Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Katika hili nianze tu kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa huduma ambazo amezitoa hasa katika Wilaya yetu ya Kakonko. Mama Wilaya ya Kakonko tumemuona katika madarasa, Mama Wilaya ya Kakonko tumemuona katika hospitali, na kadhalika, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu Kigoma barabara ndiyo siasa, lakini bahati mbaya Mkoa wa Kigoma kwa nchi hii ndiyo Mkoa haujaungwa katika Mikoa mingine, kwa maana ya kuunganishwa na mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaunganishwa Mkoa wa Kigoma kutoka Katavi, hatujaunganishwa Mkoa wa Kigoma kutoka Tabora, hatujaunganishwa mkoa wa Kigoma kutoka Kagera. Ni aibu kwa Serikali naweza nikasema. Katika hotuba ya mwaka jana Serikali ilisema kwamba, kuna hatua zinafanywa na wataalam wako kule, lakini kazi inayofanyika si njema. Ninaiomba Serikali ichukue hatua ya kusukuma mafundi ili waweze kukamilisha barabara katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimezungumza, ipo barabara ambayo inatuunganisha Wilaya yetu ya Kakonko na nchi ya Burundi ambayo inaanzia Kakonko kwenda Kijiji cha Kinonko kwenda Nyakiyobe kwenda Gwarama kwenda Kabale mpaka Muhangi. Mpaka ule Serikali imejenga soko kubwa sana, lakini soko lile halina huduma, halitoi huduma vizuri kwa sababu hatuna barabara ya kuweza kutuunganisha pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilichangia na nimeomba sana muda mwingi, hebu Serikali chukueni hatua ya kuijenga barabara hii ambayo itaongeza uchumi kwa nchi hii. Pale maji yapo, pale umeme upo, lakini shida ni hiyo barabara. Naiomba sana Serikali itujengee barabara hiyo ambayo ni barabara ya kimkakati, itatusaidia kama nchi kuweza kupata fedha katika mpaka ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo ahadi za Serikali. Mheshimiwa Lusinde amezungumza hapa, kila Mbunge akisimama atasema darasa langu halijakamilishwa, daraja langu halijakamilishwa, alisema Waziri Mkuu, alisema Mheshimiwa Rais. Kwa nini usifanywe utaratibu miradi yote, ahadi zote za Viongozi zikaweza kuorodheshwa na tukaambiwa Wabunge wote kuona kwamba, mimi ahadi yangu ambayo alitoa Rais, mimi ahadi yangu alitoa Waziri Mkuu, mimi ahadi yangu aliyotoa Makamu wa Rais imewekwa kwenye orodha, ili wote tujue kwamba, ahadi ambazo zimetolewa na viongozi zimeorodheshwa na hivi kila Mbunge ataweza kuridhika kwa sababu, atakuwa na uhakika kwamba, ahadi iliyotolewa na kiongozi kwenye eneo lake ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ikishafanywa hiyo tuanze na ahadi ambayo ilitolewa na marehemu Magufuli katika Mji wa Kakonko. Katika Mji ule tuliahidiwa kilometa tatu ambazo ziko ndani ya Mji wa Kakonko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie kwamba, mpaka muda huu ndani ya miaka Sita tumeweza kujengewa kilometa 0.63. Kwa hiyo, niombe Serikali inapochukua hatua ya kuiorodhesha miradi yote, basi namba moja uwe mradi huo wa ujenzi wa barabara ya lami katika Mji wa Kakonko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara za Mji wa Dodoma. Mji wa Dodoma unakua, hatutegemei kwamba Mji wa Dodoma sasa utakuja urudi kuwa Manispaa au uje kuwa Mji wa kawaida ni Jiji sasa, lakini Serikali hatuoni mbanano wa magari kwenye Mji huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kutoka Kisasa kuja hapa mpaka Bungeni ni shida kweli. Polisi wakishafunga barabara, labda Waziri Mkuu anakuja au Makamu wa Rais anakuja kwenye shughuli mbalimbali, inakuwa ni mtafutano kwelikweli. Ninaiomba Serikali ichukue hatua ya kujenga barabara ambayo itaruhusu malori badala ya kuingia Mjini katikati Dodoma, basi malori yaweze kupita kule pembeni, nina hakika itasaidia Mji katikati kubaki wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo huduma ambayo inatolewa kwa upande wa miamala ya fedha. kutoa fedha kutoka kwenye account kwenda kwenye mitandao tofauti-tofauti mfano, tiGO Pesa, M-Pesa, na kadhalika ili uweze kupata huduma hiyo lazima uwe na shilingi 1,000. Inaweza ikatokea kwamba, wakati uko kwenye utaratibu wa kutoa huduma hiyo network ikakata, Shilingi 1,000 imeshachukuliwa, utakaporudia usifanikiwe 1,000 imeshachukuliwa, ukirudia na kadhalika utastukia kwamba, Shilingi 5,000 zimekwenda lakini huduma ile haijatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ifuatilie hilo, kuona uwezekano wa kwamba kama huduma haikuweza kupatikana basi hizo fedha zisiweze kutoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mitandao ya simu Wilaya yangu ina shida sana ya mtandao wa simu, shida ipo kubwa sana katika Kata ya Nyamtukuza, Kata ya Nyabibuye, Kata ya Gwarama, Kata ya Rugenge, Kata ya Mugunzu, Kata ya Katanga, Kata ya Kanyonza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi nikiwa nyumbani siku ukinitafuta usinipate ujue kwamba niko nyumbani mawasiliano hadi nyumbani kwangu hayapo, ninaiomba Serikali ichukue hatua hasa kwenye Mikoa ya pembezoni na Wilaya za pembezoni ziweze kupata huduma ya mitandao ya simu ili tuwe na uhakika kwamba kila Mtanzania anaweza akafurahia mawasiliano ya simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upande wa umeme, bado kuna shida ya umeme katika Mkoa wa Kigoma. Muda huu tunaambiwa kwamba kuna ujenzi wa lane ya umeme kutoka Nyakanazi kwenda Kigoma, hao mafundi hatuwaoni ninaomba Serikali ichukue hatua ya haraka kuona kwamba Kigoma nasi tunapata umeme kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)