Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na pumzi ya kuweza kunifanya leo kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi nzuri anayowafanyia wananchi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza naomba nijielekeze kwenye fedha hizi za UVICO-19 ambako Zanzibar nayo ilipata mgao wake na kwa Jimbo langu nami nimnufaika mkubwa katika fedha hizi ambapo zaidi ya madarasa 40 nimepata yenye thamani Shilingi Bilioni Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zimefanya kazi vizuri kwa sababu katika Ward yangu ya Muhambe kuna shule ambayo kwa Zanzibar ni ya kipekee ambayo ilikuwa inaenda mikondo mitatu, sasa fedha hizi zimesaidia kuondoa mikondo ile mitatu kwa kupata madarasa 29 ya ghorofa ambapo itasaidia sana wananchi wa Jimbo langu watoto wetu kusoma vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mwendelezo wa majengo ambayo tulishayaanzisha wenyewe kwa nguvu zetu wenyewe, fedha hizi zimeingia na majengo sasa hivi Wakandarasi wako kazini kazi inaendelea vizuri, kwa hili lazima tuipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupeleka mgao kule Zanzibar na Zanzibar nao ikafanya mgao ule na wengine tukanufaika katika fedha zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili uende kwenye TASAF. TASAF vilevile kwenye jimbo langu ni mnufaika mkubwa, nimepata kituo cha afya chenye thamani ya Shilingi ya Milioni 400 kazi inaendelea, kituo hiki kitanufaisha Majimbo mengine mawili ya Chambani na Mtambile kwani ni kituo kikubwa ambacho kitaweza kusaidia kupunguza gharama za wananchi kutoka katika vituo vyetu vidogo kutumia masafa na gharama kwenda katika hospitali kubwa ya Mkoa ya Abdallah Mzee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki ninachoomba ni Serikali iongeze tena fedha kwa ajili ya kupata x-ray pamoja na theater ambapo nimshukuru Waziri Mkuu mwenyewe mbali na kuahidi katika hotuba yake lakini kituo hiki yeye ndie ambaye aliweka jiwe la msingi na akaona kazi inavyoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakamati wa kituo hiki kama tunavyojua kwamba fedha hizi kuna asilimia 20 ni nguvu za wananchi, wananchi kupitia kamati ambayo wameiteua wanafanya kazi kubwa, waliacha kuvuna karafuu, waliacha kulima msimu wa kilimo wakasimamia kituo hichi na kituo sasa kiko katika hatua ya rangi. Kwa hiyo, lazima tuipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu bado naendelea kuomba Serikali kutuingizia tena fedha ili tukamilishe X-Ray, theater pamoja na uzio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala zima la vijana katika uhifadhi wa mazingira. Katika Jimbo langu kuna vikundi zaidi ya 35 ambavyo vimeshajisajili na vinafanya kazi kubwa ya kutunza mazingira katika maeneo yao. Ninaomba kwamba vijana hawa au vikundi hivi viwezeshwe kwanza kwa kupatiwa mafunzo lakini na fedha kwa ajili ya kufanya kazi zao za upandaji wa mikoko na utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno yangu hayo na maombi yangu hayo na kwa ajili ya kutunza muda, naunga mkono hoja hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)