Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu na pili nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais kwa kuendelea kufanya shughuli ya nchi yetu kwa ufasaha zaidi. Katika Jimbo la Karatu tumepata mafanikio makubwa wakati huu kwa mwaka wa fedha tulipokea bilioni 1.2 ambayo ilikuwa inaitwa hela ya Mama Samia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuliweza kupata milioni 700 kwa kukarabati sekondari kongwe ya Karatu, lakini vile vile tulipata milioni 470 kwa ajili ya shule ya kata ya sekondari ambayo inajengwa katika Kata ya Ganako. Pia tuliweza kupata milioni 500 kwa kujenga Kituo cha Afya cha Mbuga Nyekundu. Hata hivyo, niseme kwamba asubuhi Mheshimiwa Getere aliongea kwamba kule TAMISEMI kuna vifungu kwenye hizi milioni 500 tulizopokea ya Kituo cha Afya cha Mbuga Nyekundu, mpaka sasa hivi tulipokea awamu ya kwanza milioni 250, lakini awamu ya pili tumepokea milioni
250. Mpaka sasa tunapoongea, tuna zaidi ya mwezi mmoja shilingi 250 wanaendelea kusema vifungu vya kuhamisha hizo hela mpaka sasa hivi bado, sasa inashangaza kidogo, kama hela inatolewa kutoka Wizarani, halafu inaweza kuchukua siku 30 halafu huduma hiyo isiendelee, kwa kweli hii ni changamoto, mpaka leo hii tuna zaidi ya siku 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliweza kuongea katika Bunge hili kwamba, tulikuwa tuna tatizo la fidia katika eneo la uwanja wa Lake Manyara, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais wananchi wale wamelipwa zaidi ya bilioni 5.9, katika eneo hili la fidia eneo la Lake Manyara. Sisi pia tulifanikiwa kupata hela kwenye hospitali ya wilaya lakini iko hatua zaidi ya 85% na naamini kwamba inaweza kukamilika wakati wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea eneo la TARURA kidogo, hili eneo la TARURA Kwa mwaka jana tulitenga fedha, lakini kwenye hili eneo kuna changamoto kubwa. Mwaka 2010 Karatu tuliahidiwa tupate kilomita mbili za lami, lakini Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano mwaka 2015 alituahidi kilometa nane pamoja na ile ya Mheshimiwa Jakaya 2010 ikawa jumla ni kilomita 10. Mpaka sasa hivi tunapoongea kilomita zilizojengwa katika Jimbo la Karatu ni 0.6 mita, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri shahidi, toka mwaka 2019 mpaka leo hii, kuna kilometa 0.9, mpaka leo haijakamilika, ukiuliza changamoto ni nini? Barabara ilifumuliwa kutoka mwaka 2019, mpaka leo tunapoongelea mwaka 2022. Sasa nina wasiwasi sana kwenye ahadi hizi za viongozi wetu kwamba tutaendelea kupata changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Awamu ya Tano mwaka 2020 wakati akininadi mimi kama mgombea wa jimbo lile, aliweza kusema kwamba tunaweza kwenda kujenga sasa kilometa 10; kama mita 0.9 imeweza kuchukua muda wa miaka mitatu, sasa TAMISEMI ijipange, hizi ahadi za viongozi kwa mwaka wa fedha unaokuja wajipange ni namna gani wanaweza kutimiza ahadi za viongozi wetu wakuu wanaoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda kuongelea eneo hilo hilo la TARURA kwamba ufanisi wa TARURA ni changamoto kwa sababu wao bajeti inaisha mwezi wa Sita tarehe 30, TARURA wanakwenda kwenye kujenga barabara mwezi Januari au Februari. Sasa nashangaa kidogo kwa nini bajeti ikiisha TARURA isijipange kama wenzetu wa TANROADS wanavyojipanga. Nafikiri kuna changamoto TARURA kwa kujipanga, hofu yangu ni kwamba wataalam walioko TARURA bado ni wababaishaji. Nafikiri waangaliwe upya ma- engineer hawa tunaopewa huku TARURA. Nitatoa mfano, Mkoa wa Arusha tulipewa bilioni 19, lakini ufanisi wa bilioni 19 unakuwa na changamoto katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili kuna muda tulipewa milioni 500. Milioni hiyo 500 tuliambiwa kwamba inaweza kujenga kilometa moja ya lami kwa Jimbo la Karatu ilitangazwa mara nne, mtu wa chini sana aliomba kilometa ile kwa shilingi milioni 750. Sasa nashangaa kidogo kwa nini TAMISEMI wasifanye tathmini ya kutosha kuona kwamba kilometa moja ya lami inajengwa kwa kiwango gani. Nafikiri hii inakuwa ni changamoto mpaka sasa hivi mkandarasi imeshindikana kupatikana kwa kilometa moja hii ya lami ambayo wameweza kutupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujengwa kiwango cha lami kilometa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto katika watumishi; kwa Jimbo la Karatu jumla ya eneo la shule ya msingi tunahitaji watumishi 1,500 lakini walioko ni 964. Ukienda shule ya sekondari tuna upungufu wa zaidi ya 129, ukienda afya tuna upungufu wa watumishi 188. Lakini ukiangalia Wizara watakwambia sasa wameajiri, lakini Serikali iliacha kuajiri muda mrefu, kwa idadi iliyotangazwa ya waajiriwa ambao sasa wataajiriwa, hata wale tu waliostaafu kwa miaka yote Serikali haijaajiri, nafikiri idadi hiyo haitoshi. Kwa maana hiyo ina maana wenzetu wa Utawala Bora wajipange katika eneo la ajira kwamba hao wanaoajiriwa hawatatosha. Tunaomba waangalie eneo hili la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu ni mkubwa katika maeneo yetu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)