Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Vile vile namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi ambayo amenipatia leo kuweza kuzungumza ndani ya Bunge hili tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hoja yangu kubwa ni kujikita kwenye Elimu ya Msingi, lakini napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kupitia Waziri wa TAMISEMI na Manaibu Waziri wawili, wataalam ambao tumejumuika pamoja nao hapa kwa kazi kubwa ambayo wanafanya.

Mheshimiwa Spika, nimepitia hotuba hii, ni dhahiri kwamba katika ukurasa namba 12 na 13 ni lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kutupatia fedha katika Mpango wa Maendeo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19. Jimbo letu la Busanda lilipata takribani madarasa 209 ambayo yana thamani ya shilingi bilioni 4.2. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Wizara hii kwamba tuna madarasa ya kutosha Sekondari na sasa wanafunzi wanaendelea kusoma. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Rais kupitia Wizara hii, ametupatia fedha kupitia TARURA zaidi ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya barabara. (Mkofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme wazi kwamba Wizara hii inafanya kazi kubwa na nimeona kwenye mpango kwamba fedha mwaka huu imeongezwa. Ninaamini barabara zitaendelea kujengwa vizuri kuliko ilivyofanyika mwanzo, lakini niombe sasa tuna miji yetu midogo, kwa mfano, Mji wa Katoro barabara zake nyingi hazipitiki. Naomba TARURA walichukue hili na Manaibu Waziri wote wawili wamekuja Katoro, Mawaziri amepita Katoro, ameona hali halisi iliyopo, kwamba mji ule haupitiki. Tuna shilingi 600,000,000/= ambayo ilikuwepo kutoka ardhi mji unaanza kupangwa. Tunaomba ujengwe na barabara zake zipitike ili mji uweze kuonekana ni mji mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa namba 15 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri unaonesha wazi kwamba kuna vituo vya afya 304 ambavyo vimejengwa na vinaendelea kujengwa, lakini 234 vinatokana na tozo. Tulipendekeza mwaka 2021, vituo vya kimkakati kutoka kwenye Kata zetu, mimi binafsi kwa maana ya Busanda nilipendekeza Rwamgasa, Nyakagomba na Magenge, lakini sijaviona kama vimejengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na pongezi kubwa ya kazi kubwa ambayo mnafanya, vituo hivi vya kimkakati viangaliwe kwenye maeneo yetu kutokana na jiografia. Jimbo letu la Busanda ni kubwa, nategemea kwamba mkitupatia vituo vya afya ambavyo tumevisema tutakuwa kwenye mazingira ya kuweza kuhudumia wananchi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu elimu ya msingi ambayo nilisema nataka niizungumzie, mahali popote ambapo msingi unakuwa na mashaka, ni lazima ujenzi kwenda juu, nyumba hiyo itakuwa inayumba. Elimu ya msingi ndani ya nchi hii ambayo ninaamini kwamba inasimamiwa na Wizara hii ina changamoto nyingi.

Mheshimiwa Spika, miundombinu ya elimu ya msingi Tanzania, ukipita kwenye shule za msingi utagundua mambo yafuatayo: wanafunzi ni wengi lakini madarasa ni machache. Hotuba hii inatuonesha wazi kwamba mwaka 2021 tulipanga kudahili wanafunzi kama 1,272,513 lakini tulidahili zaidi ya hapo na mwaka uliofuata ambao ni mwaka huu, tumedaili zaidi tuna asilimia 103; shule za msingi mwaka 2021 tulidahili vile vile zaidi ya asilimia102, mwaka huu tumedahili kwa asilimia 108. Maana yake hata malengo tunayoyaweka, tunazidi, wanafunzi ni wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye shule zetu za msingi ambazo tunategemea ziwe zimeandaliwa vizuri sana, kwa sababu kama hazijaandaliwa vizuri, hao walimu wanaokuja Sekondari watakuwa na kazi kubwa sana ya kushughulika na hao wanafunzi, kwa sababu wanatoka wakiwa hawana msingi wa kutosha. Kwa mfano, Jimboni kwangu kuna shule inaitwa Bwawani, ina wanafunzi 3,100 lakini ina vyumba vya madarasa sita. Sasa ukijiuliza, tunataka kuendesha shule, tunaiendeshaje shule hii? Kwamba tuna wanafunzi 301, lakini madarasa yapo sita.

Mheshimiwa Spika, tuna shule nyingine inaitwa Ibwezamagigo, ina wanafunzi 3,111, nayo ina madarasa sita. Tuna shule nyingine inaitwa Mchongomani, ina madarasa tisa lakini ina wanafunzi 3,319. Ukifikiria tu unaweza ukajua kama hapo ndipo tunapotaka kuwaandaa wanafunzi kwa maana ya msingi; tutakuwa tuna changamoto kubwa. Tutawachukua wanafunzi wengi watakaoenda kwenye Kidato cha Kwanza lakini watakuwa wana kasoro nyingi kwa sababu ya uhalisia huu ambao unaonekana huku chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ni ombi langu kwa maana ya nchi hii, huu ni mfano mdogo tu; ina maana tukiwauliza Wabunge wengi hapa kwenye maeneo yao, watagundua kabisa hakuna madawati ya kutosha, tutagundua kwamba hakuna vyumba vya madarasa vya kutosha. Hii elimu ya msingi sasa Serikali ijikite hapa, kama ilivyofanya kazi kwa Sekondari, iende sasa elimu ya msingi kuhakikisha kwamba tunaweza kuboresha, kwa sababu pamoja na madarasa kuwa machache, lakini hata walimu huko kwenye shule za msingi nao bado hawatoshi. Pamoja na kwamba tunaona sasa hivi imetangaziwa walimu wanatakiwa kuongezeka, lakini walimu hata wakiongezeka bado walimu watakuwa hawatoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, kama kuna kitu sasa tunatakiwa kufanya, tujitahidi sana kuboresha elimu ya msingi ili msingi ukiwa bora, watoto wetu wanaokwenda juu, waende wakiwa na msingi ulio bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa leo niishie hapa. Naunga mkono hoja. (Makofi)