Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwa kuipongeza sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo imejikita kwenye kuona namna ya kutatua na kusuluhisha matatizo yanayowakabili watanzania, ninaamini tukietekeza hii kama ilivyo tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais pia kwa namna ambavyo tumepata miradi mingi kwenye maeneo mbalimbali kwenye Majimbo yetu. Jimbo la Ndanda sasa limechangamka zaidi ukilinganisha na miaka mitano iliyopita wakati ule hatuna Ilani ambayo tulikuwa tunaisimamia na sasa tupo tunakwenda mstari imara wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, wananchi wamechangamka na bado wanaahidi watakichagua tena Chama cha Mapinduzi ili kuweza kujipatia maendeleo wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ninapenda kulisema pamoja na pongezi hizo ni kwamba nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wetu wa Kilimo kwa namna ambavyo juzi tu hapa tulikuwa na kikao kwa ajili ya wadau wa korosho kuangalia na kufanya tathmini ya msimu uliopita. Kuna baadhi ya mambo tumeyajadili, kwanza kabisa nimpongeze kwa kuhakikisha export levy kile kiasi cha pesa ambacho kilitengwa kwa ajili ya kusaidia wananchi hasa zaidi kwenye masuala ya pembejeo kimerudi tena na Serikali imeridhia kwamba pesa hiyo itatoa ili kupunguza nakisi ya bei ya pembejeo ili kuwasababishia wakulima waweze kuzalisha kwa gharama nafuu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimuombe sasa Waziri wa Fedha ahakikishe jambo hili analileta kwenye Finance Bill, lisiwe tu kwamba ni matakwa ya Waziri walikutana huko wakaonana lakini liwe kisheria kabisa ili kila mwaka sasa hiyo pesa iwe inarudishwa isiwe maamuzi ya kipindi kimoja kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninaomba pia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo yeye mwenyewe alete sheria itakayokuwa inasimamia masuala ya kilimo. Tumesikia hapa juzi wakati wa uzinduzi, wakati wa ugawaji wa pikipiki zile kwa ajili ya wenzetu Maafisa Ugani ameongea mambo mengi sana mazuri kwa ajili ya kuboresha kilimo, hata hivyo mambo haya hayapo kwenye sheria, afanye namna nzuri aweze kuleta sheria hapa tumsaidie kuipitisha ili iweze kuwa kama dira ya shughuli anazotaka kuzifanya kwenye Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa wa Waziri ya Kilimo, naweza nikakukumbusha mambo machache ambayo tuliyaongea wakati wa kikao chetu cha wadau wa korosho, na nafanya hivyo makusudi ili iingie kwenye Hansard uone na wewe namna ya kuyashughulikia.

Kwanza kabisa tulikushauri kwamba kuna mambo mawili, sasa hivi tunayo Bodi ya Korosho mpya na tunaona inafanya kazi yake vizuri kabisa chini ya Mwenyekiti wetu Mzee wetu Mzee Mwanjile wanafanya kazi nzuri sana, lakini tulikushauri na mimi nilitoa ushauri nikakuambia kwamba tunae Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho ambaye ameshakaa pale ndani zaidi ya miaka mitatu akiwa anakaimu, tukakuomba kama inawezekana fanya mambo mawili ili aweze kufanya kazi zake kwa uhakika, ama umthibitishe kwa sababu amekuwepo Bodi ya Korosho muda mrefu au umuondoe ulete mtu mpya ambaye anaweza akafanya kazi vizuri zaidi ya huyu aliyepo kwa sababu kwa kipindi kirefu hamjamhibitisha, sasa hatuelewi tatizo ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni kwamba kumekuwa na migogoro mingi ndani ya Bodi ya Korosho na wewe kama Waziri nafahamu labda mingine imekufikia, migogoro ya watumishi, migogoro ya wanunuzi kwa mfano kuna Kampuni moja inaitwa TF Commodities wanadai Bond yao ya Milioni 50 zaidi ya miaka mitatu sana. Tunaomba kwa sababu wale watu wanachajiwa interest kwenye mabenki au warudishiwe au wakatwe hicho kiasi ambacho kinachotakiwa kukatwa balance yake apewe ili aweze kuendesha maisha yake na hii itawapa comfort wanunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea pia suala la usambazaji wa viuatilifu, tunakupongeza sana kwa sababu kiasi fulani kimeshafika kwenye maeneo yanayotakiwa yasambazwe. Hata hivyo tunakuomba kwamba kuna migogoro mingi ya upatikanaji wa tender hizi ambazo zinasimamiwa na bodi ndogo ambayo inaitwa Bodi ya Pembejeo lakini na yenyewe haipo kisheria, kazi wanazozifanya haziwapi amani sana watu wengi wanaosambaza pembejeo kwa sababu imekuwa na aina fulani ya upendeleo, badala ya kuangalia performance wameangalia kama mambo ya kujuanana nayo tunaomba uichunge uone namna ya kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba sasa nijikite kwenye mchango wangu rasmi. Nianze kwa kusema kama Wabunge wote tunakubaliana kabisa kimsingi kwamba kuna inflation, kuna ongezeko kubwa sana la bei ya bidhaa mbalimbali. Jana tulimuona Mheshimiwa Waziri wa Fedha akiongea kuhusiana na suala hili la ongezeko la bei, tulimuona pia Waziri wa Viwanda na Biashara nae akiongea kuhusiana na suala la ongezeko la bei. Kwa nafasi zetu kama Wabunge tuna wajibu wa kuishauri Serikali ili iweze kuangalia namna bora tutakavyoweza kupata solution ya kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha uliopo sasa hivi kutokana na ongezeko kubwa la bei ya bidhaa, kuanzia bidhaa za ujenzi mpaka bidhaa za chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anaongea alisema kwamba anataka kuona namna bora ili kuweza kupunguza bei ya kodi ya sukari. Ameangalia tu element moja ya sukari, lakini nazani suluhisho lingekuwa kuangalia zile tozo mbalimbali zilizoko kwenye mafuta ya magari na kuzipunguza, kwa sababu zaidi ya asilimia 50 ya bei ya mafuta sehemu kubwa ni tozo za Serikali. Kwa hiyo wakaziangalie hizi tozo ili waweze namna ya kuzipunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala jingine ambalo tulikuwa tunaliongea kila mara kupitia Waziri wetu wa Viwanda na Bishara lakini Waziri wa Fedha nawe ulifahamu. Kulikuwa na kitu kilikuwa kinaitwa electronic tax stamps (ETS) na chenyewe kilikuwa kinalalamikiwa muda mrefu sana na wafanyabiashara nadhani Kamati yetu ya Viwanda na Bishara kwenye taarifa yake itakuwepo, lakini pia Kamati ya Bajeti na yenyewe taarifa yake itakuwepo. Oneni namna ya kukaa na wafanyabiashara tupate solution ya uhakika kwa sababu ongezeko la shilingi mbili au shilingi tatu kwenye bidhaa yoyote ya kinywaji kwa mfano, soda Coca-Cola itakapoongeza shilingi 30 kwa ajili ya kupitisha hiyo stempu wao hawawezi kuongeza shilingi 30 kwenye kinywaji watakwenda kuongeza kati ya shilingi 50 mpaka shilingi 100, kwa hiyo inaongeza gharama kubwa. (Makofi)

Kwa hiyo, kama tunasema tunataka kuangalia kurekebisha inflation tuangalie vile vitu vidogo vidogo vinavyoongeza gharama kubwa za uzalishaji ili kuweza kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine kwenye suala la Wizara ya Nishati. Wizara ya Nishati ina mpango wake wa REA ambao kwa Mkoa wa Mtwara sasa hivi kidogo imesuasua na hatufahamu sababu ya msingi ni nini, tutaomba atakapokuja hapa Waziri basi atueleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nililotaka kusema kubwa ni kwamba Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Lindi ndiko inapozalishwa gesi. Tunashangaa sana watu tunaotokea maeneo haya, gesi ni uchumi wa Kusini kama ambavyo ilikuwa miaka ya huko nyuma na maeneo mengine, lakini kwa kiasi kikubwa mikutano yote inayohusiana na kutaka kufanya mikataba ya LNG, mikataba ya gesi inakwenda kufanyikia eneo la mbali kabisa na maeneo haya. Sasa watu tunaotokea maeneo haya tunanufaika na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tuanze kuona tunanufaika tokea mapema. Mikutano inayuhusiana na masuala ya gesi ya LNG pamoja na haya mazao kwa mfano korosho na mengine ifanyike eneo la Mtwara na Lindi ili wafanyabiashara wa kwetu wa maeneo haya waweze kunufaika na mikutano hii. Kwa sababu watu watanunua chakula kwa Mama Lishe, watu watakwenda kulala kwenye lodge hizi zilizopo kwenye maeneo haya ili waanze kuona wananufaika mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia, ahsante kwa muda huu. (Makofi)