Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuongelea Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyotangulia wenzangu kusema Wizara hii inaongozwa na vijana na kwa sababu inaongozwa na vijana wanahaja ya kuacha alama katika Taifa hili, Mheshimiwa Bashungwa watu wengi wamekushauri na mimi pia nakushauri, kuna mambo yanafanyika ndivyo sivyo usipoyasimamia lawama itakupata na utaharibu jina lako na vizazi vinavyofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia TAMISEMI na hasa kwenye eneo la elimu; elimu ndiyo msingi wa maisha na elimu huanzia kwenye msingi, usipotengeneza jamii yako na hasa kwenye elimu ya msingi kwa watoto wadogo kuanzia hapo unakuwa hujajenga Taifa bora. Mimi ninaamini watu waliosoma elimu nzuri toka elimu ya msingi ndiyo wanaofanya vizuri mpaka sasa. Lakini kumekuwa na uzembe wa Serikali kutokusimamia elimu ya msingi kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti ya CAG ya mwaka 2022 inayoishia mwezi wa tatu inasema idadi ya walimu wa shule za msingi wanaohitajika ni zaidi ya walimu 40,000 lakini walimu waliopo ni 23,000 peke yake, huu ni upungufu uko chini ya 41%. Huwezi kuwa na wanafunzi ambao hawana walimu na bahati mbaya sana waathirika wakubwa ni wanafunzi wa vijijini, hao tumewaonea kwa kuwapa walimu na walimu wanaopangiwa kwenda shule za vijijini wanahama kwa visingizio mbalimbali na kuwaacha watoto wale hawana walimu.

Mimi ninasema Mheshimiwa Waziri, CAG alipoenda kufanya ukaguzi kugundua kwamba idadi hiyo ni ndogo na ninafahamu hamjaajiri zaidi ya miaka sita sasa na mnapozungumzia ajira mnaenda kwenye vyombo vya habari kusema tumetoa ajira na kutoa matangazo mengi, lakini uhalisia walimu wanaoajiriwa ni wachache kuliko wanaohitajika. Ninaomba Wizara yako isimamie hili tupate elimu bora.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa dadaangu Mheshimiwa Mwakagenda kwa hoja anayoizungumzia ya ukosefu wa walimu na ni kweli kwamba foundation ya mtoto ni wale watoto wa awali wanatakiwa wapate elimu bora ya awali, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 180; sasa unaweza ukaona kwa wastani mwalimu mmoja wanafunzi 180 tatizo ni kubwa sana.

Kwa hiyo nampa taarifa kwamba aiweke hiyo kumbukumbu kwa sababu ameongelea mafunzo awali ya mtoto kumjengea msingi kwa hiyo ni tatizo kubwa sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sophia taarif.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia elimu bila malipo lengo la elimu hii mlipotoa hilo tamko ni kumsaidia mtoto wa kijijini. Elimu bila malipo mtoto asome vizuri bila michango yoyote, lakini Serikali imekuwa haipeleki fedha kwenye hizo shule kwa ajili ya kusaidia, mmetaja fedha kweli kwa umoja wake mnaweza kusema shilingi bilioni 200 tumepeleka lakini ukienda kwenye ile shule mwisho kabisa mwalimu mkuu anapata shilingi 200,000 atafanyia kazi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu hii haiwezi kuleta tija kama Serikali haiwezi kusimamia yale inayoyasema. Ripoti ya CAG hiyo hiyo ya Machi, 2022 inasema zaidi ya Halmashauri 22 zilizofanyiwa utafiti walikuwa wanahitaji vitabu takribani vitabu 6,000,000 lakini shule hizo zimepata vitabu 1,400,000 tu peke yake unaona upungufu wa vitabu kwenye hizo shule kati ya 6,000,000 kwa 1,400,000 ni vitabu vichache sana tunaomba Wizara yako isimamie kwa sababu huwezi kupeleka watoto shuleni bila kuwa na vitabu vya kiada na ziada. Vitabu hivyo ni vya muhimu na vinavyopungua zaidi ni vitabu vya sayansi tunaomba mtusaidie katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ruzuku bila malipo ambayo inapelekwa kwenye hizo shule nimeshasema hapo mwanzo haziendi sawasawa, watoto masikini ndiyo wanakuwa waathirika, lakini udhaifu wa hizo pesa mnazopeleka kuna maeneo yanapata pesa kwa wakati kuna maeneo yanachelewa kupata pesa. Kuna upungufu zaidi ya shilingi bilioni tano katika fedha hizo mnazopeleka za uzuku kwenye hizo shule, shilingi bilioni tano ni fedha nyingi sana zinapokwenda kwa kuchelewa tunaomba mlisimamie suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa walimu ni changamoto kubwa sana tumesema hapo mwanzo lakini uwiano wa walimu, amenipa hapa mwongozo uwiano wa walimu sawa sawa na ripoti ya CAG, kuna baadhi ya wamefanya research kuna mahali walimu wanatakiwa 1,300,000 lakini walimu wapo wachache zaidi ya upungufu wa walimu 20,000 mimi ninaomba Mheshimiwa Waziri ulisimamie hilo kwa sababu upungufu na hizo ni Halmashauri chache zilifanyiwa research upungufu wa walimu zaidi ya 20,000 ni wengi sana. Tunaomba muajiri kwasababu wasomi wapo waliosoma tayari na wanazunguka mtaani, hawana kazi, tunaomba tuwaajiri watu wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wanaojiandikisha shule ya msingi wanajiandikisha kwa wingi na ninafahamu Serikali imejenga madarasa mengi na watoto wanajiandikisha, lakini katika umaliziaji wa shule elimu ya msingi watoto wengi hawamalizi shule tunaomba mfuate utaratibu kwa Maafisa Elimu wa Wilaya, Mikoa kujua ni sababu gani zinazowafanya watoto wasimalize elimu ya msingi na tumekuwa na watoto mitaani wengi sana ambao sio lugha nzuri kuwaita watoto wa mitaani kwa sababu mtaa hauzai lakini mwisho wa siku watoto wengi wanazurura mitaani, hawana mwelekeo na wakati huo hapa Bungeni tunazungumzia elimu bora, tunazungumzia kujenga madarasa lakini mijini hata hapa Dodoma kuna watoto wanaopita na kuombaomba na sisi kama viongozi tunawaona, hatuchukui hatua yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie ucheleweshwaji wa ruzuku au fedha za maendeleo katika Halmashauri zetu, shilingi bilioni 54.06 bakaa ambayo ilibaki kwa mwaka 2019/2020 zilichelewa kurudi kwenye Halmashauri na katika fedha hizo zilizochelewa karibia bakaa kati ya hizo shilingi bilioni 15 zilikuwa na Mfuko wa Barabara. Sasa usipopeleka na ukapeleka kwa kuchelewa fedha za maendeleo ya Halmashauri tunazungumzia barabara kwa maana ya TARURA ina maana wakulima ambao wao wameshalima na kupata mazao wanategemea wasafirishe kwa barabara hizo hawatasafirisha, na kama barabara ni mbovu wachuuzi wanaokwenda kununua bidhaa hizo mikoani na vijijini lazima bidhaa itakuwa bei juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba fedha za Halmashauri zirudi kwa wakati na wala tusione zikicheleweshwa kwa sababu zisizokuwa za rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ucheleweshwaji huo wa fedha za maendeleo umekuwa ni mtindo wa muda mrefu sana kwa sasa, tunaomba mzisimamie lakini sio tu hivyo wito ambao mimi niwawapa Hazina, Hazina iweze kutoa fedha kwa wakati, kama fedha zimekusanywa na zimekwenda Mfuko Mkuu wa Serikali tunaomba fedha hizo zitolewe kwa wakati ili Mfuko wa Maendeleo wa Wilaya na Halmashauri zetu uweze kupata miradi na kuweza kufanya kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo kuna wakati mnatoa fedha wanafanya kwa hiyo tunaita fast track haraka haraka ili wakimbizane na muda wa bajeti, fedha inakuwa huwezi kupata value for money, lakini pia watu wanafanya kazi kwa haraka haraka kuitisha tender za haraka hapo na uhuni unakuwepo wa kupitisha mambo ambayo sisi kama wasimamizi wa fedha za Serikali hatupendi kuona zinafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwenzangu hapa amezungumzia suala la ukatili wa kijinsia suala hili limekuwa ni kilio kikubwa sana na kwenye ripoti yako umeizungumzia idadi iliyotajwa ya wanawake na watoto wanaonyanyasika ni kubwa sana kama Taifa tusiposimama ina maana hatuna taifa bora hapo baadaye, wanawake mara nyingi tumesikia kwenye vyombo vya habari na tunafahamu sehemu za vijijini hawana vyombo vya habari itakuwaje wanawake wanauwawa wanawake wanapigwa tu kwa sababu hawana usimamizi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, malizia.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: … hasa Serikali za Mitaa lakini pia na Wizara husika Kamati imetoa ombi juu ya fedha za UVIKO ambazo zilitolewa tunaomba Wizara yako iundwe kamati…

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: …ili fedha hizi zihakikishwe kama kweli zilifanya kazi iliyotakiwa na wala hawaja divert mradi huu. Ahsante