Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia, lakini leo mchango wangu utaongozwa sana na maneno ya dini. Mtume wetu Muhammad Swalallahu Allah Wasalaam amesema; “Lamiyashukurillaha Mallam yashukurunasi” hatopatikana mtu atakayemshukuru Mungu wakati hataki kuwashukuru watu. Lakini vilevile, kwenye Zaburi 138:1 inasema; “Nitashukuru kwa moyo wangu wote na mbele ya Mungu nitakuimbia Zaburi”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza na maneno haya ya dini kwa maana, ni vyema tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya. Mwaka jana wakati kama huu nilizungumza sana kuhusiana na vilio mbalimbali katika sekta ya elimu, afya na barabara katika Jimbo langu la Mbagala. Lakini hapa ninapozungumza matatizo mengi yameenda kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika elimu msingi, shule tatu mpya zimejengwa katika Jimbo la Mbagala, yYamejengwa madarasa katika shule zilizopo zaidi ya madarasa 50, kwenye sekondari fedha za UVIKO nimepata madarasa 87, lakini mapato ya ndani tumejenga shule mpya mbili za sekondari na vilevile fedha zilizoletwa katika shule maalum nimeletewa fedha kwa ajili ya kujenga shule katika kata zisizokuwa na sekodnari. Sasa naogopa nisije nikaendelea kumshukuru Mungu bila kuwashukuru watu hawa ambao wamewezesha mambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya; sasa hivi hapa ninapozungumza kule Mbagala umeme ukikatika ukirudi tunasema huooo, sasa hivi kule Mbagala kila dakika tunasema hizooo fedha za Rais. Sasa hivi hapa wananchi wangu wananiambia hizooo shilingi bilioni mbili za kujenga Hospitali ya Wilaya zimeingia jana. Wananchi wa Mbagala wana kila namna ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa maana jana peke yake tumepata shilingi bilioni mbili za kujenga Hospitali ya Wilaya pale Mbagala Zakhiem ambayo ilikuwa ina msongamano mkubwa sana na mwaka jana nililizungumza hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vya afya; ndani ya Jimbo langu kwa mwaka huu mmoja vituo vitatu vya afya vinajengwa ambavyo vina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.5; zahanati kila kata sasa hivi tunakwenda kuwa na zahanati ambayo tunakoelekea sasa, tunaelekea kwa kila Mtaa nina kila sababu ya kuendelea kumshukuru Rais wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Nabu Spika, kuhusu barabara za TARURA tumepata fedha nyingi za kutengeneza barabara zetu za TARURA. Lakini ombi ambalo limebaki kwa wananchi wa Jimbo la Mbagala upande wa TARURA na Serikali kwa ujumla, tunao ule mradi wa uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili. Tunaiomba sana Serikali kilio chetu kikubwa sasa hivi Dar es Salaam hasa Temeke na Jimbo langu la Mbagala katika Kata za Chamazi, Charambe, Mianzini, Kiburugwa, Kibondemaji, Kilungule, Mbagala Kuu, Kijichi, Mbagala pamoja na Toangoma tatizo letu kubwa sasa hivi ni barabara. (Makofi)
Kwa hiyo, niombe sana ule mradi unaotokana na uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili, uharakishwe ili matatizo ya watu wa Mbagala yaende kuwa historia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie utekelezaji wa miradi hii yote ambayo Mheshimiwa Rais ameileta. Niwashukuru sana kuanzia Wenyeviti wa Mitaa, Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. Kazi nzuri wameifanya katika kusimamia miradi hii na ndio maana leo hii tunasimama kifua mbele kusifia miradi imefanyika vizuri.
Sasa hapa ombi langu Wenyeviti wa Mitaa wanafanya kazi kubwa na nzuri sana, sasa hivi kila jambo unalolitaka, lazima upige simu kwa Diwani au Mwenyekiti wa Mtaa akuelezee uhalisia wa maeneo hayo. Nitakupa mfano wakati tunapata fedha za kujenga vituo vya afya kwa haraka haraka ilionekana maeneo ya kujenga hakuna, lakini tulipowapigia simu Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa wametuonesha maeneo mengi ambayo yametengwa na Serikali kwa ajili ya huduma za jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuone tayari ni namna gani watu hawa walivyokuwa muhimu, lakini tuangalie na maslahi ambayo wanayapata. Nikuombe sana Wenyeviti hawa wa Serikali za Mitaa tutengeneze mazingira mazuri ya kuweza kupata maslahi yao hasa posho. Ninaamini Mheshimiwa Waziri hapa anasikia na anaweza akatoa maelekezo huko baadaye, kuhakikisha Wenyeviti hawa wa Mitaa walau tunawaongezea morale ya kufanya kazi. Anuani za makazi hizi tunazozishughulikia sasa hivi ambao wako mstari wa mbele ni Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani. Sasa niombe sana Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji nao waone namna ambayo tunaweza tukawaongeza maslahi yao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Madiwani; mimi nilikuwa Diwani, ili tuwe na Madiwani wazuri ni lazima pia tuangalie maslahi yao. Tumeanza Udiwani tukiwa tunalipwa shilingi 120,000 lakini sasa hivi imefika shilingi 350,000; ndugu zangu kutokana na hali halisi ya maisha ya sasa hivi bado ni fedha ndogo sana. Tuwaombee Madiwani hawa waongezewe fedha ili nao waweze kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa NaibU Spika, nimalizie, tuna suala zima la kujifunza Madiwani, tuombe TAMISEMI ielekeze Mikoa, Madiwani pale ambapo Halmashauri zao zina fursa za kutosha wapewe nafasi ya kwenda kujifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi hapa Dodoma inatengenezwa open market kwa ajili ya wamachinga. Kule Dar es Salaam tuna tatizo kubwa sana la wamachinga, ni wakati muafaka sasa Madiwani wa maeneo tofauti tofauti, wakaenda maeneo mbalimbali kujifunza ili mradi waone namna wenzao wanavyofanikisha mambo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini hili Mheshimiwa Waziri atalitolea maelezo ili mradi tu kama fedha wametenga kwenye bajeti zao na fedha wanazo, sioni kwa nini wawe na vikwazo vya kupewa ruhusa ya kwenda kujifunza katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)