Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Nami nichukue fursa hii kwanza kwa kuanza kuwatakia heri Waislam wote ambao wapo kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, na niombe kwa Mwenyezi Mungu atupokelee funga zetu na dua zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kupongeza uwasilishaji mzuri wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini pia niwapongeze vijana wenzangu hawa; Waziri pamoja na Manaibu Waziri wote wawili. Ni vijana wachapa kazi, nami nasema upele umepata mkunaji. Kazi kubwa kwenu ni kuingia field, kutokukaa ofisini, njooni mtukute kule Singida Kaskazini mwone kazi nzuri tunayoendelea kuichapa kule ambapo kimsingi inatokana na uwezeshaji ambao nyie mnaoufanya huku Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima ya kipekee naomba nichukue fursa hii kuwasilisha shukrani na pongezi nyingi za wana Jimbo la Singida Kaskazini kwa fedha nyingi walizoletewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi wa yale mabilioni tuliyosema ya Mheshimiwa Samia. Nashangaa watu wanasema fedha za UVIKO; zile siyo fedha za UVIKO, yale ni mabilioni ya Mheshimiwa Samia. Naomba hilo lirekebishwe. Tumepata fedha nyingi ambazo zimetuwezesha kujenga madarasa 67, Shule Shikizi pamoja na Sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza mwaka huu, wanafunzi wote wameripoti shule kwa awamu moja, tena wakiwa wamekaa kwenye madawati. Tumepata madawati zaidi ya 2,500, sasa haya kwa mwaka huu hata wazazi wamehamasika kuwapeleka watoto wao shuleni. Maana watu walikuwa wanahamasisha watoto wasiende shule. Mtoto anafaulu lakini anaambiwa asiende shule kwa sababu mzazi anabanwa kwenye michango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu, kwa haya mabilioni ya Mheshimiwa Samia, kwa kweli tunapaswa tumpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa matrilioni ya fedha. Kwa mazingira haya, wananchi wa Singida Kaskazini wameniomba nije hapa na zawadi kwa Mheshimiwa Rais. Wamesema wanampa Rais zawadi ya dumu 10 za asali; wanampa dumu 10 za mafuta ya alizeti; lakini wanampa na kuku wa kienyeji 50 wa Singida ili wakati anakunywa supu hii ya kuku wa kienyeji, huku anawafikiria kuwaletea zaidi na zaidi ili kuhakikisha wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje mambo machache ambayo yamefanyika pamoja na hayo madarasa. Tumepata fedha kwa ajili kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambayo tumepata fedha kwa ajili ya ICU na vifaa vingine muhimu. Mimi hili nimelitazama kwa heshima ya kipekee na ndiyo nasema sasa hapa kuna umuhimu wa kuunga mkono juhudi hizi ili tuendelee kuwatumikia wananchi wetu ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata fedha kwa ajili ya shule sekondari mpya shilingi milioni 470, Kata ya Kinyeto katika Kijiji cha Mkimbii, hili linaenda kukomboa watoto wetu ambao walikuwa wanakosa elimu kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, kwenye barabara tumepata mamilioni ya fedha. Kwa mara ya kwanza tumepata bajeti mara tatu ya kawaida, tulikuwa tunapata shilingi milioni 600; mwaka huu wa fedha tumepata shilingi bilioni 2.2. Sasa barabara zinatengenezwa na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kidogo kwamba, kuna madaraja mawili yanakula watu kila mwaka. Kuna daraja la Mgori na daraja la Pambaa. Madaraja haya naomba yafanyiwe kazi, yajengwe, yanyanyuliwe; wametengeneza zile drift, sasa maji yanapopita juu; juzi hapa katikati daraja la Mgori, mama wa watu amekwenda kujifungulia pale darajani, maana alishindwa kuvuka wakati anakwenda hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana jambo hili lifanyiwe kazi, tuhakikishe miundombinu yetu ya barabara inakaa vizuri na haya madaraja yakanyanyuliwe. Hapo hapo kwenye barabara, kuna suala hili la barabara za Miji Midogo pamoja na Makao Makuu ya Halmashauri za Wilaya. Serikali hii imetuletea shilingi bilioni mbili na mamilioni mengine mengi kujenga jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumepata fedha nyingi sana, lakini barabara zake zile ni mbaya na pia tunahitaji tuboreshe miundombinu zaidi. Hatuwezi kuwa na jengo zuri lakini barabara ni mbaya. Kwa hiyo, naomba sana Mawaziri waje watujengee mbiundombinu ya barabara katika hii Miji Midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la Madiwani linalozungumzwa hapa. Posho kwa ajili ya Madiwani; Diwani ndiyo kiungo, ndiyo msimamizi wa mamilioni haya tunayoyazungumza, shilingi trilioni 1.3, Msimamizi Mkuu alikuwa ni Diwani kule chini. Sasa unakuja kumpa posho ya shilingi 300,000; hivi nikikupa wewe Mwenyekiti hapo, itachukua hata masaa mawili bado ipo mfukoni? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, bajeti hii iwe ni mkombozi wa Mheshimiwa Diwani. Yeye anasimamia wataalam, wana mamilioni ya fedha wanalipwa. Wataalam kwa kiwango cha chini wana Degrees ambapo unakuta mshahara wake ni shilingi 700,000; shilingi milioni moja na kuendelea. Diwani analipwa posho ya shilingi 300,000; anaweza kumsimamia mtaalam huyu? Hebu tuache utani kwenye hili eneo. Mheshimiwa Waziri, usipoangalia katika hili, nitashika shilingi yako, tumkomboe Diwani. Tutunze heshima ya hawa Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kwa heshima ya kipekee, kwenye eneo la afya, nashukuru sana tumepata Vituo vya Afya viwili vinavyofanya kazi, lakini kuna Kituo cha Afya ambacho tumepata kile cha Makuro. Naomba sasa tupate vifaa tiba. Hospitali ya Wilaya ile nzuri tuliyoipata, Wilaya ya Ilongero, haina vifaa tiba, haijaanza kufanya kazi; ya Msange hakuna vifaa tiba, Mgori hakuna vifaa tiba. Hata hii Makuro tunayoikamilisha sasa, haina vifaa tiba. Naomba sana tupate vifaa tiba ili angalau sasa isiwe ni white elephants, zianze kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapo hapo, nawasilisha ombi sasa kwa Mheshimiwa Waziri. Kuna boma la Kituo cha Afya cha Ngimu, lina miaka 14 sasa, ni boma karibu limechakaa. Nakuomba sana sana, mwaka huu katika bajeti hii nione ukiniletea fedha kwa ajili ya kukamilisha lile boma la Kituo cha Afya lililokaa miaka na miaka halijapauliwa pamoja na lile la Kohama. Yamekaa miaka nenda rudi, wananchi wamejitolea kwa kuuza kuku wao, lakini sisi tumeshindwa kuwapokea, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri kwa heshima kubwa sana ulitazame hili kwa heshima ya kipekee na uniletee fedha Mheshimiwa na uje wewe mwenyewe uone ile hali ilivyo, jinsi wananchi wanavyopata taabu kule mabondeni kwenye bonde la ufa, wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya Mheshimiwa Waziri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekwisha! Ahsante sana, naunga mkono hoja. Ila upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ni mkubwa sana, hasa walimu, sekta ya afya na utawala. Naomba pia mnitazame kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)