Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kunipatia nafasi niweze kuchangia Hotuba hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu kwa jinsi ambavyo anaendelea kujali huduma za wananchi wetu. Kipekee niendelee kumpongeza kwa jinsi ambavyo nami nimefaidika sana katika Jimbo la Muhambwe. Tumepata miradi mbalimbali ambayo kwa kweli wananchi wa Muhambwe tunamshukuru sana kwa sababu tutaimarisha huduma za jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imeendelea kuboresha huduma za afya kupitia sera ya mwaka 2007 kwa kuendelea kutoa huduma za afya kwa makundi maalum. Hii ikiwemo watoto chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wasiojiweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hotuba ya Mheshimiwa Waziri mkuu kwenye ukurasa wa 13 na wa 53 imeendelea kujipambanua zaidi kuonyesha jinsi gani itaendelea kujali afya za makundi haya. Tumeendelea kufanya vizuri kwa sababu taifa lolote lenye ustawi wa afya ya jamii yake linapimwa kwa vifo vya mama na mtoto. Na kipekee nchi yetu kupitia takwimu za mwaka 2015/2016 Demographic survey inaonyesha kwamba tunapata vifo vya akina mama 556 katika kila vizazi 100,000 vya Watoto hai. Haya ni mafanikio makubwa sana katika jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na mafanikio yote hayo tuliyokuwa nayo, sera hii ya mwaka 2007 ya kutoa huduma kwa makundi haya maalum bado inatoa mianya ya changamoto kwa makundi haya. Tumejitahidi katika hospitali zetu tumeweka madirisha ya kuyahudumia makundi haya, kama vile dirisha la kuhudumia wazee au dirisha la kuchukulia dawa kwa wazee au mabango yanayosema kwamba mzee atahudumiwa kwanza. Hata hivyo ni ukweli usiopingika kwamba madirisha haya mengi yamekuwa kama picha au anasa maana yanaandaliwa tu pale ambapo tunasikia kuna usimamizi shirikishi (supportive supervision), ili viongozi wetu wakija wayaone, lakini kiuhalisia yale madirisha hayafanyi kazi inavyotakikana ndio maana yale makundi bado yanapata tabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile sera hii ni ya muda mrefu tangu mwaka 2007 na Serikali yetu imejikita kuwa na malengo maalum yaliyozinduliwa mwezi wa sita mwaka jana, na kuonyesha jinsi gani inaendelea kuboresha huduma za afya na kipekee makundi maalum na jinsi ambayo taarifa ya Waziri Mkuu imeonyesha, basi ni muda muafaka sasa kuipitia ile sera ili iweze kuendana na hali ya sasa. Kwa maana kwamba makundi haya yaratibiwe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ushauri wangu katika hili, kwa vile Serikali inatoa pesa nyingi kwa ajili ya kuyahudumia makundi haya basi ni muda muafaka twende kwenye bima ya afya kwa makundi haya. Ile pesa tunayotumia kama ruzuku katika manunuzi ya dawa basi tuwakatie bima za afya ili waweze kupata huduma hizi kwa uhakika. Hii itasaidia kwanza waweze kupata dawa, lakini pili itawaondolea unyanyapaa wanaoupata wanapoenda hospitalini na kuwaambia hawa ni wale wa bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile itawasaidia muda wote waweze kupata dawa, na pia itawapunguzia watumishi Maafisa Ustawi wa Jamii ambao wanafanya kazi ya kuratibu tu hawa wagonjwa kwa kugonga muhuri na kuwaorodhesha, ambapo hawa maafisa ustawi wa jamii wangeweza kufanya kazi zingine zenye maana zaidi kama vile kuratibu malezi ya watoto wetu, zero mpaka miaka nane, kudhibiti ukatili wa kijinsia ili kuboresha afya zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile naungana na wenzangu wote walioongea kuhusu ajira. Bado suala la ajira ni tatizo katika nchi yetu; na kipekee nitajikita kwa wale vijana wa Muhambwe ambao wanapitia changamoto kubwa ya kukosa ajira kwenye ile miradi ambayo tunayo katika Jimbo letu. Tunashukuru Mungu Jimbo letu lina mradi mkubwa wa barabara ya kutoka Kibingo mpaka Kasulu. Lakini ni ukweli usiopingika kwamba vijana wetu hawapati ajira katika miradi ile.
Mheshiimwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu ana sera nzuri sana ya kusema vijana wapate ajira. Lakini ni nani ana ratibu hili zoezi mpaka kufika kule? Je, mkataba wa huyu mwekezaji unaonesha ni vijana wangapi watapata kazi? Ni wangapi wazawa, na ni wangapi watafanya kazi za kubeba vibendera? Inasikitisha sana pale ambapo hata mbeba kibendera ametoka kwingine. Hatumaanishi ubaguzi lakini tunaomba vijana wa Muhambwe wafikiriwe kwanza kwenye hii miradi inayotekelezeka katika Jimbo letu ili nao waweze kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo la mradi mkubwa wa barabara, naiomba Serikali; kwa vile ujenzi wa barabara unaendelea na unatia matumaini kwa kasi nzuri sana, lakini miradi hii inayo miradi shikizi ya jamii, ikiwemo vituo vya afya, shule, kituo cha zimamoto ambavyo kwenye Jimbo langu vinategemea kujengwa pale Nyankwi katika Kata ya Busunzu. Tunaona ujenzi wa barabara unaendela lakini hatuoni miradi hii ikianza kujengwa. Ninafahamu mingine iko Kasulu na mingine iko Buhigwe. Tunaiomba Serikali basi, miradi hii shikizi ya barabara iende sambamba na ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naomba kuunga hoja. (Makofi)