Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi leo nichangie hotuba ya Waziri wa TAMISEMI. Kwanza nianze kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya katika Taifa letu. Amenikumbusha maneno ya Biblia, ukisoma Ezra 10 mstari wa 4 inasema: “inuka sasa maana kazi hii inakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; na uwe na moyo mkuu, ukaitende.”

Mheshimiwa Spika, haya maneno yananikumbusha kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais kwa sababu ameamua kuamka; ameinuka na kazi hii inamhusu yeye na ameenda kuitenda, nasi tuko pamoja naye kuhakikisha kwamba kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kaka yangu Mheshimiwa Innocent na wasaidizi wake wawili; Mheshimiwa Dugange pamoja na Mheshimiwa David, wanafanya kazi kubwa sana kwenye wizara hii ya TAMISEMI. Tunawapongeza kwa sababu tunaona matunda makubwa ya kazi ambayo mnafanya kwenye Majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Profesa Shemdoe. Kwa kweli Profesa ni msikivu sana; tunapoenda sisi Wabunge na kazi zetu pale kwake anatusikiliza na hata ukimpigia simu anapokea wakati wowote, hata akiwa hana nafasi, anasema atapiga baadaye na kweli anafanya hivyo. Nampongeza sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa TARURA, kaka yangu Seif. Kwa kweli kaka huyu ni wa mfano sana kwetu; ni mtu anayesikiliza, ni mtu ambaye ukipeleka shida yako anatatua. Anawasiliana na watu wa wilaya kuhakikisha kwamba maeneo yetu yanakuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami sasa nichangie kidogo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nianze na posho ya Madiwani. Nimezungumza na dada yangu hapa, nami naomba niseme kwamba Madiwani wanafanya kazi kubwa sana kwenye Majimbo yetu na kwenye Wilaya zetu. Ni watu ambao wanasimamia miradi yote ambayo inapelekwa na Serikali. Utamwona asubuhi Mheshimiwa Diwani anajikokota na baiskeli yake, anaenda kuangalia mradi umefikia wapi? Leo sisi kama Wabunge ni lazima tutafakari kwa maslahi mapana sana ya hao Waheshimiwa Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuja na hesabu ndogo hapa. Tuna Madiwani 5,287; ukiwapa tu posho yao hata shilingi 800,000/= kwa mwezi, tutakuwa tunawalipa kwa mwezi shilingi bilioni 4,200. Tuki-calculate hii kwa mwaka, tutawalipa shilingi bilioni 50.7. Ninaamini kwa Serikali yetu inawezekana kuwalipa kiasi hiki Madiwani ili waweze kufanya kazi nzuri kwa ajili ya Watanzania, kwani Madiwani wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata huko Mbeya najua wanakulindia Jimbo na wanafanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba wewe unapokuwa hapa wao wanafanya kazi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba eneo linabaki kuwa salama. Kwa hiyo, niseme, sasa ni wakati muafaka wa Wizara kulichukua hili na kwenda kulifanyia kazi ili Madiwani wetu posho yao iimarike, nao hata wakienda Halmashauri kusimamia miradi, wawe na kitu ambacho wanaweza kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Madiwani wengi wanatumia baiskeli, kuna haya hapa mwanzoni wanapokuwa wameshinda watafutiwe hata mkopo wa bila riba, walau wapate pikipiki. Madiwani wanapoenda kusimamia miradi, wawe na usafiri ambao sasa ni chanya kwao kutembelea vijiji na Kata zao ili waweze kusimamia miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine naomba nizungumzie kidogo sehemu ya afya. Nimesoma Bajeti ya TAMISEMI, naishukuru sana Serikali kwa kutuletea vituo vya afya. Tuna kituo cha afya pale Busega tunajenga, Ngasamo, lakini kwa bajeti hii Waziri kwa kweli hajaweka kituo cha afya hata kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba Naibu Waziri wa TAMISEMI, kaka yangu, Mheshimiwa Dugange amekuwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, anaifahamu Kata ya Kabita. Hii ni Kata ya kimkakati yenye wapiga kura wengi sana. Ni Kata ya pili kwa wingi wa wapiga kura katika Jimbo la Busega. Ni muda muafaka sasa Serikali ione Kata hii ya mkakati kuipelekea kituo cha afya. Najua hatuwezi kujenga kila Kata lakini walau Kata za kimkakati tuweze kupata kituo cha afya. Nami ukiniuliza leo, nitakwambia kwa Jimbo la Busega kipaumbele kianze pale Kabita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha pili, kwenye Jimbo langu la Busega tuna maboma mengi ya zahanati wananchi wamejenga. Tuna zaidi ya maboma 15, lakini kwenye bajeti hii nimeona ukamilishaji wa maboma ya zahanati katika Jimbo la Busega imepangiwa zahanati moja ambayo itakamilishwa. Sasa kuna haja ya kuhakikisha kwamba tunaongeza walau tufanye kama ilivyokuwa mwaka wa fedha huu unaoisha tupate zahanati tatu ili tuweze kuzipunguza zile zahanati ambazo wananchi wameanzisha. Wananchi wanatumia gharama kubwa, wanajitoa kwa mioyo, muda mwingine hawapati chakula, wanahakikisha kwamba wanatoa michango kwa ajili ya kujenga zahanati. Sisi kama Serikali, kama wadau ambao wananchi wametuchagua, sasa tuweze kuwapangia fedha ili aweze kukamilisha zahanati zao. (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Simon Songe kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, anachokisema Mheshimiwa Mbunge wa Busega ni sahihi kabisa kwamba wananchi wamejenga majengo ya zahanati, vituo vya afya na madarasa ambayo wametumia nguvu zao na hata sasa yanashindwa kumaliziwa, nguvu za wananchi zinapotea bure. Ninavyosema hivyo Kituo cha Afya Msindo, Wilaya ya Namtumbo wananchi wamejenga jengo la upasuaji, mpaka sasa hivi bado hawajapata pesa ya kumalizia na jengo lile lipo kwenye hatari ya kudondoka katika msimu huu. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Lusengekile, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, naipokea.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka nichangie ni eneo la TARURA. Pamoja na pongezi ambayo nimetoa kwa kaka yangu Seif lakini bado tuna kazi kubwa ni lazima tuongeze bajeti sasa eneo hili la TARURA ili tuweze kutengeneza barabara zetu. Vijijini bado kuna kazi kubwa ya barabara. Mfano, katika Jimbo la Busega tumetengeneza barabara za Kata zetu tatu lakini kwenye makutano ya zile barabara kuna tatizo la daraja pale Mwamigongwa.

Mheshimiwa Spika, sasa ni wakati sahihi kutafuta fedha zaidi ya milioni 500 twende tukatengeneze lile daraja ili tuwe na mawasiliano ya hizi Kata tatu, Kata ya Malili, Kata ya Imalamate na Kata ya Mkula pale kwenye makutano ili kata hizi ziweze kufunguliwa ili tuweze kusafirisha mazao na tuhakikishe kwamba wananachi wanasafirisha mazao yao yakiwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna barabara inayounganisha mikoa miwili, Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Simiyu. Barabara inayoanzia pale Sayaka inapita Nyaruande inapita Badugu inaenda mpaka Dutwa mpaka kule Bariadi. eneo hili pia tulitengee fedha ili tuweze kutengeneza kama ambavyo itakuwa imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo. naunga mkono hoja. (Makofi)