Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pia niwashukuru sana Wizara ya TAMISEMI kwa kiunganishi kizuri wanachokifanya kwa wananchi wetu na kutufanya sisi Wabunge tuendelee kutiza majukumu yetu. Nitoe vile vile pongezi kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa utekelezaji mzuri ambao unaendelea kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, nina mambo matatu. La kwanza nianze kuwapongeza sana TARURA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanayoifanya kwenye maeneo yetu. Tulipiga kelele Bunge lililopita tukiona TARURA hawana uwezo, lakini baada ya kuwapelekea uwezo kila mtu ameona kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kwenye Mkoa wangu wa Simiyu, TARURA tuna maeneo makubwa ambayo yanatoa huduma hiyo, lakini changamoto kubwa ya kwanza ambayo Mheshimiwa Waziri na jopo lake niwaombe sana, hawana usafiri wa kutekeleza majukumu yao kwenye Mkoa wetu wa Simiyu. Meneja wa Mkoa anasubiriana na Mameneja wasaidizi kwenda kutekeleza majukumu na fedha wanazileta kwenye maeneo yetu. Tumeona kwenye Jimbo langu la Itilima wametuunganishia katika vivuko, eneo la Nhamango lipo kwenye mpango, Mnamala Mbugani wameshatoa fedha ujenzi unaendelea, Tagaswa ujenzi unaendelea na maeneo mengine mengi kwenye Jimbo langu ambayo yanaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika, ombi langu, unapokuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima na bahati nzuri Mheshimiwa Naibu analijua sana eneo la Mkoa wa Simiyu, unapoizungumza Itilima mtu anapotoka Golambesi kwenda Makao Makuu ya Mkoa inabidi azunguke kwenda Makao Makuu ya Wilaya ambayo ni kilomita 110 na kuna Daraja la Nyangokorwa linaungana na Wilaya ya Bariadi, wakitutengea fedha kivuko kile kikatengenezwa, wananchi wetu hawa hawatatumia gharama ya kwenda kilomita 110 kwenda kupata huduma ya kiafya kwa maana Hospitali ya Rufaa pale Nyaumata. Kwa hiyo nikuombe sana mratibu wa TARURA utusaidie katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tunapakana na Wilaya ya Magu na tunapakana na Jimbo la Sumve, kuna kivuko kinaitwa Solo ambako barabara imelimwa mpaka kwenye kivuko ukifika pale kulingana na bajeti tulizonazo ukomo unakuwa ni kidogo. Kwa hiyo wananchi wanaotaka kwenda Mwanza inabidi warudi kilomita 120 na ukitoka tena kilomita 120 kwenda Mwanza kilomita 200 jumla 320, lakini angetokea pale Solo kwenda Mwanza angetumia kilomita 95 akawa ameshafika na kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunayo ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo ni Mto Gomalong unaunganisha Kata ya Nkulu, Kata ya Mwaswale na Kata ya Laini. Nimwombe sana, maombi haya yamekuwa ya muda mrefu, yachukuliwe yafanyiwe kazi ili wananchi wanaoishi kandokando ya maeneo hayo waweze kupata huduma safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningeomba sana kwenye mtandao wa barabara kwenye Wilaya yangu ya Itilima ulioingia ni mia tano na thelathini na kitu lakini mpaka sasa tuna mia nane na kitu, kwa hiyo 256 hazipo kabisa kwenye mtandao wa barabara na wananchi, wasamaria wema wamejitolea kufungua barabara. Ningeiomba Serikali, maeneo hayo yaingizwe kwenye mpango ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, wanapotufungulia barabara hasa Wabunge tunaotoka vijijini huko, wanaongeza uchumi na wanapunguza kasi ya gharama ya usafiri kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, niwaombe sana, lakini kuna miji inakuwa kwa kasi, nina Mji unaitwa Laini, nina Mji unaitwa Migato, nina Mji unaitwa Luguru na Nyamalapa. Maeneo haya yanahitaji kupanuliwa kwa kuwa na barabara. Sasa kulingana na bajeti ya TARURA inayokuja tungeomba kama kuna uwezekano iongezwe ili wananchi wa Wilaya ya Itilima waweze kuneemeka na Serikali ya Awamu ya Sita. Maeneo haya niliyoyataja yana uchumi mkubwa wa kichochezi kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iendelee kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ni mpya, tuna kilomita moja ya lami ambayo imepangiwa, lakini pamoja na haya tuna eneo ambalo kutoka Makao Makuu kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya na barabara zetu ni za vumbi na kwa sababu tunatengeneza afya, ningeomba TARURA kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri atusaidie sana maombi maalum, kwa sababu ni hospitali imejengwa kwa gharama kubwa, sasa huduma ya barabara kwenye hili inapokosekana tayari kunakuwa na changamoto kubwa sana. Tuendelee kuomba watutengee angalau lami kilomita tano kwa kila mwaka, itatusaidia sana kuhakikisha wananchi wa eneo hilo kuelekea Nguno mpaka Nanga itatusaidia sana kuhakikisha kwamba eneo hilo limekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la afya; Wabunge wenzangu wamezungumza humu Serikali inawekeza fedha nyingi sana inawekeza kwenye vituo vya afya, zahanati kwenye hospitali. Sasa ni jambo ambalo ni la kusikitisha, tunaweka miundombinu yenye gharama na kilio chetu kikubwa kila Mbunge anayesimama tunalalamikia mambo ya afya.

Sasa najiuliza tunapozidi kuendelea ku-invest lakini bado tuna changamoto kwenye maeneo haya mengine, mfano kwa Itilima tuna Hospitali ya Wilaya mwaka jana tumetengewa milioni 500 tumelipa MSD lakini fedha hiyo bado hata, zimekuja items tano tu, sasa utajiuliza kwamba ni kitu gani tunachoendelea kukifanya katika maeneo yetu haya. Badala ya kuwa na kipaumbele tunaanza jambo moja tunamaliza tunahamia jambo lingine. Sasa nalo kama Serikali walichukue walifanyie kazi hasa kwenye maeneo hayo muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, ninacho Kituo cha Afya Zagayu, ni cha muda mrefu, kimechakaa na hakina wodi ya wazazi, watoto na akinababa wala hakina maabara. Sasa yote hiyo ni changamoto, ningeomba sana Serikali iangalie sana maeneo hayo muhimu ili iweze kutuunganisha na wananchi waendelee kupata huduma safi ili mambo yaende vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Wizara ya TAMISEMI wanatakiwa walifanyie kazi, sisi hapa tunakuwa tunatenga bajeti. Tunatenga kwenye mifuko yetu ya kilimo, kahawa, tumbaku, pamba na kadhalika, vitu vingi. Hata hivyo, katika hali ya kawaida, tukiangalia yale mazao yetu muhimu tukatengeneza kiwango cha fedha, wananchi wetu tuna mpango wa kuwa na Bima ya Afya, kwenye yale uzalishaji unaozalishwa kila Taasisi, bodi inayozalishwa tukakata percent fulani tukawapelekea wananchi, tukapeleka bima kwa afya bure, kwa maana yake yule mwananchi atakuwa amechangia kutokana na mazao yake aliyoyazalisha, atakuwa anakwenda hospitalini kwa sababu ataamini akifika pale atapata matibabu, atahudumiwa na atatoka yuko salama.

Mheshimiwa Spika, leo tunatenga kwenye tumbaku, tunatenga kwenye pamba, tunatenga kwenye korosho; mazao yote ya kimkakati tunayatengea fedha kwenda kulima. Analima huku mtu mgonjwa baada ya kumtengea fedha hizo zikamsaidia huko mbeleni.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)