Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwenye Taifa letu ambapo mwezi wa Pili mwaka huu alipokuja Mkoa wa Mara pamoja na shughuli zote alizokuwa anazifanya, alizindua mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Bunda.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo naiomba Wizara ya Maji ni kuhakikisha kwamba zile Kata 14 zote zinapata maji kwa sababu mradi huu aliouzindua Mheshimiwa Rais ulikuwa ni mradi wa fedha nyingi na wa muda mrefu. Wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini, ni takribani kilometa tano kuona ziwa pale lakini maji bado yanatusumbua. Kwa hiyo, nawaomba watu wa Wizara ya Maji wahakikishe kwamba mradi huu unamaliza tatizo kubwa la maji ambalo tunalipata pale Bunda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili ni kuhusu fedha za UVIKO-19 ambazo kwenye Jimbo langu la Bunda Mjini lilipata takribani vyumba 51 vya madarasa ambavyo vimetekelezwa ndani ya miezi mitatu, na sasa vinafanya kazi, kwa sababu vimechukua watoto wetu kuingia madarasani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kikubwa ambacho nilitaka kukisema hapa ni kwamba watu wa TAMISEMI ni vizuri wakachukuwa mfano huu uliotumika kwenye hizi fedha za UVIKO-19, kuhakikisha kwamba miradi mingi ya vyumba vya madarasa inakuwepo kwenye Halmashauri zetu kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, hapo nyuma kabla ya fedha hizi za UVIKO-19 chumba cha darasa kilikuwa kinaweza kujengwa takribani miaka 15 ambapo leo kwa fedha hizi tumeona chumba hicho kinaweza kujengwa kwa muda wa miezi mitatu. Kwa hiyo, TAMISEMI pamoja na fedha zote hizi ambazo wanazipeleka kwenye Halmashauri, wao watoe kauli kwenye Halmashauri wakati wanapotuma fedha zao kwenda kutekeleza miradi kule.
Mheshimiwa Spika, watu wetu walioko kule chini uwezo wao wenyewe unaonyesha kwamba kujisimamia ni kazi, kwa hiyo, ni vizuri maelekezo mahususi yakatoka ili vyumba vya madarasa badala ya kujengwa kwa muda wa miaka 15 kumbe vinaweza kujengwa kwa miezi mitatu ili kupunguza tatizo hili; na kwa sababu vyumba vya madarasa vya kumalizia vipo vingi sana kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa sababu bado inaendelea kutoa fedha kwa maana ya kumalizia vyumba vile, lakini bado tatizo ni kubwa. Tunaomba TAMISEMI iendelee kutoa fedha ili vyumba hivyo viweze kukamilika na tatizo hili liendelee kupungua kwa kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie kuhusiana na TARURA. TARURA wanafanya kazi nzuri sana na hasa kwenye Jimbo langu la Bunda Mjini, muda mrefu uliopita barabara za mitaa zilikuwa hazipitiki kabisa; mitaro na barabara zake zilishaotea mpaka majani. Barabara ambayo magari yalikuwa yanaweza kuitumia Huwezi kuamini kama kuna gari lilikuwa linapita pale. Fedha tunazozipata zinapunguza tatizo, lakini bado tatizo ni kubwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililokuja kujitokeza kwenye suala hili la TARURA ni wale wakandarasi wetu wanaopewa miradi ile kuitekeleza kwenye Halmashauri zetu. Kwa mfano, Bunda Mjini pale, Mkandarasi wangu yule aliyepewa kazi pale, kasi yake bado ni ndogo sana. Vile vile fedha hizi za ujenzi wa barabara, leo unaambiwa barua ya kwanza fedha zimekuja shilingi milioni 150 kwa maana ya utekelezaji wa barabara za mitaa. Bado hizo hujajua zimeelekezwa kwenye barabara gani, kuna fedha zingine zimekuja.
Mheshimiwa Spika, bado hizo hujajua zimeelekezwa kwenye barabara gani kuna fedha zingine zimekuja. Wakati mwingine unapata wakati mgumu kwa sababu, siwezi kujua ni fedha zipi katika mradi huu na ni fedha zinazotekeleza mradi huu. Kwa hiyo, niwaombe watu wa TARURA wasimame vizuri na kwa sababu uwezo wa watu wetu hawa umeonekana bado upo chini, hivyo ni vizuri TARURA wao wenyewe wasimame imara kuzihakikisha kwamba fedha hizi zinafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais anatoa fedha kwa maana ya kuhakikisha kwamba barabara za mitaa zinakaa vizuri, halafu unapokuja kufika mwisho, atakapokuja kuangalia zile barabara akute wananchi wanamlalamikia kwenye maeneo hayo hayo, kwamba barabara hazitengenezwi, kumbe saa zingine fedha zipo na Mkandarasi hajafanya kazi hiyo. Kwa hiyo ni jambo ambalo nawaomba TARURA wasimame vizuri hapa na Wizara hii ya TAMISEMI, wasimamie wakandarasi wetu vizuri ili waweze kutekeleza miradi yao vizuri ili iendane na thamani halisi ya fedha zile ambazo zinazotolewa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine hapa ni kuhusiana na vyumba vya madarasa. Vyumba hivi vya madarasa vimekuwepo kwa muda mrefu ambavyo wananchi wao wenyewe walivianzisha, tunaishukuru Serikali kwa sababu inakuwa ikitoa fedha kwa maana ya kwenda kupunguza tatizo lile, lakini bado tatizo ni kubwa. Tuiombe tu TAMISEMI iongeze fedha ili vyumba vile viweze kumaliziwa na kukamilika vyote ili watoto wetu wote waweze kusoma vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu vituo vya afya. Niishukuru TAMISEMI kwa sababu tumepata fedha hapa kwa ajili ya utekelezaji wa vituo vya afya, tumepata shilingi milioni 250 ambazo tulipeleka kule kwenye Kata yetu ya Waliku ambayo sasa tunaelekea kumaliza jengo lile. Niiombe tu TAMISEMI kwamba tutakapomaliza ujenzi wa lile jengo watuletee vifaa vile ambavyo vitaendana na lile jengo ili kwamba huduma ya afya iweze kutolewa kwa wananchi wetu wale, kwa sababu jiografia ya eneo lile Kata ywa Waliku ipo pembeni, wananchi kutoka kule waje Bunda Mjini ni takribani kilomita 16.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Getere, taarifa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa kwamba siyo tu kwamba wapeleke vifaa, ni kwamba tumepewa shilingi milioni 250 kujenga vituo vya afya na bado kuna milioni 50 inakuja. Kwa hiyo tunaomba watayarishe milioni 250 zilizobaki ziwahi mapema kumaliza majengo yaliyobaki.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na Mheshimiwa Getere kwa sababu tunatoka Wilaya moja taarifa yake naipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hayo matatizo ya vituo vya afya ni pamoja na zahanati ambazo zimejengwa kule Mcharo na Kijambiga ambazo na zenyewe ziko kwenye hatua ya mwisho, ambazo tutaiomba TAMISEMI itusaidie kuzikamilisha vizuri na vifaa tiba viweze kupelekwa kwenye maeneo yake yale ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jiografia ya Mji wa Bunda haijakaa vizuri sana na bado barabara zile za mitaa kama nilivyosema na zenyewe bado ni tatizo hasa barabara ile ya kutoka Guta kuja Kinyambiga, kutoka Kinyambiga kuja Kabasa, Kabasa kuja Bunda Mjini, hizo na zenyewe Wizara iweze kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mara baada ya kusema hayo, nakushuru na naunga mkono hoja. (Makofi)