Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja iliyopo mezani ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nami kama walivyosema wenzangu kwa kanuni ile ya kibinadamu, usipomshukuru mtu basi hata Mwenyezi Mungu huwezi kumshukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na Viongozi wote wa Serikali kwa miradi mbalimbali ambayo wananchi wa Jimbo la Kilombero, Mkoa wa Morogoro wameendelea kuipata. Tunamshukuru Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Martin Shigela na viongozi wake wote na Wakuu wa Wilaya kwa usimamizi mzuri unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu unatakiwa kuviomba katika mjadala huu wa kupanda bei ambao unaendelea katika Bunge lako ni kuiomba Serikali na kumuomba Mwenyezi Mungu kwamba, miradi ya Serikali na mipango na mikakati yote ambayo imesomwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu isije ikakwama, kwa sababu Serikali ilishajipanga kutuletea maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tulipambana katika corona baadhi ya miradi haikukwama, tumuombe sana Mwenyezi Mungu miradi yetu isikwame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi kama Wabunge tunatoa mawazo yetu hapa, lakini kama walivyosema baadhi ya Wabunge tusisahau kumtanguliza pia Mwenyezi Mungu mbele, tumuombe Mwenyezi Mungu atusaidie janga hili tuvuke salama. Semeni Amina. (Makofi)
WABUNGE: Amina. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwenyezi Mungu awajalie viongozi wetu busara na hekima tushikamane wakati huu Watanzania, semeni amina!
WABUNGE: Amina. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa 29. Ni imani yangu kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu atanisikiliza, ukurasa wa 29 ametoa taarifa ambazo napenda Waziri wa Kilimo azisikilize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tatizo hili la kupanda bei lakini kama wananchi wetu wanaendelea kuzalisha halafu katika kuzalisha huko wanakutana na vikwazo, tunazidi kuongeza uchungu mara mbili. Mheshimkiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa 29 anasema, katika vyama vya ushirika 6,013 vilivyokaguliwa vyama vyote hati mbaya, hati chafu, kasoro vyama 300 tu vya ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka kusema hapa vizuri kabisa, kama Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake ameona katika vyama 6,013 vya ushirika vilivyokaguliwa na CAG, vyama 2,674 Hati yenye Shaka, vyama 1,253 Hati Isiyoridhisha, vyama 1,729 Hati Mbaya kasoro vyama 300 tu. Mpaka tunavyozungumza hivi huko kuna wakulima wanauza mazao yao kupitia ushirika, Warajisi wa Ushirika wapo maofisini wanaendelea kula bata, biashara kama kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo nina imani naye ananisikiliza kwamba, tunaomba mabadiliko. Kwa mfano, Mkoa wa Morogoro tumeshalalamika sana kuhusu Mrajisi wa Mkoa. Tumeshalalamika sana kumhusu Mrajisi wa Kanda na nimesikiliza baadhi ya Mikoa hapa wamelalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni moja. Mimi nilikuwa DAS Rombo na wewe ulikuwa DAS Arusha unakumbuka, tumeondoka Kilimanjaro tuna malalamiko ya Mrajisi wa Mkoa. Tumefika hapa aliyekuwa Waziri wa Kilimo wakati ule akatumia siku tatu kufanya mabadiliko ya Warajisi wa Mkoa. Kwa nini Kilombero hawafanyi mabadiliko na Mkoa wa Morogoro haufanyiki mabadiliko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaeleza sababu na Mheshimiwa Waziri nimemtumia mpaka video na sauti kwamba, kuna watu kule wanasema mua na sukari ni dhahabu nyeupe, wanafanya wanavyotaka. Sasa mwananchi akizingatia huku kuna bei zinapanda, huku ana mua wake kiwandani, hapewi nafasi ya kwenda kuuza hasira inapanda mara mbili. Tunaomba Waziri wa Kilimo mmezindua kilimo vizuri sana vijana wameanza kupenda kilimo, lakini ushirika utawavuta nyuma na ushirika unaweza ukawa kama dude ambalo limewashinda Mawaziri wengine huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fanyeni mabadiliko Kilombero na katika Mkoa wote wa Morogoro. Kwa nini Mrajisi huyu haondolewi malalamiko yote tumeyasema? Kwa nini huyu Mrajisi wa Kanda sijui anaitwa Ndugu Mshumba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitakuomba nita-play sauti ya mwananchi mmoja kati ya wananchi 20 walionipigia simu kumlalamikia huyu mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapandikiza Wakandarasi, wanafanya mambo yao, wanavuruga kilimo na kilimo cha mua ni muhimu katika nchi yetu. Kilimo cha mua ni muhimu kwa wananchi wa Kilombero. Kilimo cha mua kinatusaidia kujitegemea katika sukari, lakini Warajisi wanafanya madudu wanavyotaka wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaenda kwenye Mkutano Mkuu wanavunja Bodi wao wanalazimisha kuleta watu wa bodi wanaowataka wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sishangai Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kusema vyama vyote vya ushirika vilivyokaguliwa ni hovyo, wala sishangai kwa sababu ya Warajisi hawa ambao tunawalea. Nimemuona Mbunge wa Katavi hapa Kaka yangu Kakoso analalamikia mambo ya ushirika, kwa hiyo naomba ichukuliwe hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako naomba ni-play sauti mojawapo ya mwananchi ukiniruhusu, tusikilize hapa mwananchi analalamika kuhusu mambo ya ushirika ili Mheshimiwa Waziri aweze kuchukua hatua.
MWENYEKITI: Hapana Mheshimiwa, haujaruhusiwa kufanya hilo jambo.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Asenga unatakiwa uombe na Kiti kikikuruhusu ndiyo uendelee. Endelea kuchangia.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-play sauti ya mwananchi akitoa malalamiko yake kuhusu…
MWENYEKITI: Table Mezani halafu itapokelewa.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Naomba kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza suala la ushirika nataka kuzungumzia kidogo kwenye suala la ujenzi. Ni imani yetu hapa kwamba, Mawaziri watakapokuja watatusaidia kujibu baadhi ya changamoto. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amejaribu kuzungumza baadhi ya miundombinu inayojengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kilombero tuna changamoto moja kubwa ya barabara ya Ifakara – Kidatu. Sasa hivi tumekuwa wataratibu na wapole kwa sababu, tunaona dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Katibu Mkuu wa Wizara Injinia Aisha Amour na Meneja Mkuu wa TANROADS Injinia Mativila. Tuna imani kwamba, Waziri atakapokuja hapa atatuambia ule mkwanziko wa settlement na Mkandarasi kikao kitafanyika lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ukija hapa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi atatusaidia kujua ahadi ya Mheshimiwa Rais katika eneo la Mang’ula Kona aliyotupatia itaisha lini? Fidia za wananchi waliotoa kuhusu ile barabara zitaisha lini? Na kwa nini Kilombero ilirukwa katika taa za barabarani? Nafikiri tutapata majibu hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema katika ujenzi nataka kuzungumza katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kidogo, nina imani Mawaziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa watakuja hapa. Sisi kama wananchi wa Kilombero katika Bunge hili la Bajeti tunatarajia tulitoa wazo kwamba, kama ilivyofanyika katika Wizara ya Maji, Mheshimiwa Rais amenunua miundovifaa vya kupima maji na kuchimba maji, tulitoa wazo TARURA ni vizuri Serikali ikanunua vifaa kama ma-grader, excavator, kwa baadhi ya Wilaya ikazipatia vifaa hivi ili kupunguza gharama kubwa za ujenzi wa barabara ambazo sasa hivi hali yake ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamesema hapa upande wa Wizara ya Afya nami nataka kuchangia kidogo. Wakati nimesimama hapa nazungumza nilimpa Naibu Waziri wa afya juzi ki-memo changu kumwambia hospitali yetu, kituo chetu cha Kibaoni-Ifakaraka ambacho tunakitumia sasahivi kama hospitali ya Wilaya hakina dawa kiasi kwamba, wamama wajawazito wanarudishwa nyumbani bila dawa. Sasa Wabunge wengi wamesema hapa kuhusu mambo ya MSD na mimi naomba Serikali na Mheshimiwa Waziri Ummy wachukue hatua za haraka iwezekanavyo kuhakikisha wanakabiliana na suala la dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji. Tuna imani Waziri wa Maji atakapokuja hapa tunataka kusikia habari ya Miji 28. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia ametaja miradi ya Miji 28 na Ifakara, Kiburubutu, ipo ndani ya miradi ya Miji 28. Imani yetu ni kwamba Waziri wa Maji atakapokuja hapa atatupa picha na muda gani mradi wetu ule unaenda kutolewa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sitaki useme. Naunga mkono hoja. (Makofi)