Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Suleiman Masoud Nchambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu wa Spika, wabheja sana. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kuipongeza sana nchi yetu kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya na hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. Jeshi hili zuri limetokana na matunda yetu sisi Watanzania. Ni mti mzuri umezaa Amiri Jeshi mzuri, umezaa Mkuu wa Majeshi mzuri na Wanajeshi wazuri, watiifu, hodari na wavumilivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo moja la msingi sana. Unaweza ukawa na sikio halisikii, unaweza ukawa na macho, hayaoni na unaweza ukawa na mikono, miguu, viungo vya mwili wako usijue neema hiyo aliyokupa Mungu ni neema ya aina gani. Maana katika Quran tunasema, fa‟amma bini‟imati rabbika fahaddith (na tuzisimulie neema ambazo ametupa Mwenyezi Mungu). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Wabunge hapa leo nimeshangazwa sana, sisi wengine kwa bahati nzuri treni ya siasa hatukuidandia tumeanza chipukizi darasa la tatu lakini nashangazwa sana na Bunge hili, Mbunge anasimama pengine hajui aelimishwe, this is not vocational training centre, hili ni Bunge. Watu wamekutuma hapa siyo kuja kufundishwa. Wamekutuma kuja kufanya kazi wakiamini wewe ni mwakilishi wao, unaomba kufundishwa Bungeni, haya ni mambo ya ajabu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka hata Mungu mbinguni ana jeshi lake, malaika na vimetaja vitabu vya Mungu. Jeshi letu naomba sana Mheshimiwa Mwamunyange liheshimike. Nilitegemea sana Wabunge wote tumuunge mkono Rais, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuvaa combat ya jeshi na kuanza kukimbia. Nchi zote duniani zinakimbia sisi hapa Wabunge, Bunge lililopita na Mabunge yaliyopita tulikuwa tunalalamika tunatambaa leo Magufuli anaikimbiza nchi watu wamekazana kuleta mambo ya u-baby hapa hatutakubali. Watu wamekazana kuleta mzaha hatutakubali. Watu wanataka kuleta kejeli na jeshi letu hatutakubali. Sisi wengine bado vijana, tunahitaji kuona matunda ya Taifa letu na wajukuu wetu wakute amani ya Taifa hili, jeshi halina siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mwamunyange kwamba yamesemwa mengi sana lakini mimi nataka kumwambia yeye, Maafisa na Wanajeshi haya yaacheni humu humu, tuchukue mazuri yaliyosemwa. Jeshi sehemu yoyote duniani linalo heshima ya juu sana. Wamesema baadhi ya Wabunge hapa, hawa wote wanaopiga kelele humu wakisikia risasi moja tu wanabanana mlangoni…
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Hawatakwenda ulipotokea mlipuko wakaangalie lakini jeshi linakimbilia…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nchambi naomba ukae.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Wabheja sana.
NAIBU SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Msigwa...
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri sana huyu ni kama Mchungaji mwenzangu kwa sababu na mimi Vitabu vya Mungu navijua, namheshimu sana. Naomba nisipokee taarifa yake niendelee kutiririka na mtiririko ambao naona una maslahi kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa yamesemwa mambo, silaha feki zilikuja, haya ni mambo very serious. Kama mtu anaweza akajua taarifa za ndani za jeshi, unayo Kamati ya Maadili imuite Mbunge aliyetoa kauli hiyo kwa sababu tunaporopoka hapa ziko nchi jirani zinajua…
MHE. HALIMA J. MDEE: Kuhusu utaratibu.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Kumbe jeshi letu linazo silaha feki, linaweza likafanya manunuzi ya silaha feki jambo ambalo litahatarisha…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nchambi naomba ukae, kuhusu utaratibu....
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wabheja sana lakini naomba muda wangu uulinde, dakika sita zimepotea kwa taarifa.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Halima Mdee wakati nikitoa taarifa alisema mimi siyo size yake ni kweli, wala mimi sikatai kwa sababu amemchukua dada yetu amekwenda naye kule ametushinda. Mimi wala siwezi kuona kwamba yeye hajashinda ni kweli ameshinda na mimi upande wao sijachukua mtu wa aina yangu nikamleta huku. Kwa hiyo, yeye ni mshindi, namkubalia kabisa, sawasawa aendelee na dada yetu hatuna shida.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirejee katika hoja. Ninachotaka kusema, Ndugu zangu Wanajeshi, Maafisa wa Jeshi na Mkuu wa Majeshi, Wabunge ndiyo wenye uwezo wa kuongeza fedha ama kupunguza. Wengi wamekuwa hapa wakilalamika kwamba haiwezekani jeshi likose fedha, Bunge hili Afande Mwamunyange ndilo lenye mamlaka ya kuielekeza na kuishauri Serikali itoe fedha. Sasa hawa wenzetu wanaoendelea kubeza na kudharau jeshi, jambo la silaha ambalo lilitolewa taarifa nimesema ni serious sana, naomba sana suala hili lichukuliwe na ofisi yako kuhusiana na Mheshimiwa Kubenea aliyetoa taarifa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili hatuwezi kukubali kuliingiza jeshi letu katika kashfa kwamba mpaka silaha zimekuja, zimeonekana feki, siri za Kamati ya Ulinzi na Usalama awe nazo mtu mmoja hili ni jambo la hatari sana kwa jeshi letu. Ni jambo ambalo linaweza likahatarisha hata usalama. Sehemu yoyote duniani jeshi ndicho chombo makini kinacholinda Taifa lolote. Tunao uhuru wa aina tatu. Tunao uhuru wa bendera, wa mawazo na kiuchumi lakini yote haya ni bure kama hatuna vyombo vinavyoweza kusimamia uhuru wa mawazo yetu, uhuru wa kiuchumi na hata bendera yetu kusimama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa sana niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tusiweke kejeli kwa jeshi letu. Jeshi letu linafanya kazi nzuri, tusilete jambo lolote linaloashiria kulibeza jeshi letu. Jeshi letu linafanya kazi nzuri. Tena niwaombe sana maana katika Maandiko Matakatifu ukienda katika Mhubiri 9:10 inasema, lolote unaloweza kulifanya lifanye kwa mkono wako sasa maana hakuna hekima, maarifa, busara wala shauri unaloweza kulifanya huko kuzimu uendako. Waheshimiwa Wabunge, mikono yetu ifanye mambo sasa wakati sisi ni Waheshimiwa Wabunge. Tulitengeneze jeshi letu, tulitie moyo, tulisaidie lakini tusiendelee kuwa tunazomea huku tunapuliza kwa utaratibu wa panya. Mimi nishukuru sana kwa sababu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nchambi muda wako umekwisha.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wabheja sana. Naunga mkono hoja na Mungu awabariki.