Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa fursa kuweka mchango wangu leo kwenye Wizara hii nyeti katika maendeleo ya nchi yetu. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais mama yetu shupavu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ipo Ofisi ya Rais, kupitia Mheshimiwa Rais tumeona fedha nyingi zimepelekwa kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya miradi mbalimbali. Zimeenda fedha nyingi kwenye miradi ya afya, miradi ya elimu na miradi ya maji, hususani katika hizo huduma muhimu kwa jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa dhati kabisa ni muda wa kumpongeza na kumtia moyo sana yeye pamoja na wanaomsaidia katika hii ili tuweze kupata tija kubwa zaidi katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na fedha nyingi ambazo zinapelekwa kwenye halmashauri zetu, tuna changamoto kubwa sana ya miradi viporo, tuna miradi ya muda mrefu ambayo inasuasua. Inawezekana tunashindwa kusimamia vizuri, namna gani ambavyo tunaweza tukasaidia halmashauri zetu kuhakikisha kwamba miradi inayoanzishwa isikae muda mrefu sana bila kukamilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ili kuweza kutengeneza usimamizi mzuri, miradi inayoanzishwa iweze kukamilika kwa wakati kuna haja kubwa sana ya kuboresha kada ya Madiwani. Madiwani ndio wasimamizi wakubwa wa shughuli katika halmashauri na kwa mujibu wa majukumu yao, Madiwani ndio kiungo kati ya wananchi na halmashauri yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu mengine ambayo yameainishwa katika Kanuni za Kudumu za Madiwani namba 72(1) na (2). Madiwani wana hali mbaya, wana hali mbaya kwa sababu hawajawezeshwa kufanya kazi kwa maana ya kuzunguka kwenye kata zao, kijiji kwa kijiji kusimamia miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili Diwani aweze kufanya kazi vizuri, anahitaji kusafiri kutoka eneo moja hadi eneo lingine, lakini posho ambayo wanalipwa, ni ndogo sana na mwisho wa siku tumeishia kuwalaumu Waheshimiwa Madiwani katika maeneo yetu kwamba pengine kada hiyo ipo lakini hatuoni tija kutokana na nafasi ambayo wamepewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili tuweze kwenda kupata tija kwenye halmashauri, Wizara ya TAMISEMI, tukizungumzia TAMISEMI, tunazungumzia halmashauri zetu nchini, tunazungumzia Waheshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa kwa ujumla wake. Sasa ili waweze kuleta tija kwa nafasi zao, kuna haja ya kutazama upya, kuangalia namna gani tunaweza tukasaidia kuboresha maslahi ya Madiwani, maslahi ya Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa… (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Husna Sekiboko, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mwandabila.
T A A R I F A
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nilitaka nimpe taarifa Mheshimiwa Husna Sekiboko kuhusu maslahi ya Madiwani, nataka kumwambia kwamba kazi wanaoifanya yote hiyo lakini bado hawana mshahara na posho wanayopewa ni ndogo sana kiasi kwamba utekelezaji wa kazi kwao unakuwa mgumu. Ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Husna Sekiboko, unapokea taarifa hiyo?
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, naipokea hiyo taarifa kwa mikono miwili. Nataka nimwambie Mheshimiwa Neema, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Madiwani, kanuni 84(1) na (2) kifungu cha kwanza kinasema wajumbe wa Baraza la Madiwani watalipwa posho kulingana na mapendekezo ya halmashauri zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili tayari ni tatizo na ni kichaka baadhi ya Wakurugenzi kubana maslahi ya madiwani. Kwa maana kwamba halmashauri inasizingizia kuwa imepewa nafasi itawalipa kulingana na makusanyo au kulingana na uwezo. Hivi, ni nani alichagua kuzaliwa Mbeya, Dar es Salaam au Kakonko ambako makusanyo ni madogo, hakuna ambaye amechagua kuzaliwa Singida, wote hao wamezaliwa kwenye hayo maeneo bila kuchagua. Kwa nini walipwe kulingana na makusanyo ya halmashauri? Ikiwa wanatumika, wanafanya kazi zinazofanana katika muda wote na wanaisaidia Serikali katika majukumu ambayo yameainishwa katika kifungu cha 72A. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili Diwani aweze kufanya kazi vizuri, pamoja na posho ambayo tumeihamisha kutoka kwenye halmashauri inalipwa sasa Serikali Kuu tulete usawa, Madiwani nchi zima walipwe kama ni mshahara, sio kwenye posho waende kwenye mshahara walipwe sawa, lakini posho zao ziwe na tija hapo tutaweza kuona uwajibikaji wao na mwisho wa siku, hizi fedha ambazo tunapeleka TAMISEMI, trillions of money kwenda TAMISEMI, zitakuwa na wasimamizi wazuri na tutaona tija ya miradi ambayo tumeipelekea fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukizungumzia ten percent, ambayo tunazopeleka kwa akinamama, vijana na wenye ulemavu, msimamizi number one ni halmashauri na ndio mtekelezaji, lakini nataka nikuhakikishie wako Waheshimiwa Madiwani ambao hata hii ten percent hawajapata nafasi ya kuelimishwa vizuri na kujua namna gani wanaenda kuisimamia. Hii inatokana na nini? Ni udhaifu, tumeshawatengenezea Madiwani udhaifu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimekuwa Diwani kwa miaka mitano, tangu 2010 mpaka 2015, Mkuu wa Idara ambaye sasa anapaswa kusimamiwa na Diwani, yeye ndiyo mkubwa kwenye halmashauri. Mtendaji wa Kata ambaye ni Katibu wa Ward C Diwani ni Mwenyekiti, yeye ndiyo mkubwa kwenye kata? Kwa nini? Kinachomjengea heshima ni kipato anachopewa. Madiwani wetu siwasemi kwa ubaya, lakini wanakopa kwa watendaji, hivi leo umetoka kwa Mtendaji wa Kata, umekopa kwa Mkuu wa Idara, kesho utakwenda kumsimamia afanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna haja kuamua kwa dhati kabisa kama tunataka kuleta tija, TAMISEMI tuangalie upya kada ya Madiwani. Madiwani wapewe nafasi ya kuwajibika baada ya kuboreshewa maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kuhusiana na vifaa tiba, pamekuwa na mjadala kidogo baina ya Mheshimiwa Mabula, kuhusiana na Mheshimiwa Mzanva kuhusu vifaa tiba. lakini nataka nikupe mifano, kuna zahanati zimekamilika ni mwaka wa pili sasa hazifanyi kazi, majengo yanachakaa kwa sababu hamna vifaa tiba. Tuna vituo vya afya vimekamilika, tuna hostel, pale Magamba Wilaya ya Lushoto, inaanza kubomoka, hakuna vifaa. Sasa tukianza kujigawanya na kuamua ni wakati gani tununue vifaa tiba na wakati gani tujenge majengo tutakuwa pengine hatufanyi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ambalo nataka niishauri Serikali ni kwamba, tukamilishe miradi yote ambayo imeshaanzishwa kabla hatujaanzisha miradi mipya, ili tupate nafasi ya kuhakikisha kwamba miradi iliyopo inakamilika lakini vilevile na vifaa ambavyo vinatakiwa kwenye miradi hiyo na vyenyewe vinaweza kupelekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho nikushukuru sana lakini niendelee kuipongeza Wizara ila nitoe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, ila nitoe ombi moja kwa Wizara ya TAMISEMI watazame upya…
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga, ni jambo jipya unaanza au unamalizia sentensi?
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)