Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema. Pia nichukue fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Mawaziri. Nimpongeze sana kaka yangu Bashungwa pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Nimpongeze kaka yangu Katibu Mkuu Profesa Shemdoe na timu yake nzima kwa kweli wamekuwa wasikivu na kazi kubwa inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Singida Mjini tumepata miradi ya kutosha sana ya elimu, afya, barabara na kazi inafanyika na leo tukifanya ziara tunazungumza kwa vitendo na wala siyo maneno kama ilivyokuwa awali, niwapongeze sana kwa kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye ukurasa wa 103, Serikali imezungumzia malengo mahususi yatakayotekelezwa mwaka huu wa fedha. Lengo la kwanza limezungumziwa Mfuko wa Jimbo. Wameweka nyongeza ya zaidi ya asilimia 45, ni jambo jema sana, hongereni sana. Tunatambua mchango mkubwa na CAG amesema tumetekeleza kwa asilimia 100 Mfuko wa Jimbo, ni jambo jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili tumezungumzia bima ya afya ya Madiwani, kwamba bajeti iliyopita Madiwani sasa posho zao zilikuwa zinalipwa na Serikali kupitia Serikali Kuu, ilikuwa ni jambo zuri. Wakati wanalipa hawakuwa wame- include bima ya afya, mwaka huu wametenga milioni 600 kwa ajili ya bima ya afya, hili ni jambo jema sana, Serikali imetambua eneo muhimu.
Mheshimiwa Spika, hapa kwenye eneo hili la Madiwani nataka kushauri na umetoa ufafanuzi mzuri. Nami nataka nishauri na niwakumbushe Serikali, umuhimu wa maslahi ya Madiwani ni mkubwa kuliko tunavyofikiri sisi hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unapotangazwa tu na Tume ya Uchaguzi maana yake utumishi wako umekoma, unaingia kwenye utumishi mwingine, lakini huu utumishi mwingine tunautambua kwa posho wa Madiwani, hatuutambui kwa ajira. Nataka kuiomba Serikali, utumishi huu wa Madiwani tuutambue kwa ajira ya mkataba. Ukishazungumza ajira ya mkataba maana yake huyu mtu sasa hatuzungumzii mambo ya posho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tulipoamua sisi Serikali Kuu kulipa posho za Madiwani maana yake tumeua kabisa Kanuni ile ya Baraza la Madiwani ambayo inazungumza posho. Sasa kama tumeua hii, tuje na kanuni mpya itakayozungumzia mkataba wa ajira kwa Madiwani. Mkataba wa ajira kwa Madiwani utakuwa na nyongeza nzuri ya mshahara, utakuwa na nyongeza nzuri ya kila mwaka ambayo Serikali inaongeza. Tutaondokana na haya malumbano ambayo tunaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakuna ubishi kwamba wenzetu wanafanya kazi kubwa sana na wanafanya kazi nzuri sana ya kusimamia miradi ya Serikali. Miradi yote hii na hasa mchakato wa bajeti kuanzia chini, Mwenyekiti wa Kamati ya Ward C ni Diwani lakini wataalam wake ukizungumzia mshahara wa chini sana ana TGS D, ambapo hapa unazungumzia zaidi ya laki saba na kuendelea. Sasa anamsimamiaje mtu yeye ana posho! Kwa hiyo lengo la msingi la wote kuwaweka kwenye ajira, huyu atakuwa na ajira ya kudumu na huyu atakuwa na ajira ya mkataba.
Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali tukabadilishe miongozo yetu, tuje na mwongozo ambao unaonesha dhahiri kwamba tunahitaji sasa Madiwani wetu waingie kwenye ajira ya mkataba wa miaka mitano ili wao na malipo yao yaendane na ajira.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu suala la malipo ya mshahara na tofauti na posho, ukizungumzia posho, hii siyo mandatory, posho siyo lazima, huku chini maana yake tulikuwa tunategemea makusanyo ndiyo mtu aweze kulipwa, lakini tukienda kwenye ajira ni lazima, hata Diwani anaweza kwenda kuudai mshahara wake Mahakamani kama hajapewa, kwa sababu mshahara ni sheria lakini posho hii tumetengeneza utaratibu tu wa kuwawezesha kujikimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili hapa, ni mradi wa TACTIC. Mradi huu umeanza muda mrefu sana na nimeona Serikali imeeleza vizuri katika ukurasa wa 92. Mradi wa TACTIC wa Miji 45, Singida Mjini ikiwemo. Hata hivyo, kwenye huu ukurasa wa 45 tumeelezea sana TARURA. Kazi ya TARURA ni suala la barabara. Sasa mradi huu na fedha zote hizi tukizungumzia kwenye barabara peke yake watakuwa wametubana sisi ambao tayari tulijua mradi huu unaenda kuboresha maeneo yetu ya masoko, unless otherwise sijaona kwenye bajeti, nitaomba ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri watueleze, mwanzoni component ya mradi huu wa TACTIC ulikuwa unazungumzia masoko.
Mheshimiwa Spika, pale Singida Mjini tuna Soko la vitunguu, soko lile lilikuwa linajengwa kwa kuwa soko la kimataifa linagharimu zaidi ya bilioni sita na upembuzi yakinifu umeshafanyika na sisi tumewaeleza wananchi kwamba Serikali inafikia hatua za mwisho katika kuja kukamilisha ujenzi wa soko lile la kimataifa la vitunguu, lakini humu ndani sijaona, nitaomba Serikali ije na majibu.
Mheshimiwa Spika, la pili lake, tuna soko kubwa pale la majengo ambalo nalo linatakiwa lijengwe kuwa soko la kisasa kupitia mradi huu huu wa TACTIC, sasa sijaona hapa wakizungumzia masoko, naona Miji 45 tunazungumzia habari ya barabara, lakini Miji 45 wameweka phase jambo jema sana. Sisi tuko kwenye phase ya pili, tutasubiri, lakini tutasubiri tukiwa na component zote Mji unakua, Mji ambao sisi tunatarajia uwe Jiji hauwezi ukawa Jiji kama masoko haya hatujayajenga kuwa masomo ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine nitaiomba sana Serikali au Mheshimiwa Waziri, Ofisi yetu ya Manispaa, jengo la Utawala tulishawaomba na tumeleta ramani na kila kitu, tunahitaji kujenga Jengo la Utawala ambalo linaendana na hadhi ya Singida Mjini. Kwa mazingira hayo nitaomba Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii atuzingatie tujenge Jengo la Utawala la kisasa. Sasa leo wenzangu wa Singida DC kule, wenzangu wa Itigi huko wana jengo zuri, mimi ndiyo mwenye Mji wa kisasa, una kila kitu, halafu jengo limebaki kuwa la kizamani, hapana. Niwaombe sana tuhakikishe tunaweka jengo la kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jambo jema sana. Sisi tulikuwa na changamoto ya Hospitali ya Wilaya na tukaomba Hospitali ya Mkoa ile tukabidhiwe. Hapa nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Ummy akiwa Wizara hii alitoa maelekezo hivi tunavyozungumza mwezi wa Saba kwa maelezo yao kwamba watatukabidhi majengo ya Hospitali ya Mkoa yawe Hospitali ya Wilaya na kuwa Hospitali ya Wilaya itakuwa chini ya TAMISEMI. Nataka niwaombe wenzangu wa TAMISEMI watusaidie, wametuletea fedha milioni 500 tutakwenda kujenga kituo cha afya kwenye Kata yetu ya Unyambwa ile milioni 500 waliyotuletea kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ili haya majengo ya Hospitali ya Mkoa tutakapokabidhiwa, watusaidie kuyasimamia. Hospitali ya Mkoa majengo yake yawe Hospitali ya Wilaya na hili jambo kuwa Hospitali ya Wilaya tutahitaji kuwepo na rasilimali watu, tunahitaji kuwa na watumishi wa kutosha. Wakati tunakabidhiwa tuwe na watumishi wa kuendesha Hospitali yetu ya Wilaya. Tuwe na vifaa tiba vya kuendesha Hospitali yetu ya Wilaya, tusije tukakabidhiwa majengo halafu nikarudi tena Bungeni kuja kuanza kutembeza bakuri na kuwaomba jamani naomba watumishi, naomba vifaa tiba, hapana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kazi hii ambayo tunakwenda kuifanya na kuhakikisha Jimbo letu la Singida Mjini na sasa tunataka tuweke malengo makubwa ya Jimbo hili kuwa Jiji likiambatana na Jiji la Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)