Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kwanza niipongeze bajeti ya TAMISEMI, kwa taarifa nzuri ya utekelezaji. Utekelezaji unaakisi hali halisi tuliyoiacha huko kwenye Majimbo yetu, lakini napongeza Mpango unatupa matumaini makubwa sana. Nianze na masuala ya Kitaifa kabla ya kwenda Jimboni. Suala la kwanza katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia magari yaendayo kasi Mpango wa Dar es Salaam DARTS. Inaelezwa kwamba abiria 180,000 wanasafirishwa kwa siku na tutafikia watu milioni 2,500,000 kwa siku. Ushauri kwa Serikali, wekeza katika magari yanayotumia gesi asilia haraka sana (natural gas vehicles) haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, naishauri Serikali tunayo mahitaji ya watendaji lakini tunao watendaji wengi wamehitimu na hawajapata kazi, lakini jambo la kufurahisha kwa taarifa za uhakika Serikali imeanza kuajiri. Hata hivyo, haiwezi kumaliza kuajiri kwa mwaka huu, lakini kuna uhakika mwaka kesho na mwaka kesho kutwa itamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pendekezo langu, vijana wote ambao wako tayari waende katika Taasisi iwe afya iwe shule kusudi wajitolee; na wanapojitolea uwepo utaratibu wa kuwa-monitor na kuwa-mentor. Kusudi wanapokwenda kuajiri sasa wamchukue yule mtaalam aliyekwenda kuwa mentored na wataalam kuliko kwenda kuokoteza. Sio sawa mtu ambaye miaka sita amemaliza shule hajawahi kufundisha unampeleka kwenda kufundisha. Hii itatusaidia sisi kwamba wale vijana kuliko kwenda kuzurura wawe na kazi maalum. Huo ni ushauri wangu kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Jimbo langu na Mkoa wangu. Nashukuru kwa ajili ya Jimbo langu la Muleba Kaskazini, yote waliyotekeleza na Mpango wao. Nashukuru kwa niaba ya Wilaya yangu ya Muleba na Mkoa wangu wa Kagera. Nataka niwaeleze katika Wilaya yangu ya Muleba tunazo shule za msingi 250, za sekondari 40, tuna wanafunzi 157,372, kwetu sisi tunao wanafunzi wa sekondari 33,255. Hoja yangu ni kwamba tunahitaji Walimu wa shule za msingi, Walimu tunaowahitaji ni 1,390. Wakati ratio ya Taifa ni 1:60 Muleba ratio yetu ni 1:71, naomba wanapokuja kugawa Walimu sisi watuangalie kwa macho matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, sisi Muleba tunao watoto 23,500 ambao wanaingia form one, mwaka kesho katika mwaka kilele wa elimu bila usumbufu. Wanaopaswa kuingia darasa la tisa ni watoto 23,500. Kwa uwezekano wa ushindi wa asilimia 85, Muleba watoto 19,000 watakuwa tayari kwenda shuleni. Naomba watuangalie kwa jicho zuri na nimeiona mipango ya Serikali, tunahitaji vyumba 243 ili kuweza kuwapokea watoto hao. Nimeona mpango wa Serikali kwamba tutasaidiana kujenga na sisi Wabunge wa Muleba tumeshajiandaa, mwezi Mei tutaomba ruhusa kwa Spika tunakwenda kuanzisha ule mchezo wetu wa Bank ya Matofali. Kwa hiyo, watatukuta huko safarini aje atupe lift Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sekta ya afya. Tunavyo vijiji 166, zahanati 142 lakini vijiji ambavyo havina na kata ambazo hazina, wananchi wameshaanza, kwa hiyo kumbe Mheshimiwa Waziri atawakuta njiani. Jambo ambalo sisi hatuwezi tunao upungufu wa wataalam 505, Mheshimiwa Waziri anapogawa wataalam chonde chonde atuangalie kwa macho matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpe salamu zake Waziri kutoka Bumbile, Mazinga na Ikuza wanamshukuru kwa kutoa boti ambayo itakwenda visiwani; na nimewaambia hiyo boti inayokuja inaitwa ambulance, atuletee ambulance usafiri mwingine tutajijua. Sisi tuna square kilometer 10,200 wanasema kama kobowagabiyolengelao, wanaomba boti ya pili, 10,200 boti moja haitatosha, lakini tunashukuru kwa hicho kidogo kilipotoka kingine kitaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye sekta ya elimu. Kumbe sasa hatua tuliyofikia Tanzania kufikia 2025 watoto wote wa msingi wanaweza kwenda sekondari. Jambo lililonifurahisha katika Wizara hii kuna kauli inasema utawala bora TAMISEMI ya wananchi na Mheshimiwa Waziri wanasema you are walking the talk, kauli yako uliyoitoa juzi, ikamfanya Mbunge wa Nyamagana aende kula chakula na Mkuu wa Mkoa na yule muuza ndizi, you are walking the talk. Hata hivyo, sasa ndugu yangu akipiga watoto awapige watoto wote, yeye vijiji vyake vyote vimeandikwa chini ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kijiji changu kimoja cha Rutoro, kuna watoto asilimia 23 ndio wanafika shule asilimia zaidi ya 77 hawaendi shule, kuna shule nyingine just 53 ndio wanakwenda shule katika watoto 540, kitu gani. Ni kwamba kuna tatizo la utawala bora. Vijiji vilivyoandikishwa vya Kata ya Rutoro wamekuja watu wanafukuza watu kwenye vijiji vilivyoandikishwa. Kama ni utawala bora, a-walk the talk, aende akawaulize vijiji alivyovisajili chini ya TAMISEMI katika maeneo ya Kata nane, ni nani mwenye mamlaka ya kuja kupangua vijiji vile bila yeye kuhusishwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa Wakuu wa Mikoa wote wawe kama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, mnakaa watu mnajadiliana. Yule kijana aliyekuwa anasukuma ndizi amenipigia simu, anasema ameridhia makosa yaliyotokea amewasamehe wote. Sasa na wengine waambie kama wanasikia Mbunge anahoji, wamuite Mbunge wakae naye wajadiliane, hatuwezi kuishi kwa kebehi. Mtu anakwenda anakatakata mashamba ya watu anasema Muhaya ukimpa heka sita zinatosha, hiyo dharau isiletwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka 100 ya Nyerere, huwezi kusimama kuwabagua watu kikabila, unasema heka sita kwa Muhaya ni nyingi, nani alikuambia Muhaya hawezi kuwa na heka sita. Mimi nina zaidi ya heka 30, sio Muhaya? Hata hivyo, kwa nini tunatafuta ukabila? Hatuwezi kukubali kudharauliana, Mheshimiwa Waziri a-walk the talk, ahakikishe wale wote wanaohusika wakutane wote, Wizara zote zinazohusika, wakamalize matatizo yale, TAMISEMI ya wananchi, lakini sio wale wananchi ambao wanakuwa 75 kwenye ranking za FIFA. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)