Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu ili kuchangia hoja ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wote waliopo Serikalini kwa jinsi wanavyofanya kazi na kupita maeneo mbalimbali wakihamasisha shughuli za maendeleo. Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru Serikali ya CCM. Unapopata kidogo ni lazima ushukuru. Ninaishukuru sana Serikali ya CCM kwa kuweza kuendelea kuufungua Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Kabingo – Kibondo mpaka Buhigwe yenye urefu wa kilometa 260 inaendelea kujengwa. Sasa, niiombe tu Serikali iongeze fedha ili barabara hiyo ikamilike mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze mama yetu mpendwa kwa kutupatia fedha ya COVID-19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nchi nzima na kila jimbo; tunamshukuru sana mama yetu. Mwaka huu hakuna mtoto ambaye amemaliza form IV na anatakiwa kwenda shuleni ambaye amebakia nyumbani, wote wameweza kwenda shule. Wapo wengine ambao walisafiri kwenda maeneo mbalimbali kabla ya matokeo kutoka. Niwaomba wazazi wao wawahamasishe watoto hao ili waende shule kusoma kwa sababu nafasi zipo na madarasa yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwaombe viongozi wa elimu waliopo kwenye majimbo na Wilaya zetu, kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kwenda Sekondari waweze kwenda Sekondari. Nisiishie hapo, niendelee kuipongeza Serikali kwani zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya zimejengwa na nyingine zimekarabatiwa; kwakweli tunamshukuru sana Mama yetu mpenzi kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kuhusu nishati ya umeme na eneo la pili ni kuhusu kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mikoa ambayo bado haijaunganishwa kwenye grid ya taifa, mikoa hiyo ipo minne, ambayo ni; Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Katavi pamoja na Rukwa. Niiombe, kwasababu mikoa hiyo ipo pembezoni, Serikali ifanye kila namna kusudi mikoa hiyo nayo iweze kufaidi matunda ya taifa kwa kuunganishwa kwenye grid ya taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Kigoma zipo njia mbili. Njia ya kwanza ni grid ya taifa kutoka Tabora kuja Kigoma kwa KV 132. Ninaomba, mradi huu ambao tayari umeanzishwa ukamilike, kwasababu mpaka sasa hivi mradi ule unasuasua. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba TANESCO waongezewe bajeti ili iweze kukamilisha mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo pia mradi wa kutoka Nyakanazi – Kigoma nao tena unatakiwa kukamilika kwasababu mwanzo Serikali walisema kwamba ungeweza kukamilika 2022. Kwa hiyo tunaomba juhudi ziongezeke ili miradi hiyo ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ukishapatikana Mkoa wa Kigoma utafunguka. Hii ni kwasababu Mkoa wa Kigoma ni lango kuu la uchumi, ni Mkoa ambao umepakana na nchi za DRC, Burudi na hata wakati mwingine Zambia. Kwa hiyo basi umeme ukishapatikana wawekezaji watakuja kujenga viwanda Kigoma, na kwasababu watu wa nchi hizo zinazotuzunguka wanachukua bidhaa kutoka Kigoma; kwa hiyo hawatakwenda mbali, watachukulia bidhaa kutoka katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma tuna Bonde la Lwiche. Kama umeme ukipatikana tunaweza kufanya kilimo cha umwagiliaji; kusaidia juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo; kwasababu tutaweza kusukuma mitambo ya kumwagilia mashamba yetu kwasababu umeme utakuwa wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kuhakikisha mbolea ipatikane kwa bei rahisi, kama mbolea ikipatikana kwa bei rahisi wananchi wetu wataweza kuzalisha kwa wingi zaidi wakiwemo na wanawake. Mimi ni mama, ninawakilisha wanawake. Ni kwamba, wanawake wa taifa hili ni wazalishaji wakubwa, ni wakulima wazuri sana. Kwahiyo, wakipata mbolea wataweza kuzalisha kwa wingi, watapata chakula na kuongeza kipato kutokana na uzalishaji wa mazao watakayokuwa wamelima.

Mheshimiwa Mwenyekiti,niendelee kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha kilimo cha Mchikichi Mkoani Kigoma, tunamshukuru sana, kazi aliyoifanya inaanza kuonekana, michikichi baadhi inaanza kutoa matunda. Kwa hiyo tunaomba Serikali iendelee kutuangalia Mkoa wa Kigoma katika zao letu la Michikichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameweza kuendelea kuelewa maana ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: …Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: …naunga Mkono hoja (Makofi)