Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii ya kunipa kuchangia kwenye ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uelekeo huu wa bajeti ambazo tumezijadili kwenye Kamati zetu na sasa tunazijadili kwenye Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 tulitunga Sheria ya Manunuzi ya Umma na baadae tukaifanyia marekebisho mwaka 2013. Sheria hii ya Manunuzi ya Umma ni sheria muhimu sana kwa sababu zaidi ya asilimia 70 ya fedha zote tunazopitisha hapa kwenye bajeti, tunakwenda kuzitumia kupitia Sheria hii ya Manunuzi ya Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii ya Manunuzi ya Umma tunamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali walete Muswada tuifanyie marekebisho kwenye kipengele cha ununuzi wa madawa. Sheria hii tulivyoitunga ni cross-cutting, kununua mabati tunatumia sheria hii, matofali sheria hii, kununua vifaa vingine ni sheria hii pia. Ni lazima sheria hii tuirekebishe ili kipengele cha ununuzi wa madawa kiwe na focus yake, kiwe na umuhimu wake, kiwe na utofauti wake, nitaelezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii kwenye ununuzi wa madawa inatoa mianya mitatu mibaya. Mwanya wa kwanza unaitwa price rigging au price curtailing. Sheria kwa jinsi ilivyo tunapokwenda kuitekeleza kupitia mtandao wa TANePS, hasa ukizingatia kwamba MSD inanunua madawa asilimia 90 tunayaagiza kutoka nje. Kwa hiyo, sheria hii inaitaka MSD kutangaza tender kupitia mfumo wa TANePS na hapa hushindanisha wazabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazabuni hawa kwa mara nyingi kumekuwa na tabia ya watu kujipanga, wakijipanga anayechukuliwa ni yule mwenye bei ya chini, kiuhalisia ukiangalia bei ya chini, ambayo wao wanaiita lowest evaluated bid ukiangalia hii inayoitwa bei ya chini siyo bei ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano MSD walipotangaza kununua mashine inayoitwa Hematology Analyzer mzabuni aliye-tender bei ya chini ali-tender kwa Shilingi Milioni 117 wakati bei ya soko halisi ni Shilingi Milioni 20. Nitatoa mfano wa pili, MSD walipotangaza tender ya mashine inayoitwa immunology analyzer, mzabuni aliye-tender kwa bei ya chini ali-tender kwa Shilingi Milioni 149 ilhali mashine hii bei ya soko inauzwa Shilingi Milioni 37. Nitatoa mfano wa tatu, MSD ilipotangaza kununua mashine ya kuchakata maji kwa ajili ya kutumika katika kusafisha damu, mzabuni aliye-tender bei ya chini ali-tender kwa Shilingi Milioni 129 ilhali bei halisi ya mashine hiyo ni Shilingi Milioni 32. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Mpembenwe.
T A A R I F A
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kidonge cha kilo moja cha kuweza kutengeneza dawa ya kutoa madoa yaani ile JIKI soko halisia inauzwa kwa Shilingi Milioni Nne lakini MSD wamenunua kwa Shilingi Milioni 262 na ushahidi upo. (Makofi)
MWENYEKITI: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Kwagilwa?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naipokea na ninataka nisisitize kidonge kimoja cha kilo moja cha kutengeneza JIKI bei sokoni ni Shilingi Milioni Nne na MSD kidonge hiki wamepelekewa bei ya Milioni 262! (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halikubaliki duniani wala mbinguni. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa subiri kidogo Mheshimiwa Kwagilwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya.
T A A R I F A
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji. Ni kweli Sheria ya Manunuzi ya Umma inaweza ikawa na changamoto lakini bado haizuii MSD kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 Rais Magufuli alituelekeza tuachane kununua dawa kutoka kwa madalali, tununue kutoka kwa wazalishaji, mwaka 2017 angalieni vyombo vya habari. Tulifanya press tuliweza kushusha bei za dawa kwa zaidi ya asilimia 40, kidonge cha Amoxicilline kilichokuwa kinauzwa Shilingi 11,000 tulikinunua kwa Shilingi 4,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashuka kutoka Shilingi 22,000 tuliyashusha mpaka Shilingi 11,000. Tatizo lililopo MSD siyo tu Sheria ya Manunuzi ya Umma, mipango mibaya ya utekelezaji wa manunuzi ya umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, MSD hiyo hiyo kwa Sheria hii ilianza kufanya vizuri. Kwa hiyo, hiyo ni taarifa nataka kusema sheria ipo lakini tunaweza tukabadilisha sheria, lakini kama hatuna mipango mizuri ya procurement ya dawa, vifaa na vifaa tiba tatizo la MSD litaweza kuendelea. Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo Wizara tunayafanyia kazi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri kwa taarifa. Mheshimiwa Kwagilwa unapokea taarifa?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa kwa maana moja nzuri sana kwamba Mheshimiwa Waziri…
MWENYEKITI: Haya na ninakuongezea dakika moja na nusu kwa kumalizia hoja yako.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anakubaliana kwamba lipo tatizo, kama tunataka kumsaidia Mheshimiwa Rais, ambaye amekwishatoa maelekezo ya kwenda kumulika MSD tumsaidieni sisi kwa sababu sehemu yetu ni kutunga sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inayo shida, shida hii inatupeleka hata Bima yetu ya Afya haifanyi kazi. Huwezi kuwa na Bima ya Afya inayohudumia vifaa ambavyo viko overpriced. Madawa yapo overpriced, vifaa vinavyotumika viko overpriced, Bima yako ya Afya itashindwa ku-cover haiwezi! Siyo tu hivyo, namuongelea mwananchi wa Kata ya Kwamagome anayeumwa figo akafanye diagnosis kwa Shilingi 300,000 haiwezekani! Shilingi 500,000 haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuongelea mwananchi wa Kata ya Malezi, namuongelea mwananchi wa Kwaluala, mwananchi wa kwa Sindi haiwezekani! (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!
MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri Daktari Godwin Mollel una taarifa?
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti…
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilindie muda wangu umechukuliwa. (Makofi)
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Afya ameshalielezea vizuri, jambo lenyewe liko straight forward na akasema Rais wetu wa Awamu ya Tano alishaeleza kwamba tuendeni viwandani. Kwa hiyo, anachochangia ni kizuri sana hatuna shida, lakini tukishatoka tukaelekea upande wa viwanda tumekata huo mzizi wa fitina, na vyombo vyetu vingine vikifanya kazi vizuri kuhakikisha wanasimamia hakuna namna yoyote hayo yanayosemwa wakati hii Nchi ina vyombo vyake ninakuhakikishia hakitatokea hicho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Afya ameshatoa maelekezo na kazi hii inaendelea.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mollel kwa taarifa yako. Mheshimiwa Kwagilwa, unapokea taarifa?
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada zote hizi za Serikali inaonesha kwamba lipo tatizo. Ninachotaka niseme ni nini?
Mimi nitamshangaa sana Mtanzania yeyote ambaye haelewi hiki ninachokisema hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kwamba Mheshimiwa Rais amepeleka Shilingi Bilioni 200 MSD na bado Watanzania hawana madawa kwenye hospitali! Mheshimiwa Rais amepeleka shilingi bilioni 200 na bado hazitoshi kununua dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria mazingira ambayo mwongozo uliotolewa na Serikali… (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kwagilwa kwa mchango wako sasa namuita Mheshimiwa…
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)