Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja hii ya Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Waziri na watalaam wake wote kwa namna ambavyo wamewasilisha hoja hii. Naomba na mimi niseme tu kwamba napongeza kama wenzangu wote walivyopongeza na pongezi zote zilizotolewa ni za kweli na ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwanza nataka kuongelea juu ya upungufu wa vyumba vya madarasa lakini lazima ni declare interest kwamba mimi jimbo langu nila vijijini yaani hata pale Makao Makuu ya Chemba bado panaitwa kijijini. Sasa labda nitoe takwimu kidogo mahitaji ya vyumba vya madarasa kwenye jimbo langu kwa ujumla ni vyumba 1,562 lakini vilivyopo ni vyumba 700 tu maana yake ni nini? Kuna upungufu wa zaidi ya asilimia 50 na ukweli ni kwamba watu wa vijijini tunafahamiana kwamba ni watu maskini, uwezekano wa kujenga vyumba hivi vingi vyote hivi haiwezekani, kama tulivyofanya kwenye sekondari lazima tuje na mkakati wa makusudi wa kuangalia namna gani tunaweza kwenda kuongeza vyumba hivi vya madarasa hivi shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi ambao aliufanya wa kuidhinisha zile fedha za UVIKO zitumike katika kujenga madarasa ya sekondari. Kwa hoja ile ile mimi nawashauri Wizara ya TAMISEMI lazima waje na mpango mwingine muhimu ili walau kupunguza kwa kiwango fulani upungufu mkubwa wa madarasa kwenye shule hizi za msingi. Hoja hiyo pia iendane pia na upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu mkubwa sana wa walimu lakini kuna jambo huwa najiuliza sana kwamba unaona kabisa takwimu zinaonesha labda Wilaya ya Chemba ina upungufu mkubwa zaidi kuliko wilaya nyingine, lakini wanavyokuja kuletwa walimu unaona wamegawiwa kwenye yale maeneo ambayo kuna walimu wengi zaidi. Sasa hili jambo hili nililisema mwaka jana, lakini naomba safari hii lizingatiwe kwamba ndiyo tunaenda kuajiri walimu lakini kwa nini tusiajiri walimu tukawapeleka kule ambapo kuna upungufu mkubwa zaidi. Changamoto hii inaweza ikaendelea kwamba kila siku tunaendelea kuongelea habari ya upungufu wa walimu. Mwaka huu tunaongelea upungufu walimu, walimu wanaajiriwa lakini hatuzingatii ni wapi kuna upungufu mkubwa ili walau tukapunguze gape kule kuliko kupeleka kule ambapo kuna walimu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo shule zangu za msingi zinawalimu wanne na wanafunzi 500 ninamna gani katika mazingira haya walimu hawa wanaweza kufundisha kule kijijini na ni ukweli usiopingika kwamba kuna Mbunge mmoja alitoa hoja ya msingi sana kwamba kuna umuhimu wa kuwaajiri wale walimu ambao wapo tayari kukaa kule porini. Kuna walimu wanajitolea, zilipotolewa ajira wao wakanyimwa wameendelea kujitolea na tunalazimika sisi Halmashauri au vijiji kuchanga fedha kuwalipa wale walimu kufuatana na mazingira yetu, lakini wale wanaojitolea wapo pale hawaajiriwi.
Mimi nafikiri safari hii kuwe na mkakati wa makusudi wa kuangalia kwamba huyu yupo hapa miaka mitatu anajitolea, ajira zimekuja hakuajiriwa, kijiji kinaendelea kuchanga fedha kwa ajili ya kumlipa walau kwa kumuajiri tutakuwa tumepunguza mzigo kwa wale wanakijiji waliopo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; nilitaka niongelee kidogo kuhusu na mimi naamini Mawaziri hawa vijana wanaenda kutatua changamoto hii. Kuna changamoto kubwa sana kwenye malipo ya Madiwani hasa zile stahiki ndogo ndogo kama posho, hii ni changamoto kwa Tanzania nzima. Mimi ni mjumbe wa LAAC nimejaribu kupita kwenye hizo Halmashauri unaona hapa wanalipwa vingine, hapa wanalipwa vingine. Sasa ni lazima tuje na mwongozo mmoja kwa sababu asilipwe kama hisani hali iliyopo sasa hivi malipo ya Madiwani yale ya posho yanazingatia tu namna gani yule Mkurugenzi anajisikia wakikutana na Mkurugenzi mwenye roho mbaya ni mgogoro kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nini nataka kusema lazima TAMISEMI wenyewe waje na mwongozo mmoja kwa Halmashauri zote ili kila Mheshimiwa Diwani ajue kabisa yeye anapoenda kwenye kikao stahiki zake ni zipi mgogoro huu wa malipo umeharibu sana mahusiano kati ya Mkurugenzi na Madiwani na kazi zinakwama .
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe vijana mliopo hapa ambao sisi tunawaamini sana kwamba nendeni sasa kuanzia bajeti hii andikeni waraka mmoja na futeni nyaraka nane, tisa zilizopo ambazo hazieleweki na ni kweli ukianza wewe kama Mbunge mara nyingi unajaribu kurekebisha ugomvi kati ya Wakurugenzi na Madiwani, lakini unaona kabisa Madiwani wana hoja wana waraka, Mkurugenzi naye ana waraka sasa sijui inakuwaje! Kwa hiyo, unaanza unakaa unashindwa uchukue waraka wa Mkurugenzi aliokuja nao au waraka wa madiwani waliokuja nao.
Mimi niiombe wizara kwenye bajeti hii njooni na waraka mmoja na futeni nyaraka zingine vyovyote vile ambavyo mtaona itafaa itasaidia kutuliza hali ya migogoro iliyopo kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, jambo lingine ni usimamizi wa fedha; usimamizi wa fedha kwenye miradi yetu nimesema mimi ni mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali kuna changamoto kubwa sana kwenye fedha hizi zinazopelekwa kwenye miradi, lakini pia na shida hii naiona huku TAMISEMI kwanini labda nitolee mfano mmoja tumeenda kwenye Halmashauri ya Magu kuna jengo limeanza kujengwa mwaka 2011 mpaka leo halijamalizika, lakini pia ukimuuliza Mkurugenzi anasema apewe fedha zilezile ambazo ziliandikiwa proposal mwaka huo zitamaliza kujenga jengo lile. Mimi nikamwambia hiki kitu hakiwezekani yaani wakati mfuko unauzwa shilingi 11,000 ndiyo ujenzi ulianza, leo mfuko mara mbili ya bei ile bado anasema fedha ile ikija atamaliza lile jengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nafikiri hapa kuna shida, lakini shida nyingine kubwa pale kuna mtu anaitwa Mkaguzi wa Fedha za Ndani, Mkaguzi yule yupo chini ya Mkurugenzi, ni namna gani anaweza kuandika taarifa wakati mtu anayemlipa ni Mkurugenzi? Ni lazima hivi vitu viangaliwe upya kwamba kile kitengo ni cha muhimu sana kwa sababu fedha nyingi ambazo tunapeleka pale, lakini mtu ambaye anaweza kuandika ripoti ya kweli analipwa posho na Mkurugenzi ni kwa namna gani sasa ni vipi ambavyo yeye anaweza akasimama akaandika ripoti ya aina yoyote ya kuhusu Mkurugenzi ambaye yeye ndiye anayemlipa posho anakaa kwenye dawati pale kuandika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka pia nilisemee hilo, lakini la mwisho pengine Mheshimiwa Waziri kwenye jimbo langu alipokuwa Waziri Ummy alikuja na akaahidi kutengeneza barabara ya kilometa 18 kwa kiwango cha changarawe, barabara ile ndiyo inayotumika kila siku, sasa baada ya kuwa ni ahadi ya Waziri sisi hatukuitengea fedha tulizopewa, sasa watu wakipita pale wananitukana mimi, lakini unaona wewe shida imeanza kwenu msingetuahidi mnatujengea barabara ile maana yake nini maana yake ni kwamba sisi tungetenga fedha zile ambazo mmetupa kujenga barabara ileā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaj)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)