Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara hii ya TAMISEMI na Serikali za Mitaa. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kanijalia afya na nimeweza kusimama hapa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye Halmashauri yangu. Mimi ni Diwani kwenye Halmashauri ya Tabora Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuzungumzia kuhusiana na suala la wamachinga. Hili ninalizungumza kwa sababu natamani sana kuwekwe utaratibu mzuri kuhusiana na suala zima la Wamachinga. Kwa sababu pale Tabora Mjini kilichotokea kwa kweli siyo kitendo cha kiungwana. Wamachinga wale wamevunjiwa vibanda vyao tena usiku wa manane, wao wenyewe wakiwa wamelala hawana Habari, asubuhi wanakuja wanakuta vibanda vyao vimevunjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kabisa Mheshimiwa Waziri atakuwa na taarifa hii, lakini naomba nitoe ombi kwa Mheshimiwa Waziri, kama bajeti yake itakuwa imepita hapa, namwomba sana aende Tabora. Nenda Tabora ukapate uhalisia wa jambo hili, ukapate ukweli wa jambo hili, usisikilize tu peke yake watendaji wako, nenda kawasikilize na wananchi shida iko wapi? Ni kweli wametengewa eneo, lakini eneo lile ni dogo. Je, watendaji hawa wamefanya tathmini ya kujua Wamachinga ni wangapi katika Manispaa ya Tabora? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mahali walipojenga wametenga eneo la watu 500 peke yake. Tabora Mjini haina Wamachinga 500 peke yake, wapo zaidi. Pia nenda kawape watendaji wako elimu, Wamachinga ni watu gani? Kwa sababu wao wanachochukulia, Wamachinga ni wale wanaouza bidhaa tu peke yake za kawaida, lakini hawa akinamama ntilie, wamama wa mbogamboga, wamama wa matunda, wamama wanaopika chapati, mandazi, wanasema wale sio Wamachinga, sasa wale ukiwakuta barabarani unawafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, watoe mwongozo kwenye Halmashauri zetu, kama ambavyo leo tuko hapa, eneo la Wamachinga linajengwa tena kwa ustadi mkubwa na kila kitu…
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, taarifa.
T A A R I F A
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba changamoto za Tabora Manispaa ziko pia Jimbo la Kawe maeneo ya Tegeta, Magwepande na Bunju. Kwa hiyo, nakupa taarifa ili Waziri adake akijua akitoka Tabora Manispaa aende na Jimbo la Kawe kuna shida kubwa. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwaifunga unapokea taarifa?
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba dhana ya Wamachinga inaonekana viongozi wetu huko chini hawaielewi. Ndiyo maana unakuta kumekuwa na changamoto kubwa sana kiasi kwamba, kunakuwa hakuna maelewano baina ya wananchi pamoja na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ukichukuliwa utaratibu kama uliofanyika maeneo ya Morogoro; leo hapa Dodoma Wamachinga tunapita tunakutana nao mitaani, wanasubiri eneo lao special. Wale wakishagawiwa ukimkuta barabarani yule kweli unaweza ukapambana naye; lakini unaenda kupambana na mtu ambaye hata eneo la kufanyia biashara hujampa, unategemea huyu mtu anakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana na namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nenda mwenyewe kashuhudie hali halisi, vinginevyo hali ya Tabora Manispaa itakuwa haieleweki. Hali ni tete, wananchi mitaji yao imekufa kwa sababu wamevunjiwa wakati wakiwa wamelala na hawana walichokiokoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la afya. Kuna Sera ya Zahanati Kijiji kwa Kijiji. Hii sera inaonekana kwamba haitekelezwi ipasavyo. Katika Jimbo la Tabora Mjini lina kata za mjini na kata za vijijini. Katika Kata za vijijini unakuta kuna zahanati moja peke yake katika Kijiji ambacho kina vitongoji vitano ama sita.
Kwa hiyo, mtu kutoka Kitongoji kimoja kwenda Kitongoji kingine anatembea zaidi ya urefu wa kilometa tano mpaka kumi kufuata hiyo zahanati. Kwa hiyo, naomba sana, hii sera ya zahanati vijiji vyote, naomba iweze kutekelezwa. Pia mliiweka hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tunawaomba sana mtusaidie ili wananchi wetu wa vijijini nao waweze kunufaika na sera hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata moja ya Isevya; ile Kata ina watu wengi sana. Kutokana na watu wengi sana, pale kuna zahanati. Tulikuwa tunaomba sisi wakazi wa Tabora, kikiwekwa kituo cha afya pale kitaweza kusaidia wananchi wa kata za karibu kuweza kufika pale, kwa sababu pale wanazalisha mpaka watu watano mpaka tisa kwa siku. Nafahamu Mheshimiwa Waziri taarifa hii anayo, naomba utusaidie, tupelekeeni fedha mtuwekee kituo cha afya na pale ili na kile kingine kilichopo maili tano kiweze kusaidia wananchi wa eneo la kata za mjini, ili wawezze kupata huduma sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusiana na masuala ya elimu. Kwenye suala la elimu kumepelekwa fedha nyingi sana katika ujenzi wa shule hasa za sekondari, lakini shule za msingi zimesahaulika kabisa. Pale Tabora Mjini kuna shule kongwe, kama Shule ya Isike, Shule ya Msingi Gongon na Shule ya Msingi Kitete. Shule hizi ni kongwe na zimekuwa ni za zamani sana. Leo imefika mahali mabati yanavuja, mvua zikinyesha yale madarasa wanafunzi hawaingii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde, Waziri mwenye dhamana tunaomba mtusaidie, hizi shule za zamani mtusaidie kuzifanyia ukarabati. Nazungumzia shule za msingi, lakini pia msaidie kuongeza madarasa kwenye hizi shule ili wananchi wengi ambao wanaishi maeneo ya mjini watoto wao waweze kupata elimu karibu na maeneo ambayo wanakaa kuliko ilivyo hivi sasa mtoto anatoka umbali mrefu kufuata shule wakati kuna shule ambazo unaweza ukajenga madarasa na zinaweza zikasaidia watoto wetu kusoma karibu na maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)