Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niendelee kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri sana zinazofanyika chini ya jemadari wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja na wenzetu wa TARURA, kuna vitu ambavyo vinashangaza sana. TARURA na TANROADS wanaishi kama watoto ambao hawajatoka baba mmoja, mama mmoja, kuna tatizo kubwa sana. Nimeshuhudia kwenye wilaya kwenye Jimbo la Kyela, wakati tuna matatizo ya madaraja, wananchi wanatembea kilomita 30 kwenda kulikuta daraja, barabara mpya ilipojengwa, madaraja mawili makubwa yamepotea wakati kuna uhitaji wa zaidi ya madaraja nane kwenye Wilaya ya Kyela. Sasa unajiuliza hivi TARURA na TANROADS ni watoto wa nani? Je, wanafanya kazi wanafanya kazi ambazo zinaendaje? Mwisho wa siku, mpaka naamini kwamba inawezekana kanuni iliyounda TARURA kuna sehemu haikuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo, TANROADS, wako hapo hapo lakini wanabeba daraja kwa sababu tu eti hiyo barabara ambayo daraja hilo lingefaa wanaoshughulikia ni TARURA. Sasa ningeomba kuwe na coordination nzuri kati ya TANROADS na TARURA, mambo yote yataenda sawa. Kwa sababu mama ameamua kupeleka na kufungua pochi yake kwa ajili ya wananchi walioko huko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote, kipindi kilichopita nilisema hapa katika wilaya zinazopata mvua kwa wingi, lakini wilaya ambayo iko chini mno, ambayo inapokea mvua zote na maji ya mvua zote kutoka milimani ni Kyela, maana yake nini? Maana yake ni kwamba, kama Kyela ipo chini madhara makubwa yapo kwenye miundombinu iliyoko kule. Sasa matokeo yake Kyela huu ni mwaka wa sita haijawahi kupata fedha za development kwenye miundombinu. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba kila barabara iliyopo kule imegeuka kuwa ni sehemu ya kupitisha maji, imegeuka kuwa mto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe ni shahidi, unapita mara nyingi, mafuriko yakitokea unatuma kule vijana wako wa Red Cross, wewe unajua. Unapoenda kule Bwato, hakuna barabara, kuna daraja limejengwa pale Ngorwa, limeishia ukingoni, barabara hakuna na daraja lingine la kumalizia hakuna. Sasa ningeomba niseme hivi, nataka kujua sababu ni kwa nini Kyela imenyimwa siku zote hizo fedha za development.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwahidi Mheshimiwa Waziri, kama hajawahi kushikiwa shilingi yake, basi kesho nisipopata majibu sahihi, nitashika shilingi kwenye mshahara wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye fedha za UVIKO, Wabunge hapa watashangaa kama hawajawahi kushangaa sasa hivi watashangaa. Tulipopata fedha za kujenga madarasa 67 nilitafuta mdau ambaye alikuwa tayari kutoa bilioni 1.1 kuongeza kwenye fedha hizo kumuunga mkono Mheshimiwa Mama Suluhu Hassan. Kilichotokea mpaka leo hizo fedha mhisani ameondoka nazo na hazijafanya kazi kwa sababu ya coordination, watu kutafuta umwamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, tumefika mahali ambapo mtu anakuwa anaamua badala ya wananchi kuamua nini wanakitaka. Nataka kusema hata kama ni fedha ambayo haifai, lakini kwa vile nilikuwa najenga madarasa, mhisani alisema mnajenga 67, hizo fedha leteni tuchanganye, nitajenga madarasa 154, mwisho wa siku tumeishia 67 tu, sasa hili linasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili lazima nimshukuru sana ndugu yangu Naibu Waziri wa TAMISEMI alishughulisha sana walihangaika, lakini yule mhisani yupo anaendelea kusaidia sehemu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kimetokea hapa, katika ujenzi huu nataka nijifunze kutoka TAMISEMI, nani alisema cement inayotakiwa kutumika ni ile ya 42.5? Kila sehemu nani amewaambia? Nimejaribu kupekua kila literature kujua kuna tofauti gani, kwa nini utumie hii 42 badala ya 32? Kila sehemu unaambiwa ya 42 inatumika kwenye structural elements kama beam, lakini hili limetumika kama kivuli cha kuiba fedha. Fedha mama Samia alizitoa ili zikasaidie na wananchi, lakini nawaambia hapa ndugu zangu reflection ya fedha zile kwa wananchi haziko, walikuwa wanachukua wanapeleka kwenye makampuni, badala ya kununua kwa wazubuni walioko hapa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlaghila, muda wako umekwisha, tunakushukuru sana kwa mchango wako.

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)