Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Na mimi niungane na wenzangu ili kuipongeza Serikali kwa nzuri inayofanyika, na hasa mimi nitajikita katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 13 na 51 ambao unaongelea suala la afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kwamba Serikali imeendelea kuboresha miundombinu kwa kufanya ukarabati, lakini pia kujenga miundombinu mipya ya afya, na hasa tumeona Hospitali za Rufaa za Kanda, za Mikao, Halmashauri Vituo vya Afya na Zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupongeza tena Serikali tumeona fedha zilizotokana na mkopo wa 1.3 trillion, bilioni 466 zote zilielekezwa Wizara ya Afya ili zikanunue dawa na Vifaa Tiba na wananchi wetu waendelee kupata matibabu ambayo ni bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili kwenye fedha hizo zinazopelekwa Wizara ya Afya asilimia 60 na 70 ni fedha ambazo zinanunua dawa, na dawa hizo zinatakiwa zisambazwe katika vituo vyote vya kutolea huduma dhamana hiyo imepewa MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nitajikita katika utendaji kazi wa Shirika letu la MSD; na ninaomba kabla sijaongelea sana MSD niwape chimbuko kidogo la MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia Sera ya Afya ya Juni mwaka 2007, naomba kunukuu, kwamba; “Dawa na vifaatiba ni bidhaa muhimu katika kutoa huduma za afya zilizo bora, bidhaa hizo zinahitajika utaalam na umakini mkubwa wakati wa kuagiza, kutunza na kusambaza”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nasimama mbele yako nikisitika sana, Shirika letu la MSD halina mtaalam hata mmoja wa kusimamia haya ambayo yameainishwa katika Sera ya Afya. Ukiangalia katika watumishi 700 walioko ndani ya MSD ni asilimia 6 tu ya wataalam wa dawa walioko pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia katika kanda zetu 10 zote ambazo MSD inasimamia kusambaza dawa kule hakuna mtaalam wa dawa. Serikali imesomesha wataalam wa dawa kwa gharama kubwa sana, na nikisema katika rank ya gharama ya kusomesha wataalam tunaanza na doctor of medicine tunaenda na doctor of medicine and surgeon tunaingia pharmacist, ni taaluma ambazo zinasomeshwa miaka mitano na internship mwaka mmoja. Pharmacy inasomwa miaka minne na internship mwaka mmoja, ni gharama kubwa kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunao professor pharmacist’s wako 13, leo tunao PhD holders pharmacist wako 20, leo tunao Masters holders 167 ambapo kati ya hao wamesomeshwa procument na supply chain management system; lakini masikitiko yangu ni kwamba ukienda pale MSD leo idara ambayo ni mahususi kwa ajili ya kufanya makadirio ya dawa Tanzania inaongozwa na mtu wa manunuzi tu sifa kubwa ni mwanajeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba Serikali mniambie hivi dawa zimegeuka kuwa bunduki au risasi? Ni kitu gani ambacho kinafanya wataalam waachwe pembeni halafu waende kuchukua mtu wa kawaida? Inasikitisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na leo tunatarajia matokeo makubwa kutoka MSD, haiwezi kutokea; sisi wote kwa imani zetu kila mmoja anaomba afike peponi, pale Mwenyezi Mungu atakapomchukuwa, lakini lazima ufe kwanza. Leo tukitaka MSD ifanikiwe lazima tuhakikishe tunabadilisha tunarudi kwenye Sera ya Afya ambayo ilisema inahitaji mtalaam na umakini mkubwa, wataalam wakabidhiwe ile taasisi iweze kuendeshwa. Tofauti na hapo tutakuja kuona billions of money zinapelekwa MSD zinazama leo nikisimama hapa nikirudi miaka 3 nyuma MSD dawa zilizo-expier ni bilioni 26 kwa sababu gani hakuna mtaalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuambie mimi bahati nzuri ni mfamasia dawa zinatengenezwa katika ma-group nikikuambia group la fetharisporincy kuna dawa kama 100 leo ukiniletea dawa ya cephalexin na cephoxine zote ni fetharisporincy lakini kama sina moja kwenye stoo nitakuambia hii cephalexin itakufaa, lakini wenzetu kwa sababu hakuna wataalam akiambiwa dawa A kama haipo ni out of stock, wanarudi nyumbani kule dawa iliyopo nyingine ina-expire. Leo tunapoteza bilioni 26 ambayo ni sawa na zahanati tunazopeleka milioni 50 522.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vituo vya afya vya milioni 500 ni vituo 52 hapa tunaangalia miaka mitatu miaka mitano hadi 10 ijayo ni nini; Mheshimiwa Rais ameliona hili. Wakati anapokea taarifa ya CAG alisema MSD inatakiwa ifanyiwe overall, ifanye maboresho makubwa, na tumsaidie kumshauri kwamba kilichotokea na kinachosababisha MSD isifanikiwe ni kwa sababu wameacha utalaam wamepeleka watu wa interest ambazo hazijulikani ninaomba Serikali kabidhi taasisi hizi za wataala ili wataalam hawa waweze kufanya kazi ya kitaalam na matokeo makubwa yaweze kuonekana lakini kila siku wananchi wataendelea kuachana dawa hazipo na dawa zina-expire…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kushukuru kwa kulinda muda.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo taasisi ambazo zinafanya vizuri kwa sababu ya kusimamiwa na watalaam wake…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Tabasamu!

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hawezi kusema ni mtu wa kawaida yule mwanajeshi aliyeko pale ni Daktari Bingwa na aombe radhi namuomba Mheshimiwa Mbunge aombe radhi katika jambo hilo hansard iwe sawa (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kyombo unaipokea taarifa!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana kaka yangu Tabasam taaluma ninayoiongelea naongelea pharmacists. Nikienda kwenye mifumo ya ufamasia nikakuambia pharmacokinetics ya dawa nitakuambia…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: …nitakuambia procurement and management supply chain kwakweli naheshimu taaluma nyingine zote. Na nilikua naenda huko kuhitimisha. Kwa hiyo mimi ninaposema vile nasema mtu ambaye ame-specialize kwenye dawa, si kwenye matibabu daktari ana…

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: …ndicho kitu ninachoamaanisha. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba tuishauri vizuri Serikali, tusilete ushabiki, ili twende vizuri Mheshimiwa Rais wetu ili naye aweze kupumzika kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya miradi…

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: … kwamba pale tusiweke watu ambao wanaweza wakakaa na dawa, wakasimamia dawa, wakambaza dawa na zikafika kwa wananchi.

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nikupe mifano mizuri ya taasisi ambazo zinasimamiwa ambazo zinasimamiwa na taaluma za pharmancy ambazo…

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: … zimefanya vizuri tunayo TMDA, mamlaka ya chakula…

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Spika kaniamba...

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya dawa na vifaatiba inafanya vizuri ndani ya nchi na nje ya nchi

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na inatoa gawio hata kwa Serikali.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Masaburi!

T A A R I F A

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge anayeongea kwanza afute ile kauli ya kusema yule si mtaalam, ni mtu wa manunuzi. (Makofi)

MWENYEKITI: Hiyo taarifa au nikufuta kauli?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, afute kanuni ili...

MWENYEKITI: Kanuni namba ngapi?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti ili hansard zikae vizuri…

MWENYEKITI: Unasimama kanuni namba ngapi Mheshimiwa Mbunge?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kyombo, endelea. (Makofi)

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru, tukisikiliza vizuri hoja yangu nimesema mtaalam wa dawa, na nchi hii hakuna mtaalam wa dawa, sijasema medical doctor, nimesema mtaalam wa dawa. Naomba tujikite kwenye hoja ili kusaidia nchi hii ili wananchi wetu wawe wanapata dawa na shughuli zote ziweze kwenda kwa mujibu wa taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,

MBUGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MWENYEKITI: Taarifa wapi ahh Mheshimwa wa Ulinzi

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante!

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu.

T A A R I F A

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa. Taarifa nyingi zimetolewa lakini na mimi nilitaka kuongeza sauti kwamba hatuwezi kusema Mwanajeshi ni mtu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili imeshaelezwa kwamba yeye pamoja na kwamba ni Mwanajeshi ni professional yake pia ni udaktari, tatu Chief Executive Officer wa taasisi yeyote si lazima awe na taaluma ya fani hiyo, anaweza kufanya kazi akiwa na taaluma nyingine yoyote ilimradi ana wataalam wa kufanya naye kazi kwa hiyo naomba ieleweke kwamba si sahihi kabisa… (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa ya Waziri wa Ulinzi, ni taarifa.

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jenerali kwamba ni mtu wa kawaida. Ahsante.

MWENYEKITI: Unapokea taarifa amesimama kwa kupitia kifungu namba 77 taarifa.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijui ambapo sieleweki ni wapi namheshimu sana Waziri wangu mpendwa lakini suala nililosema….

MWENYEKITI: Unapokea taarifa au haupokei?

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.

MWENYEKITI: Ahsante, endelea

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachomaanisha nasema ni mtaalam wa dawa na sijapinga kuwepo kwa brigedia pale, nimesema asilimia sita tu ya wataalam walioko MSD ndio wataalam wa dawa, lakini asilimia iliyobaki yote ni watu wasaidizi ni wanasheria ni wahasibu, nikasema katika kanda 10 hakuna mtaalam wa dawa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio mchango wangu. Kwa hiyo naishauri Serikali iweze kuboresha taasisi yetu ya MSD ifanya vizuri iwatumie wataalam iliyowasomesha kwa bei kubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja ahsante sana.