Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya ajira ni changamoto inayokumba nchi nyingi za Afrika na dunia kwa ujumla, tofauti pekee iliyopo kwa nchi ambazo tunakumbwa na changamoto ya ajira kwa vijana ni namna ama approaches tunazotumia kwenye kukabiliana na changamoto ya ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali kwa program mbalimbali zinazofanyika kwa vijana kwa ajili ya kutatua changamoto ya ajira ikiwemo program ya kukuza ujuzi kwa vijana ambayo mpaka sasa imewanufaisha vijana zaidi ya 5,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi ningependa nishauri masuala kadhaa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, program ya kukuza ujuzi ilitakiwa iongezwe na kuwa program ya kukuza ujuzi pamoja na mitaji. Nasema hivi kwa sababu ninaogopa kwamba tunapoelekea program hii ya ujuzi inaenda kuleta daraja lingine la wahitimu tofauti na wahitimu tulionao wa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, program hii kama nilivyosema imezalisha wahitimu zaidi ya elfu tano ambao hawana mitaji wapo mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti ya mhitimu wa program ya ujuzi na mhitimu wa Chuo Kikuu ni kwamba wa Chuo Kikuu anakuwa na ujuzi wa darasani huyu anakuwa na ujuzi wa stadi za kazi lakini wana-share kitu kimoja wote hawana ajira na hawana mitaji. Halmashauri zetu Tanzania nzima karibia 185 zinatoa takribani Shilingi Bilioni 28 kila mwaka kwa ajili ya mikopo ya vijana, program hii ya ujuzi imetengewa Bilioni Tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani haina tija program kutengewa Bilioni Tisa halafu iende kwenye mafunzo, mikutano, tathmini na masuala mengine ambayo hayaweki masuala ya mitaji kwa vijana halafu tumeweka Bilioni Moja ya mitaji kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, naona hapa hesabu hazijakaa sawa yaani Bilioni Tisa iishie kwenye mafunzo halafu Bilioni moja iende kwenye mitaji nadhani ilitakiwa iwe vice versa. Bilioni Moja ya mafunzo, Bilioni Tisa iwe ni mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ni muhimu lakini haiwezekani tukaweka Bilioni Tisa kwenye mafunzo halafu bilioni moja kwenye mitaji sisi kama vijana haturidhiki tuambiwe kwamba kuna vijana 5,000 wamepewa mafunzo na wako mtaani haiwezekani tunaomba Wizara itusaidie ili fedha hizi zinazotolewa ziweze kuwa na tija kwa vijana end result lazima iwe ajira ama mitaji kwa vijana lakini siyo kuongeza idadi ya wahitimu ambao wanaenda kukaa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatusaidia sana kuwekeza kwenye masuala ya ICT na kwa kweli nipongeze Serikali digital infrastructure imewekezwa kwa kiasi kikubwa, mfano ni National na Regional ICT broadband backbone ambayo imeweza kuwa connected kwenye three International undersea cables.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya uwekezaji kwenye ICT kwa maana ya kukuza matumizi ya teknolojia na tunategemea kwamba Wizara nyingine itaenda sambamba na utekelezaji wa mambo kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inayohusiana na masuala ya vijana ninadhani inabidi wawasaidie vijana kuwekeza katika program za ubunifu ili waweze kutumia hizi infrastructures ambazo zinatengenezwa na Serikali lakini leo hii startup programs tunawajima mikopo ya vijana. Sasa ninapenda niwaulize hivi tumeambiwa model ya kutoa mikopo ni ile tu ya kusaidia vijana ambao wanataka kufanya physical investment kama viwanda? tunapoelekea kweli tunahitaji kukumbushana kwamba sayansi na teknolojia ndiyo habari ya mjini? Kwa hiyo, Serikali inawekeza hii miundombinu ili tufanye nini sasa kama vijana hawawezi kupewa mikopo ili wawekeze kwenye startup programs?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini Serikali inaweka miundombinu ili vijana waweze kufanya program za ubunifu ambazo zitasaidia kutoa huduma lakini zitasaidia kuajiri wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, startup program ikiwa properly invested inaajiri zaidi ya vijana hata 100. Sasa kwanini hatuoni hili? Wataalam watusaidie! Haiwezekani tukawa tuna model moja ya kutoa mikopo ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wote ni sawa, wale wenye bunifu na ambao wanataka kufanya physical investments wote ni wa aina moja na wote ni vijana wa Tanzania. Wizara ipanue mawazo ku- accommodate vijana ambao they want kufanya startup programs.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunawaambia benki wawakopeshe, watawakopesha vipi kama sisi wenyewe tu tunashindwa kuwakopesha. Kwa hiyo tunaomba Serikali itusaidie vijana hawa wapo wengi mno, startup programs zipo tunahitaji uwekezaji hapa ili infrastructure zinapotengenezwa na Serikali ziweze kusaidia vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ndiyo tunaongoza East Africa kwa idadi kubwa ya watu (population), hapa tunavyoongea tupo kwenye kuweka sera kwa ajili ya uhamaji wa nguvukazi ndani ya East Africa. Tusipokuwa makini changamoto ya ajira itaendelea kukua hapa nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nitoe mfano, startup program 24 katika Afrika Mashariki ziliomba capital ya pamoja na wakaweza kupatiwa zaidi ya USD Milioni Moja. Nataka niwaambie Tanzania startup program zilikuwa ngapi? Ilikuwa ni Moja, 17 Kenya, Sita Uganga. Sasa tunapoendelea huku kwenye masuala ya uhamaji wa nguvu kazi lazima tuhakikishe tunaweka mambo yetu vizuri ili tuweze ku-compete katika Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho kuhusiana na mikopo ya Halmashauri. Mikopo hii haina mjadala, inasaidia vijana wengi sana, lakini sasa hivi tumeenda kwenye aina ya kuweka mikopo kwa maana ya viwanda. Utaratibu uliokuwepo huko mwanzoni, ule muda wa vijana kuweza kufanya marejesho ya mikopo ilikuwa ni miezi mitatu, lakini ilikuwa ni kwa sababu tulikuwa tunatoa startup capitals za Milioni mbili mpaka Milioni tano, lakini model ya sasa hivi ni viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wakaanza kufanya marejesho ndani ya miezi mitatu kwa sababu wote tunafahamu mpaka uweze kupata vibali SIDO, uweze kupata vibali TBS sijui BRELA, ufungiwe umeme kule kwetu kijijini Mbinga ni zaidi ya miezi mitatu. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ipitie kanuni upya ili vijana hawa wanaopewa mikopo kwa maana ya kuanzisha viwanda, mikopo, majeresho yaweze kuongezeka muda, at least wapewe muda wa matazamio miezi Sita. Ndani ya miezi mitatu kwa kiwanda huwezi kufanya marejesho kuangalia na hali yetu ya Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na hili suala sitaogopa kulirudia na naliongea mara nyingi sana. Wizara ya Vijana lazima msaidie Wizara nyingine iweze kuona mambo yenye tija kwa vijana, hususani pesa za kimtandao kwa malipo nje ya nchi. Nalirudia tena tunataka PayPal iweze kufanya kazi hapa Tanzania. Kama Wizara ya Fedha hawalioni, Waziri utusaidie kuwaonesha kwamba vijana wanaojiajiri hapa Tanzania wanahitaji kulipwa na wenyewe kupitia njia hizo, siyo tu sisi tulipe alafu tusilipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapoendelea kupambana na changamoto za ajira sisi kama vijana tunaumia roho kwamba sisi tunakuwa tu ni soko la watu wengine kuchukua bidhaa zetu lakini sisi hatuwezi kuuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara mtusaidie muwaambie Wizara nyingine kwamba vijana wa Kitanzania kwa sababu ninyi ndiyo mna uchungu na ajira za vijana, muwaambie Wizara nyingine haya masuala yanayohusiana na vijana ni lazima yachukuliwe kwa tahadhari kubwa sana na kwa u-serious mkubwa sana kwa sababu changamoto ya ajira ni kubwa sana nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunategemea katika Bunge hili la Bajeti suala la PayPal tunaomba litafutiwe ufumbuzi. Tumeshalizungumza hatuwezi kuzungumza kitu hapa zaidi ya miaka tisa hadi kumi na Serikali mpo. Tunaomba mtusaidie PayPal ifunguliwe, vijana wafanye malipo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)