Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu; vile vile niwashukuru Mheshimiwa Waziri na Manaibu Waziri pamoja na watendaji wa TAMISEMI kwa usikivu wenu. Usikivu huo muuendeleze kwa kuu-transform kwa watendaji ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia Wizara hii nikijielekeza katika fedha za maendeleo ambazo zinatolewa. Wizara hii inagusa moja kwa moja wananchi kule ngazi za chini. Wizara hii ni nguzo kabisa, ni kama uti wa mgongo wa Wizara zote katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza hivi kwa sababu, fedha za maendeleo zimekuwa zikipelekwa tofauti kwa Halmashauri tofauti. Kuna Halmashauri zinapata fedha zaidi ya asilimia 100 waliyoomba, kuna Halmashauri ambazo zinapelekewa fedha za maendeleo chini ya asilimia 50 ya zile fedha ambazo wameziomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anapohitimisha atueleze nini kinasababisha hivyo? Kwa sababu, tumeona kuna Halmashauri ambazo zina uhitaji mkubwa na hazipati fedha kwa wakati. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Momba imekuwa inapata fedha ndogo sana ukilinganisha na Halmashauri nyingine ambazo zipo. Kwa hiyo, tunapenda kuwe angalao na msawazo, Halmashauri zipate fedha ambazo zitawakwamua katika miradi yao ya maendeleo, ili waweze kufanya maendeleo ya Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kukosa usimamizi wenye weledi na uratibu mzuri katika Wizara hii. Ninazungumza hivi kwa sababu, kumekuwa na miradi ya maendeleo ambayo imeratibiwa toka miaka mingi na mpaka sasa haijakamilika. Miradi ambayo inakamilika lakini haitumiki na miradi ambayo inakamilika lakini katika ubora wa chini sana. Sasa hivi vyote vinaleta changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora mkawa na miradi michache mizuri, ikamilike kwa wakati ndipo tutaona thamani ya fedha ambazo tunazipeleka katika Halmashauri zetu. Kupeleka miradi mingi ambayo haimaliziki kwanza inaongeza fedha nyingi kwa sababu wakandarasi waki-stop kuna pesa wanakuja wanadai, na hii fedha wananchi wanaigharamia pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nitoe mfano. Kamati yetu ya LAAC, tulikwenda Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali; ninavyosema usimamizi, ni kwa sababu gani? Halmashauri ya Mbarali, ina mradi wa muda mrefu, lakini tumekwenda pale, kwa sababu tulitoa taarifa, ndiyo kwanza walianza kuchonga barabara, walikwenda kuchoma moto, kwa sababu kuliota nyasi nyingi sana. Wamechoma moto hadi gutters ziliungua; ujue hizo nyasi zilikuwa na urefu gani? Maana yake ni kwamba, usimamizi haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini usimamizi haupo? Wenzangu wamezungumza hapa, kuna Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji, na Madiwani. Hawa wote ni wasimamizi katika zile ngazi. Kama hatuwawezeshi, hawawezi kuangalia hii miradi vizuri kwa ufasaha.

Kwa hiyo, tuangalie namna ambavyo hawa watawezeshwa kwa namna moja au nyingine, na kuwe na mfuko wa ufuatiliaji. Huu mfuko wa ufuatiliaji utasaidia wale ambao wako katika kufuatilia waweze kwenda na kuona fedha zinazowekwa pale. Mradi wa takribani shilingi bilioni nne na zaidi haukaguliwi, hakuna anayeufuatilia! (Makofi)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Asenga Abubakari.

T A A R I F A

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji, ukweli katika Mradi wa Hospitali ya Mbarali anaouzungumzia ni mradi very serious ambao umeharibiwa na wasimamizi wa mradi ule. Namkumbusha tu kwamba, tulikuta hata bohari ya dawa imewekwa dawa ikiwa kuna joto kali sana. Hakuna vipooza joto. Kwa hiyo, anachosema ni sahihi, namwongezea taarifa hiyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Grace Tendega, unapokea taarifa?

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kwa sababu, bohari ya dawa iliwekwa sehemu za joto na wanaharibu dawa nyingi sana ambazo ni fedha za wananchi na ni dawa ambazo zingeweza kutumika. Kwa hiyo, hivi ndivyo vitu tunavyovizungumza kwamba usimamizi hakuna. Kwa hili niko serious kwa sababu, kama hamtasimamia hizi fedha takribani shilingi trilioni nane zinakwenda kule chini, tutakuta madudu makubwa yako kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumzia pia manunuzi yasiyozingatia sheria. Haya manunuzi hayazingatii sheria, lakini vilevile sheria yetu ina changamoto; unakuta bati linalouzwa shilingi 30,000/= wananunua kwa shilingi 110,000/=. Kwa hiyo, hizi ndiyo changamoto. Namwomba Mheshimiwa Waziri waangalie, kama hizi sheria zina shida walete turekebishe humu ndani ili tunusuru Watanzania pesa zile zitumike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya CAG inasema, Halmashauri 40 zilifanya manunuzi yenye thamani ya shilingi bilioni 5.37 bila ushindani. Halmashauri 59 zilifanya matumizi ya shilingi bilioni 8.86 bila idhini ya Bodi ya Zabuni na Halmashauri tatu zilitekeleza miradi isiyokidhi viwango na kusababisha hasara ya shilingi milioni 32.64. Hii maana yake ni kwamba, kama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Hitimisha hoja yako, muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha. Nawaomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, muwe mnazingatia usimamizi kwa mali za Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)