Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini mimi niungane na wenzangu kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa anavyotusikiliza Wabunge tunavyokuwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano na vilio vyetu huwa anavisikia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Ndugu yangu Innocent, kwa kweli Waziri huyu sijui niseme nini kwenye Bunge lako hili tukufu. Ni kijana msikivu, lakini ni kijana ambaye anaelewa matatizo ya kila Mbunge kwenye jimbo lake, ni kijana ambaye simu yake saa 6, saa 8 za usiku anakupokelea simu; kwa hiyo, tumpongeze sana na Mungu ambariki. Lakini vilevile wasaidizi wake wamekuwa ni marafiki sana kwa Wabunge wote wawili, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nishukuru katika jimbo langu nimepata shilingi milioni 440 za madarasa ya sekondari, naishukuru sana Serikali, namshukuru Mheshimiwa Rais. Lakini nashukuru nimepata shilingi milioni 260 kwa kituo cha afya pale Kata ya Ufukoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nianzie kwa kituo cha afya. Kituo hiki cha Afya ili kikamilike kinahitaji lazima tuwe na jiko ambalo linawezekana likawepo pale lakini tuwe na eneo la kufulia nguo, ambulance, sasa tayari kile kituo kimekamilika lakini wauguzi bado hatujawapata. Kwa hiyo, niombe tunapoelekea kwenye kutekeleza haya mambo adimu kwa wananchi, huduma za wananchi tunapozimaliza kwenye majengo twende kwenye huduma nyingine ya watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Jimbo la Mtwara Mjini tulikuwa tuna mradi wa kufunga taa barabarani; na mradi huu ulikuwa mwaka 2017/2018. Lakini kwenye bajeti ya mkandarasi ya malipo kwenye mradi huu ilielekezwa apewe shilingi 1,065,000,000, lakini kwa sintofaham Mkurugenzi na watumishi wengine ambao wana uwezo au wana mamlaka ya kulipa fedha hizo walilipa fedha 1,653,000,000; kuna fedha karibu milioni 588 ambazo zimelipwa nje ya mkataba. Fedha hizi ni fedha za wananchi, na CAG alishaelekeza fedha hizi zirudishwe lakini mpaka leo ninapozungumza fedha hizi zipo mikononi kwa watu na hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niishukuru Serikali hasa kupitia TARURA, lakini nataka nitoe angalizo au nitoe ushauri majimbo yapo tofauti, Jimbo la Mtwara Mjini huwezi kulinganisha na Jimbo la Nanyamba, Jimbo la Mtwara Mjini huwezi kulilinganisha na Jimbo la Kilombero, haya majimbo yapo tofauti. Lakini tunaingia kwenye migao ya fedha tunasema kwenye package ya migao ya kila jimbo TARURA tupeleke labda shilingi 1,500,000,000 au tupeleke shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo manispaa, zinakusanya almost zaidi ya shilingi bilioni 60 kwa mwaka na zipo Halmashauri hazina uwezo wa kukusanya hata shilingi milioni 200 kwa mwaka. Kwa hili mimi nilikuwa naiomba Wizara twendani tuangalie kwenye mazingira haya kama tunataka kuziinua hizi Halmashauri na manispaa basi tuangalie ni manispaa gani, Halmashauri gani ambayo ipo chini sana ili tuweze kuzisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya mradi ya TACTIC wenzangu wamezungumza, miradi hii inatakiwa iende na wakati. Jimbo la kwangu Mtwara Mjini, ikinyesha mvua leo hapa Bungeni mimi nakuwa na wasiwasi, nitapigiwa simu ngapi mafuriko! Mradi huu tunauomba uende kwa wakati kwa sababu toka tumesikia mradi huu zaidi ya miaka miwili, kila siku mazungumzo yanafanyika. Ni mazungumzo yapi yasiyokwisha? Kwa hiyo, nikuombe mtusaidie kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo la Madiwani, tulikaa kwenye Bunge letu hili hapa tukaelekeza kwamba tufike mahala kwamba Serikali Kuu mishahara yao ipitie kwenye Serikali Kuu. Lakini pamoja na hizi posho ambazo zinapita kupitia kwenye Serikali Kuu, hali ya Madiwani ni mbaya, ni mbaya. Hali ya Madiwani kwa kweli inapelekea Diwani anashinda kwenye Halmashauri utafikiri yeye labda ni mtumishi pale; sasa kwa namna moja ama nyingine Diwani huyu hawezi kwenda kuhoja chochote chenye maslahi ya wananchi kwenye eneo husika. Hili mimi naomba tuliangalie sana, Madiwani hawa waongezewe posho, wanafanyakazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nishukuru kwa Hospitali ya Rufaa pale Mtwara Mjini. Nataka niombe kwa ridhaa yako nilizungumzie hili, hospitali imejengwa pale, lakini leo tukihitaji huduma ya simu kwenye jengo lile huduma ya simu haipatikani. Lakini unapozungumza na wahusika wanakueleza kwamba mkitaka kupata mnara basi mamlaka zinazohusika zaidi ya miezi sita watoe kibali. Jamani tupo nchi gani? Kibali cha mnara mmoja kinachukua takribani miezi sita! Hivi leo tupo pale tunataka sasa tufungue ile hospitali yetu, kuna wagonjwa, Hospitali ya Rufaa itaunganisha na mkoa mmoja wa Mtwara, Lindi na Ruvuma; mtu yupo Ruvuma anataka kujua mgonjwa wake anaendeleaje tunampataje? Hebu sasa kwenye huduma hizi nikuombe tufike mahali sasa tujiwekeze kwenye mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumejenga shule na tunaishukuru sana Serikali na iendelee kutusaidia kwenye majimbo yetu. Shule hizi tayari zimeshajengwa, lakini walimu kwenye shule hizi hakuna, majengo yale yapo lakini walimu hawapo. Kwa hiyo, Serikali ichukue hatua za kila aina tuweze kupatiwa walimu kwenye haya madarasa mapya ambayo tumejenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye Jimbo la Mtwara Mjini sisi tunatofauti ya walimu shule za msingi tunataka tusaidiwe walimu zaidi ya 200 katika shule zetu za msingi. Lakini shule za sekondari katika Jimbo zima tunahitaji tupate zaidi ya walimu 300. Kwa uwiano huu mnaouona je, tuna elimu kabisa ambayo inawezekana mbadala wake watu wakapata elimu sahihi? Kwa hiyo, nilikuwa ninaliomba hilo ili tusaidiwe na sisi inawezekana tukafika mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili ni janga ambalo nataka nilizungumze wako wakandarasi wanapewa na TARURA kwenye maeneo yetu; na sielewi kwenye hii mikataba ni sheria gani ambazo zinatumika. Mkandarasi anashinda tender, anaposhinda tender kabla hajaingia site anawezekana akapewa period yake, labda ndani ya wiki mbili kwa mujibu wa sheria au mwezi mmoja haingii site. Lakini inafika takribani mpaka miezi minne, miezi mitano mpaka miezi sita mkandarasi hajaingia site, lakini tayari TARURA wameshampatia mkandarasi asilimia fulani ya mradi ule. Matokeo yake wanatuambia bwana mkandarasi ameshindwa kutengeneza barabara, lakini katika fedha ambazo tumeshampatia nadhani ana-insurance bank yatalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ni kweli tumefikia hapa na kama sheria zipo hivyo kwa nini tusiingie hapa tukabadilisha hizo sheria? Kwa hiyo, nataka nikuambie haya mambo yanafanyika na kwenye Jimbo langu ndio mchezo ambao unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwashukuru sana Mameneja wa TARURA pale wa Wilaya na ninamshukuru kwa sababu amekuwa ni mtu ambaye anapambana sana na wakandarasi na shida ipo. Kwamba, leo mkandarasi anatoka anakotoka yeye…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante ya pili, hiyo mengine andika.

Mheshimiwa Chaurembo, jiandae Mheshimiwa Sanga, jiandae Mheshimiwa Kanyasu. (Makofi)