitali ya kawaida kama ilivyokuwa, ina majengo mazuri lakini haina vifaa sasa hivi. Ukienda Iyumbu vile vile kituo cha afya kizuri, lakini hakuna vifaa. Kwa hiyo haya maeneo yote haya ni lazima tuwekeze nguvu ukienda Magu kwa Kiswaga na kwingine kote maeneo mengi naamini, tumeona fedha kwa ajili ya kupeleka vifaa kwenye zahanati 300 na vituo vya afya 159, tunatamani sana tuone orodha hi ili tumshauri Mheshimiwa Waziri na tuhakikishe kila eneo limeguswa ili tuweze kuwa na maana nzuri hasa ya utekelezaji wa maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ningependa sana nizungumzie habari ya machinga. Sisi tunaotoka kwenye miji mikubwa, sisi tunaotoka kwenye majiji na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ameona juzi hapa kuna kitendo ambacho nashukuru Mungu sana alikiingilia haraka na sisi tukahakikisha kwamba haya siyo malengo ya Serikali, malengo ya Serikali ni kuwapanga wafanyabiashara kwenye maeneo mazuri, wafanye biashara ili waweze kujikwamua kutoka daraja moja kwenda daraja lingine. Kwa hiyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mkuu wangu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuchukua haraka tukio la unyanyasaji la juzi ambalo lilikuwa siyo tukio zuri na naamini haya siyo malengo ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu sasa tunafikiria kwamba katika maeneo haya yote tunayoenda nayo, maeneo mengi tu wafanyabiashara wamekubali kwenda kwenye maeneo yao. Kwa mfano, nimepata milioni 500 kwenye Jimbo langu hii peke yake haitoshi kuwafanyia kuwatengenezea wafanyabiashara mazingira bora ya kukaa na kufanya biashara.
Mheshimiwa Spika, naomba waweke kipaumbele kwenye miji mikubwa Jiji la Mwanza, Mbeya, Dodoma, Tanga, Arusha, kama tumeamua kuwapanga watu hawa itengwe fedha maalum ya kuhakikisha tunaboresha maeneo. Halmashauri zetu Mheshimiwa Waziri hazijitoshelezi kuweka fedha ya kukarabati miundombinu yote. Tusukume fedha kwa wingi tuwasaidie vijana ili tuwawekee mazingira. Wamekubali kutoka barabarani na wanafanya vizuri sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: ...hata hivyo tuwalinde kwa sababu ni vijana wa Taifa la leo na tunawategemea sana.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda na Mungu akubariki sana nafahamu changamoto za Jiji la Mwanza ndizo changamoto za Jiji la Mbeya, kwa hiyo tushirikiane kuhakikisha kwamba vijana wetu na ndugu zetu wanafanya kazi vizuri na kusaidiwa sana. Mungu akubariki sana na ahsante. (Makofi)