Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote naomba niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa wenyeviti wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja mbili tu, kwanza nilitaka nilikumbushe Bunge siyo kila mtu anayechangia humu ndani kwa maslahi ya Taifa inaonekana kuna jambo limepita au kuna mtu amenunuliwa au kuna rushwa imefanyika ni lazima kama Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kuwakilisha wananchi, lile ambalo tunaliona haliendi sawa tuna umuhimu wa kuja kulisema hapa na Serikali iweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile upande wa Waheshimiwa Mawaziri pale wanapoona kuna tatizo basi walisimamie hili jambo liweze kuisha kuliko kuwa na uwoga wa kutokulisimamia jambo ambalo tunaona haliendi sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilikuwa Makamu Menyekiti wa Hesabu za Serikali, tulikuwa na mgogoro wa uwekezaji kule Kigamboni katika mradi wa Dege ECO Village. Spika aliagiza na baada ya kuagiza Kamati ikakaa na baada ya Kamati kukaa, ikaunda Kamati ndogo kufuatilia jambo hili, majibu yakaja ndani ya Bunge, Bunge likapitisha Azimio lakini cha kushangaza baada ya Bunge kuvunjwa Mkurugenzi wa NSSF pamoja nafikiri na Waziri labda anaweza kuwa anahusika sina uhakika sana, ikachukuliwa maamuzi ya kumkamata Mwekezaji na kumuweka ndani siku 21 na kumnyang’anya kila kitu ambacho alikuwa amewekeza katika mradi ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi ni mkubwa sana, Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika mradi wa Dege Eco Village ambao uko Kigamboni. Sasa matokeo yake mradi ule umekuwa magofu haujulikani uko wapi, ukienda Serikalini kuuliza wanakwambia mradi huu tumeuchukua umeuchukua kwa njia gani, haijulikani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni kwamba tumemkamata Mwekezaji tukauchukua kwa kumlazimisha, leo Serikali imechukua ule mradi unatafuta Mwekezaji mwingine uweze kuuza, wasiwasi wangu na angalizo langu ni kwamba mwakani au baada ya muda mchache Mwekezaji anaweza kwenda Mahakamani na akashinda kesi ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Serikali ije na majibu mazuri. Kwanza ituambie ni njia ipi iliyotumia kuweza kumnyang’anya mwekezaji share zake. Pili, mradi ule ulikuwa na Wakandarasi wako site, wale Wakandarasi wanalipwa na nani? Mradi umechukuliwa lakini wale Wakandarasi wanadai fedha zao. Je, Serikali italipa au ndiyo wanadhulumiwa moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linasikitisha sana kulikuwa na Wakandarasi zaidi ya 20 pale, yuko Mkandarasi Mkuu wako ma-subcontract wengi sana walikuwa wamefanyakazi pale. Lakini mpaka leo hawajalipwa pesa na mradi umechukuliwa na Serikali sasa nani atakayelipwa ninamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu hii taasisi iko chini yake, aweze kutuletea majibu anapokuja kufanya majumuisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa zaidi ambalo nimeliona ni vizuri Serikali ikafahamu, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameongelea suala la SGR hapa kwamba ni mradi mzuri unakwenda vizuri tumeanza na loti namba moja tumekuja na loti namba mbili na sasa hivi tunaelekea loti namba tatu na tunaelekea kumaliza na loti namba nne mpaka namba tano na namba sita, naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa sana iliyoifanya. Lakini ninaona kuna changamoto na changamoto hiyo nisipoiongelea nitakuwa siyo mzalendo wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kujenga loti namba moja, tumejenga loti namba mbili tukaruka tukaenda kujenga loti namba tano. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, Wajumbe wa Kamati wenzangu wengine wako hapa, tulipoenda kukagua maeneo yote tumeridhika kabisa na maeneo namba moja na namba mbili tumeenda namba tano tumekuta hali si shwari, Mkandarasi wa pale amejenga kwa asilimia Nne tu mpaka sasa na ana muda wa mwaka mmoja na miezi minne lakini hakuna jambo lolote lililofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu inakuja tumetangaza tender nyingine loti namba sita ambayo inatoka Tabora kwenda Kigoma hapa kuna harufu mbaya sana ya rushwa, Waziri anatumia madaraka vibaya ya kutumia neno linaitwa single source kugawa kazi kwenye makampuni ambayo hayana sifa. Mkandarasi aliyeshinda nafasi hiyo ambayo amepewa tender ya kujenga barabara ya kutoka Tabora kwenda Kigoma, Mkandarasi huyu ndiye anayejenga loti Namba Five ambaye amejenga asilimia Nne, na sasa hivi wanampa kujenga loti Namba Sita kwa single source.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii single source nataka niijue inatumia vigezo gani ili kuweza kumpa Mkandarasi aweze kuendelea na mradi mwingine.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa anayezungumza sasa hivi Mheshimiwa Mbunge, kwamba wakati tunakagua mkandarasi huyu wa China katika loti hiyo ambayo anaisema ya Isaka Mwanza, tuligundua mapungufu makubwa sana mojawapo ikiwa ni matatizo ya kiusalama kwa wafanyakazi hata First Aid Kit hakuna, ambulance zinazotakiwa ziwepo hakuna, hata sasa hivi kama unavyosema muda aliopewa hadi sasa ni asilimia Nne tu. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba angekuwa na sifa ya kupewa hiyo single source ni yule aliye perform vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nataka nimpe hiyo taarifa.

MWENYEKITI; Ahsante, na muda wako ndiyo kama hivyo Mheshimiwa Aeshi.

MHE. AESHI. K. HILALY: Hapana!

MWENYEKITI: Basi hitimisha hoja yako kwa dakika moja Mheshimiwa.

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ngoja niendelee, nimeipokea taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa nitapunguza taarifa kwa sababu muda upo mwishoni halafu wachangiaji lazima wamalizie wale wawili, malizia Mheshimiwa Aeshi kwa dakika moja.

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa, lakini la msingi hapo ninataka kusisitiza ni kwamba Mkandarasi huyu ambaye ameshindwa ku-perform amepewa tena tender ya kujenga kutoka Tabora kwenda Kigoma. Hoja ya single source ni pale Mkandarasi anapo-perform vizuri, anapofanyakazi vizuri ndiyo apewe kazi nyingine. Sasa mtu ambaye amejenga kwa asilimia Nne, hatujajua anajenga kwa kiwango gani tunamuongezea kazi nyingine ambayo hii hata asilimia 10 hajafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo ni kwamba kuna vitu havifanyiki sawa, nasi Wabunge hatutakiwi kukaa kimya.

MWENYEKITI: Ahsante. hata hivyo muda wako umekwisha.

MHE. AESHI. K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza kusababisha watu kutaka kutoa rushwa, hatuwezi kukubali. Ninaiomba Serikali ije sasa na majibu mengine au iangalie upya utaratibu uliofanyika hauko sawa. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua mchango anaosema Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Aeshi nilitaka nitoe taarifa kwamba loti Namba Tano tangu ianze ilikuwa haijawahi kupata financing, fedha iliyokuwa inatoka ilikuwa ni fedha ambayo ilikuwa inawekwa akiba toka Serikalini. Hivi ninavyoongea ndiyo tunamalizia evaluation ya financing ya loti yote kuanzia Namba Three, Namba Four na Namba Five. Kwa hiyo, kwa sababu financing yake haikuwepo ni dhahiri kwamba kusinge kuwepo na kasi kubwa sana ya loti Namba Tano kwa sababu hakukuwahi kuwa na financing ambazo ziko attached na loti hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hili ambalo amelisema nadhani ni michakato ndiyo inaanza hamna mtu ameshapewa kazi nadhani ni michakato ambayo inaendelea.

Michakato ikiwa inaendelea hatuwezi tuka-conclude kwamba kuna tatizo kwamba kuna mtu amepewa.

MHE. AESHI K. HILALY: Taarifa ya Mheshimiwa Mwigulu siipokei, kwa sababu haiingii akilini mtu ambaye amejenga kwa asilimia Nne hata kama fedha haijapatikana, halafu mtu huyo huyo mnaanza mazungumzo naye tena ya awali ya kumpa kazi nyingine ambapo kazi ya kwanza hajaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya ukandarasi lazima awe na uwezo, kama uwezo anao angeanza kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hili uliweke sawa, kuna jambo hapa haliko sawa kabisa. Mheshimiwa Waziri anataka kuhalalisha jambo ambalo halipo, bado dakika moja nilikuwa nahesabu hapa.

MWENYEKITI: Hitimisha hoja yako sasa.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninahitimisha. Ninaiomba Serikali iangalie upya utaratibu huu wanaotaka kuufanya, utaratibu huu wa single source unataka kutumika vibaya, unataka kuhalalisha vitu ambavyo hatutoweza kukubali wala kuvifumbia macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)