Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuhitimisha hoja yangu jioni ya leo. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hoja hii, wale waliochangia kwa kuzungumza ambao idadi yao ilikuwa ni 24 na wale waliochangia kwa maandishi ambao idadi yao ilikuwa ni 31. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Halima Mdee alinitahadharisha kwamba nisije nikasema muda wa kueleza umekwisha. Ukweli ni kwamba kwa idadi hii si rahisi kumgusa kila mmoja wenu. Nataka niwahakikishie kama kawaida yetu, baada ya kukamilisha kazi hii tutaleta majibu yote kwa maandishi kwa kila mchangiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. Leo asubuhi wakati tumeanza shughuli za bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nilipata moyo sana kuona kwamba Wabunge wote wa pande zote mbili wakiwa wanaliunga mkono jeshi letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali kabisa kwamba, baada ya uchaguzi siasa huwa zinahamia Bungeni. Pia ni sahihi kabisa kila mmoja kupiga siasa humu ndani ya Bunge lakini naendelea kuwasihi Waheshimiwa Wabunge tujitahidi sana kutoliingiza jeshi katika siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwa bahati mbaya sana, nadhani ni kwa sababu ya kuzidiwa tu na hisia zetu za kisiasa zimetoka kauli humu ambazo kwa kweli zisingepaswa kutoka lakini bado tunayo nafasi ya kujirekebisha. Naamini Waheshimiwa Wabunge wa Kambi ya Upinzani na wa Chama Tawala sote tunatambua mchango mkubwa wa jeshi katika nchi yetu na sote tunaliunga mkono na ndiyo maana asubuhi mlimshangilia sana Mkuu wa Majeshi kwa kutambua mchango wa jeshi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba niingie katika hoja za Waheshimiwa Wabunge. Nitaanza na hoja za Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kwanza walisema kwamba Serikali itoe fedha za maendeleo zitakazotengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ukamilifu na kwa wakati na pia Serikali ilipe madeni yote yaliyohakikiwa na Hazina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ambao ni Wabunge tunafahamu kwamba tunapanga bajeti lakini mwisho wa siku inategemea sana na makusanyo ya Serikali. Ni mategemeo ya kila mmoja wetu kwamba Serikali ikikusanya vyema kama ambavyo mwelekeo unaonesha, bila shaka fedha hizi zitapatikana na tutaweza kutekeleza yale ambayo tumeyapanga katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia imetakiwa tushiriki kubuni mbinu za kuzalisha mazao ya kiraia ili kuongeza mapato. Napenda kutoa taarifa kwamba mashirika yetu yote, Suma JKT, Mzinga na Nyumbu, yanafanya juhudi mbalimbali ya kuzalisha mali ili waweze kupata kipato cha ziada. Kwa mfano, shirika la Mzinga wanazalisha risasi za kiraia pamoja na milipuko kwa ajili ya migodi. Nyumbu wanazalisha power tillers na mashine za matofali. Suma JKT wanasindika mazao ya nafaka na uunganishaji wa matrekta. Aidha, mashirika haya yanaendeleza ubunifu mbalimbali ili kuweza kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya wanajeshi zilengwe kwa askari wa vyeo vya chini. Hapa tunasema katika mradi huu unaoendelea sasa ambapo nyumba 6,064 idadi yote imeelekezwa kwa askari wa vyeo vya chini. Hivyo ushauri huu unaenda sambamba na mpango wetu. Ni awamu ya pili ambayo tunalenga kuwapatia nyumba maafisa na wale askari wa vyeo vya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi kumiliki maeneo ya ardhi kisheria. Suala hili tunalitambua ilikuwa ni kasoro kubwa. Siku za nyuma taasisi za Serikali zilikuwa zinapewa government allocation peke yake lakini kila siku zikienda na uhaba wa ardhi imekuwa kuna uvamizi katika maeneo haya na ndiyo maana sasa tumeona umuhimu wa kupima maeneo yote ya jeshi na kuyapatia hati ili waweze kumiliki kisheria. Wakati tunafanya hayo, tutaendelea kuhakikisha kwamba maeneo ya jeshi yanatunzwa hivyo kuweza kupunguza uvamizi unaotokea katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upimaji na ulipaji fidia kwa maeneo ya jeshi ufanyike. Kama ilivyoelezwa kwenye hotuba yangu, ibara ya 60 na 61 katika ukurasa wa 43 na 44 na kufafanuliwa katika hoja Namba tatu ya ukurasa wa 57, Wizara itaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kukamilisha upimaji na ulipaji fidia kwa maeneo ya jeshi. Natambua Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika maeneo haya ya kutaka uthamini, upimaji na ulipaji wa fidia. Katika bajeti ya mwaka huu kama mtakavyoona katika fedha za maendeleo, tumeweka shilingi bilioni 27.7 lengo ni kuanza kupunguza yale maeneo ambayo yanahitaji kulipiwa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi kutambua na kulinda mipaka yake. Jambo hili sasa linafanyika kwa nguvu zote, tunaweka mabango na tunapanda miti katika maeneo yetu ya mipaka ili wananchi waelewe fika wapi maeneo ya jeshi yanaanzia na wapi yanaishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kurasimisha makabidhiano ya maeneo yanayotolewa na mamlaka za kiraia kwa jeshi na kuweka uzio maeneo yote ya jeshi. Ushauri umezingatiwa, tutashirikiana na mamlaka za mikoa kuhakikisha kumbukumbu za makabidhiano ya ardhi waliyoitoa kwa jeshi zinawekwa vizuri. Uwezekano wa kuweka uzio maeneo yote ya jeshi ni mdogo kwani maeneo hayo ni makubwa sana mfano eneo la Monduli, Tondoroni na Msata. Tunachoweza kufanya ni kuweka ukanda wa tahadhari yaani buffer zone na mabango ya tahadhari ya maeneo yote ya jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uboreshaji wa pensheni za wanajeshi wastaafu hasa kwa ngazi ya kuanzia Private hadi Brigedia Jenerali kwamba limefikia wapi. Serikali imetambua umuhimu wa kuboresha pensheni kwa wastaafu ikiwemo wanajeshi. Hivyo suala hili linaendelea kufanyiwa kazi kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutenga bajeti ya kutosha kuwezesha JKT kuchukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. Ushauri huu umepokelewa na ndiyo azma yetu. Hata hivyo, kama tulivyojibu, Wizara itaendelea kuwasiliana na Hazina ili kutoa fedha za kutosha kuliwezesha JKT kuchukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa wakati mmoja kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, fidia kwa vijana wa JKT wanaoumia wakiwa mafunzoni. Wizara imepokea ushauri wa Kamati na itaufanyia kazi sanjari na kuboresha Sheria ya Ulinzi wa Taifa na sheria iliyoanzisha JKT.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maeneo hayo ambayo yalitolewa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, naomba sasa niingie kwenye hoja ya Kambi ya Upinzani. Kwanza kulikuwa na hoja ya upendeleo katika ajira za jeshi. Labda nielezee kidogo utaratibu unaotumika katika ajira ili tuondokane na wasiwasi kwamba kuna upendeleo. Kwanza niseme tu kwamba ajira jeshini kwa sasa wanachukuliwa vijana ambao wako katika makambi ya JKT peke yake, jeshi halichukui tena uraiani. Kwa maana hiyo ni kwamba wale vijana wanaokwenda JKT wakati wa ajira wanafanyiwa usaili vijana hao, kwa hivyo sioni upendeleo unatokea wapi. Sasa hawa wa JKT wanapatikanaje? Kila mwaka tunatoa nafasi kupitia mikoa hadi wilaya, ili wilaya zenyewe zichuje vijana katika maeneo yao na kuwapeleka JKT. Kwa hiyo, hii hoja ya kwamba kuna upendeleo, kwa kweli sioni upendeleo huo utatokea wapi wakati hatuchukui uraiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa Wizara inalishughulikiaje suala la migogoro ndani ya vyama vya wanajeshi wastaafu. Jibu ni kwamba Wizara kupitia Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, imevishawishi vyama vyote vya wanajeshi wastaafu kuunda chama kimoja tu cha Kitaifa ambacho kitaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za kijeshi. Hivi sasa kuna vyama kama alivyovitaja lakini viko chini ya kanuni za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO‟s). Kwa hivyo, inatupa shida kama Serikali kufanya nao kazi na kuwasaidia kama inavyotakiwa lakini wakiwa chama kimoja ambao watafuata taratibu za kijeshi, bila shaka itakuwa rahisi kwetu kuwapa msaada utakaostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uteuzi wa wanajeshi kwenye nafasi za kisiasa kama ilivyokwishasemwa na walionitangulia AG na wengine, ndugu zangu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumchagua mtu yeyote kwa nafasi yoyote. Kwa hivyo, haijavunjwa Katiba hapa na kwa utaratibu wa sasa wanajeshi wote hawaruhusiwi kujihusisha na vyama vya siasa. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu anayo mamlaka ya kumpangia kazi mwanajeshi yeyote kadiri anavyoona inafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili napenda nikuambieni kwamba yapo maeneo ya nchi yetu ambayo yako katika mipaka yana changamoto nyingi za kiulinzi na usalama ndiyo maana ikaonekana ni busara kupeleka Wanajeshi. Kuna Wilaya kule kuna wakimbizi ambapo hali ya ulinzi na usalama imeharibika kwa sababu ya silaha zinazoingizwa, kwa sababu ya watu wanaoingia kwa mawimbi makubwa ya wakimbizi na kadhalika. Wakipelekwa wanajeshi kule experience imeonesha kwamba kazi ya ulinzi na usalama inafanyika vyema zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali iwaagize Wakuu wa Vikosi vyote vya JKT kutengeneza programu ya uzalishaji mali katika kilimo, uvuvi na mifugo. Kama ilivyoelezwa katika ibara ya 53 ya hotuba yangu, ushauri huu umepokelewa na taarifa za uzalishaji mali na mapato itaendelea kutolewa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Ukweli ni kwamba programu za uzalishaji mali katika vikosi vyote vya JKT zipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itoe fedha zote zitakazotengwa katika bajeti ya Wizara ya Ulinzi. Hili ni kama nilivyosema awali, itategemea sana na mapato ya Serikali lakini ni mategemeo yetu kwamba kwa sasa kwa sababu ukusanyaji ni mzuri, hatuna shaka kwamba fedha zilizotengwa zitaweza kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niingie katika kile kisehemu ambacho kilikuwa kinazua mgogoro, nacho ni jeshi kuingilia kazi za polisi Zanzibar. Ndugu zangu nataka niseme, wakati nachangia hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais nilitoa maelezo ya kina na nilidhani tumeelewana ni kwa nini jeshi wakati wa uchaguzi linakuwa standby. Narudia kusema kwamba wakati wa uchaguzi au nianze kwa kuelezea majukumu ya jeshi, majukumu ya jeshi makuu ni matatu. Kwanza ni ulinzi wa mipaka yetu; pili ni ulinzi wa amani; na tatu ni kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanapohitajika kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati wa uchaguzi Zanzibar, jeshi liliona ni muhimu kukamata major installations kwa ajili ya usalama. Maeneo ya airport, bandari, redio na maeneo mengine kama hayo vililindwa na jeshi kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa ziada lakini hakukuwa na nia ya kumtisha yoyote, nia ilikuwa ni kuleta usalama. Kama walivyosema wengi hapa, naomba nirudie kauli ile kwamba, walinzi ni walinzi anayeogopa mlinzi ni mhalifu. Hakuna sababu kwa nini uwaogope walinzi kama huna nia mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachosema ni kwamba, wanajeshi walikuwa on standby endapo itatokea vurugu na mamlaka ya vyombo vingine vya ulinzi na usalama watahitaji msaada wao wawe tayari kutoa msaada. Hata hivyo, ukweli unabaki pale pale kwamba wakati wa uchaguzi, ninyi ni mashahidi, mimi pia nilikuwa Zanzibar nimepiga kura, sehemu zote zilikuwa zinalindwa na polisi, jeshi walikuwa kwenye barracks zao isipokuwa hizo major installations nilizoelezea hapa, basi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba ni faida gani tunapata kwa JWTZ kushiriki katika operesheni za amani. Kwanza nishukuru kwa wote waliochangia na kusema kwamba kazi inayofanywa na jeshi kwenye ulinzi wa amani ni nzuri, tumepata sifa nyingi na tunawaunga mkono wanajeshi wetu waendelee kutuwakilisha vyema sehemu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, faida tunazozipata kwanza tunapata uzoefu wa Kimataifa na mbinu mpya. Pili, wanajeshi binafsi wanafaidika kwani hupata kipato kwa kushiriki ulinzi wa amani. Tatu, ulinzi wa amani umeliletea sifa jeshi letu Kimataifa. Katika takwimu za ubora zilizotolewa hivi karibuni jeshi letu Kimataifa lipo katika nafasi ya 27 ndiyo sababu sisi tunapata nafasi nyingi za kwenda kulinda amani katika nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na hoja nyingine kama ifuatavyo:-
Ushauri wa kutumia vyombo katika shughuli za maendeleo na uzalishaji. Hili alilitoa Mheshimiwa Shamsi Nahodha nadhani nimeshalisema kwamba taasisi zetu zote zinafanya kazi hii ya kuzalisha mali na kufanya tafiti ili ziweze kupata kipato cha ziada.
Vijana wanaomaliza JKT wasiachwe bila ajira. Kama nilivyosema na alivyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, tuna mambo mawili, si rahisi kuwaajiri vijana wote ambao wanaingia JKT, lakini ni lazima tujipongeze kwa sababu tumefanya kazi nzuri. Takwimu zinatuonesha kuanzia mwaka 2001 - 2015, kati ya vijana wote waliochukuliwa katika makambi ya JKT walioajiriwa ni asilimia 72.9, hawa wameingia katika vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika,Waliobaki ambao ni wachache kama asilimia 30 sasa ndiyo tumekuja na mpango huu wa uwezeshaji, wanapewa mafunzo kule na wakitoka watapewa mitaji ili waweze kujiajiri wao wenyewe. Kusema kuwaajiri asilimia 100 haiwezekani, ingekuwa vyema na ningependa iwe hivyo lakini kwa bahati mbaya bado uwezo wetu haujafikia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na ushauri wa kuwa na database ya vijana wa JKT. Database hiyo ipo kwa wale wanaoajiriwa na wale wanaorudi nyumbani kwa sababu nao ni jeshi la akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuimarisha vyuo vya ufundi stadi JKT ili vijana wapate stadi za kazi. Ushauri umepokelewa, Wizara inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha vyuo vya ufundi stadi JKT kwa kuviwezesha kivifaa na wataalam kadiri bajeti inavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa ardhi Tondoroni, Makuburi na Ihumwa. Tondoroni mgogoro umekwisha kupitia Mahakama kesi namba 48 ya mwaka 2005 ambapo Serikali ilishinda. Hata hivyo, wahusika halali walikwishalipwa fidia kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa Makuburi Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni imeandaa mchoro wa mipango miji kwa kuzingatia marekebisho ya mpaka mpya wa kambi ambapo eneo la jeshi litazungukwa na viwanja vilivyopimwa. Tulichofanya pamoja na kwamba wananchi walivamia eneo la jeshi tumeweka mipaka mipya wao tukawatoa nje ya ile mipaka kuweza kuwa-accommodate ili wasilazimike kuondoka au kulipwa fidia. Kwa maana hiyo, tatizo hapa naliona limekaa vizuri lakini manispaa nayo imechukua jukumu la kuwapimia wananchi wale ili wawe na hati na isiwe tena ni eneo ambalo halijapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Kambi ya Ihumwa halina mgogoro. Tatizo lililopo ni la eneo dogo la nyongeza ambapo taratibu za kulipima na kulifanyia uthamini bado hazijakamilika. Kama nilivyosema tukipata fedha tutakamilisha taratibu hizo ili tuweze kulimiliki kihalali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zungu alitaka pensheni za vyombo vya ulinzi na usalama ziwe na taratibu zake maalum badala ya taratibu hizi za kawaida za utumishi wa umma. Hili ni wazo zuri, tunalipokea na ushauri huu utazingatiwa na tutawasiliana na wenzetu wa Hazina na Ofisi ya Rais, Utumishi ili tuangalie ni jinsi gani tunaweza kufanya lakini sote tunakubaliana na ninyi kwamba kuna baadhi ya wenzetu ambao walistaafu zamani pensheni zao haziridhishi, ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu misheni zetu tunapokwenda nje ya nchi, walitaka kujua fedha za misheni, hili nadhani nimeshalijibu na nitoe tu ufafanuzi wa ziada kwamba ziko fedha ambazo zinapatikana ukiacha zile ambazo wanalipwa wanajeshi wenyewe, sisi tunawalipa asilimia 80 ya zile zinazolipwa kutoka kule UN lakini jeshi pia linapata fedha kwa ajili ya kuwa na zana zake kule na pili matengenezo na tatu kuweza kupeleka zana mpya. Kwa hiyo, malipo ya fidia ya UN yanatolewa na fedha hizo zinalipia posho kwa wanajeshi, kugharamia ukarabati wa zana, kununua vifaa na zana mpya, kuandaa vikosi vipya kwenda kubadili vile vinavyorejea na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya kutaka kujua tofauti ya Chapter Six na Chapter Seven katika malipo. Malipo ya fidia ya UN hayatofautishi kama ni operation ya Chapter Six au ya Chapter Seven, yote yanafanana na ni sawa, ni chapters zinazotofautisha utendaji katika eneo la ulinzi na amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wanajeshi wetu waliopoteza maisha au kuumia kwenye operations hizo wote walishalipwa kikamilifu kwa mujibu wa taratibu za UN na za JWTZ. Kwa sasa hakuna familia yoyote inayolidai jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lililochangiwa lilikuwa ni suala la Duty Free Shops kama alivyochangia Mheshimiwa Maryam Msabaha kwamba bidhaa zinazouzwa kule hazina nafuu na zile zinazouzwa mitaani. Tumepata malalamiko haya na nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalifanyia kazi kwa nguvu kabisa. Lengo letu ni kwamba mashirika yetu ya jeshi ndiyo yaendeshe maduka haya ikiwemo Mzinga ambao wameshaanza katika baadhi ya vikosi, tunataka Suma JKT waingie ili hatimaye maduka yote ya jeshi yaendeshwe na jeshi lenyewe na kwa kufanya hivyo tutaondokana na tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za mabwalo kweli tunalo tatizo na kazi ya ukarabati wa mabwalo linatekelezwa kwa kadiri bajeti zinapopatikana. Ni kweli kwamba mabwalo mengi kwa sasa hali yake sio nzuri kutokana na uhaba wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kuhusu bajeti, madeni na maeneo ya jeshi, nadhani hili tumeshalitolea ufafanuzi. Tumesema kwamba bajeti ikiruhusu tutahakikisha tunaondoa matatizo yote haya yanayoonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali moja lilikuja kuhusu wastaafu kulipwa kila mwezi. Tunachosema ni kwamba wala hatuna tatizo na wastaafu kulipwa kila mwezi kwa sababu hapo awali wastaafu walikuwa wanalipwa kila mwezi, ni wastaafu wao wenyewe waliomba kwamba sasa walipwe kwa miezi sita, walidai kwamba ile pensheni ya kila mwezi ni ndogo na wanakuwa wameshakopa, kwa hiyo, angalau wapewe ya miezi sita, wakapewa ya miezi sita. Baadaye wakabadilisha wakasema hiyo inakuwa muda mrefu sana, wakaletewa ya miezi mitatu. Kwa hiyo, kama sasa hivi wako tayari kurudi mwezi mmoja wala sioni tatizo lolote, haya ni matakwa ya wastaafu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uanzishwaji wa bima ya afya kwa wanajeshi hili tunalipokea na tunaona umuhimu wake. Bima ya afya kwa wanajeshi ni muhimu kwa sababu sasa hivi tunapata shida sana, bajeti ya kutoa huduma za afya jeshini haitoshelezi na kwa maana hiyo tunao mpango wa kuanzisha bima kwa ajili ya wanajeshi wote, wawe kazini au wastaafu ili hatimaye tuondoe matatizo yao ya kupata huduma zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yaliyochangiwa kama nilivyosema ni mengi, naomba sasa niingie kwenye hoja za Mheshimiwa Sophia Mwakagenda. Anasema Amiri Jeshi Mkuu kuvaa sare za jeshi yeye anaona hili sio sawasawa. Kwanza nieleze kwamba Uamiri Jeshi Mkuu siyo cheo bali ni wadhifa. Kwa mujibu wa taratibu za kijeshi, Amiri Jeshi Mkuu anapoamua kuvaa sare ya jeshi katika shughuli yoyote ile ya kijeshi kama vile kufika katika eneo la mazoezi ya kijeshi, anaruhusiwa kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili wala halijaanza hapa kwetu wala halijaanza katika awamu hii, Baba wa Taifa alivaa sare za jeshi, hapo nchini Kenya juzi juzi tu tumeona Rais Kenyatta kavaa sare za jeshi. Sioni kwa nini hii inakuwa hoja kubwa kwa sababu yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu. Anapoamua kuvaa afanane na wanajeshi wakati anaenda kwenye mazoezi yao wala hakuna tatizo hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wanajeshi wastaafu kuvaa sare za jeshi, maelezo ni kwamba mwanajeshi mstaafu anaweza kuvaa sare za jeshi katika shughuli yoyote lakini awe amepata kibali cha Mkuu wa Majeshi. Mkuu wa Majeshi huwa anatoa vibali hivyo kwa shughuli maalum ikiwemo ile ya kuapishwa Wakuu wa Mikoa alitoa kibali wavae kwa sababu wala hakuna tatizo, wale ni wanajeshi kwa sasa baada ya kustaafu ni jeshi la akiba, watakapohitajika wakati wowote wanaitwa ili waweze kufanya kazi za jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kai alikuwa na hoja ya kukosekana kwa fedha za maendeleo kwa Ngome. Hili nimeshalizungumza toka awali, tunaelewa changamoto za bajeti na hii ni kwa Serikali nzima na wala siyo Wizara ya Ulinzi peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja pia kukosekana kwa fedha za kulipia fidia maeneo ya ardhi. Kama nilivyosema mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 27.7, ni mategemeo yetu kwa kiwango kikubwa tutaweza kupunguza tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa marudio Zanzibar. Jeshi kupelekwa Zanzibar Waziri atafute maneno mengine lakini siyo kwamba hawakupelekwa. Ndugu zangu naomba nirudie, nilisema hivi, watu wakisikia kwamba tunasema jeshi lilipelekwa Zanzibar wakati wa uchaguzi kila mtu atadhani jeshi halipo Zanzibar. Zanzibar kuna brigade siyo platoon wala siyo kombania kuna brigade. Brigade ya askari wa infantry iko Zanzibar na isitoshe kuna vitengo vya wanamaji, kuna vitengo vya airforce. Sasa tunapokuwa tunabishana kwamba jeshi lilipelekwa au halikupelekwa, naona haina msingi sana kwa sababu tayari jeshi lipo Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi liko Zanzibar kwa dhumuni moja tu, nalo ni kulinda mipaka ya nchi yetu ya ujumla ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiyo kazi yake ya msingi kulinda mipaka yetu. Kwa hiyo, haiwezekani wasiwepo wakati mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko mpaka kule Zanzibar. Kwa hiyo, nadhani kama walipelekwa au hawakupelekwa isiwe hoja, hoja ni kwamba jeshi liko pale kwa kazi moja ya kulinda mipaka yetu na wakati wa uchaguzi kama ilivyo international standard kwa nchi zote wanajeshi wanakuwa standby ili kukitokea machafuko waweze kusaidia, basi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi limetumika kuwatisha watu waliotulia. Mimi nasema jeshi limekuweko pale kusaidia watu watulie kwa sababu matukio yalikuwepo na wala hatuwezi kukataa. Mabomu yalirushwa wala sisemi mimi vyombo vya habari vimesema karibia na uchaguzi na wakati wa uchaguzi si kulikuwa na mabomu ya mkono yanarushwa, si yalitokea? Sasa kweli jeshi lisingekuwepo ile hali ya usalama na amani ingekuwepo mpaka leo? Sisi tunasema jeshi liko pale kwa kazi moja ya kulinda amani si kwa kazi ya kumtisha mtu yeyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba wanajeshi wa ngazi ya chini wanalipwa ration allowance tofauti na wa ngazi ya juu, si kweli. Jeshini ration allowance ni moja tu, anayopata private na anayopata general ni hiyo hiyo. Kama umepata taarifa kwa mtu yeyote si kweli, hapa nakataa kabisa, ration allowance ni hiyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Fakharia anasema nafasi za ajira za Zanzibar, kwa nini vijana wasichukuliwe kutoka JKU badala ya kupitia mikoani na wilayani. Jibu ni rahisi, sisi huwa tunapeleka nafasi za Zanzibar kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Tunawaachia uhuru wa kuamua wanazigawa kwa taratibu gani. Wakiamua kupeleka mkoani na wilayani ni juu yao, wakiamua kupeleka JKU ni juu yao. Kwa hiyo, kama tunaona JKU ni utaratibu mzuri zaidi kwa pamoja sisi Wabunge wa Zanzibar tuishauri SMZ ichukue vijana hao kupitia JKU. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba za makazi zijengwe na Unguja pia, hii iko katika mpango wetu wa Awamu wa II. Awamu ya I kwa Zanzibar ilianza Pemba na Awamu ya II tutapeleka Unguja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanajeshi wastaafu kulazimika kwenda Bara kushughulikia mafao yao. Hili nalikubali kwamba ni usumbufu, hawa watu hawana fedha, wanatakiwa wasafiri mpaka makao makuu, tutatengeneza utaratibu ili brigade pale ishughulike na mafao haya kwa kuwasaidia kuchukua maelezo yao wao wayapeleke makao makuu ili waweze kupata huduma kwa urahisi bila kusafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maswali ya Khadija Hassan Aboud ambapo yeye alishauri vijana wa JKT waajiriwe jeshini. Napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba ndivyo tunavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, aliendelea kushauri JKT iwe na aina mbili za mafunzo wale wa ujasiriamali na wale wa kuingia jeshini, tunadhani kwa sasa huo hautakuwa utaratibu mzuri sana kwa sababu uwezo wa kufanya hivyo hatuna. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba lengo la JKT si kutoa ajira ni kuwafunza vijana wetu wa Kitanzania uzalendo, utaifa na kuhakikisha kwamba wakiwa pale basi wanapata mafunzo ya kijeshi lakini pia ujasiriamali kwa maana ya stadi za kazi ili waweze kujiajiri. Kwa hiyo, hili tutalitazama kwa wakati ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niingie katika hoja za Mheshimiwa Kubenea ambazo kwa kweli zimenisikitisha sana kwa sababu hazina punje ya ukweli ndani yake. Nasikitika kusema kwamba Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano anaweza akachukua maneno ya mitaani akaingia nayo ndani ya Bunge akayasema bila ya kuwa na ushahidi, hii ni hatari tena ni hatari kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwarifu Mheshimiwa Kubenea, sijui kama yupo humu ndani…
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakiongea bila mpangilio)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuhuma anayoitoa kwamba jeshi limeingia mkataba na kampuni inayoitwa Hainan Construction ambapo jeshi litatoa eneo kubwa la ardhi kwa kampuni hiyo ili ijenge nyumba na kwamba kampuni hiyo itatumia kwa miaka 40 hazina punje ya ukweli ndani yake. Si kweli na naku-challenge ukiweza kuniletea uthibitisho huo mimi nitajiuzulu kwa sababu maneno unayoyasema ni ya mitaani. Nasikitika sana Mheshimiwa Mbunge kuleta maneno yasiyokuwa na uthibitisho kwa sababu maneno hayo ni ya uwongo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili alilolisema ambalo limenihuzunisha zaidi, anasema kampuni hiyo hiyo itaingia mkataba pia wa kumjengea nyumba Dkt. Hussein Mwinyi, huu siyo mgongano wa kimaslahi? Naliomba Bunge lako litumie utaratibu wa kikanuni, Mheshimiwa Kubenea akishindwa kuthibitisha maneno haya achukuliwe hatua stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwa sababu tusije ndani ya Bunge tukaharibu majina ya watu, tukawadhalilisha kwa sababu tu ya kuwa na uhuru wa kuzungumza ndani ya Bunge na immunity tunayopewa. Nasema uhuru tunao, immunity tunayo lakini kudhalilisha watu kwa maneno ambayo hayana ushahidi kukomeshwe. Huu ni uwongo mtupu, hakuna jambo kama hili. Kwanza hiyo kampuni hata kuwajua siwajui. Pili, haiwezekani maneno haya akayaleta kama hakuna mkataba wa ushahidi kama anao alete tuuone, hakuna hiki kitu, ni uwongo mtupu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kubenea aliendelea kusema kuwa kuna tuhuma za udhalilishaji kwa wanajeshi wetu waliokwenda kulinda amani Kongo, je, ni hatua zipi zimeshachukuliwa hadi hivi sasa? Nataka nimweleze Mheshimiwa Kubenea kwamba, tuhuma zinapotolewa ni wajibu wa mamlaka zinazohusika kuchunguza, huwezi kuvamia tuhuma ukachukua uamuzi. Jeshi liliunda Bodi ya Uchunguzi, wamekwenda Kongo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa ufanyike uchunguzi wa kina ili watakapokuja kutoa taarifa za uchunguzi na ikithibitika kwamba kuna unyanyasaji wa kijinsia ulifanyika au walifanya askari wetu hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya waliofanya vitendo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi hili linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za jeshi, kwa hivyo, hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya jambo lolote kinyume na utaratibu akaachiwa lakini tunachosema uchunguzi ni lazima ufanyike. Udhalilishaji uliosemwa na Umoja wa Mataifa ni pamoja na ubakaji, baadhi ya watu wamedai katika ubakaji huo wamepata watoto, unafanyaje uamuzi wa kwamba huyu amekosa bila kufanya DNA test ya kugundua kama hao watoto kweli ni wa huyo anayeambiwa ni baba yao? Kwa hiyo ni kwamba uchunguzi unaendelea na ni mategemeo yetu kwamba utakapokamilia na ukithibitika hatua stahiki zitachukuliwa. Hii ni kawaida kabisa wala Mheshimiwa asipate tatizo lolote hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine nyingi ambazo zimetolewa, lakini nadhani kwa ujumla wake nimezi-summarize kwa pamoja ili tuweze kupata maelezo ya ujumla lakini nitakuwa tayari kutoa maelezo ya ziada nitakapohitajika. Kama nilivyosema awali wakati wa vifungu pia nitakuwa tayari kutoa maelezo kwa kadiri yatakavyohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.