Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nami naomba nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa kupata fursa ya kuweza kuchangia mada iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, mimi nitalenga zaidi kwenye masuala mawili; suala la kwanza, nitazungumzia mfumuko wa bei, hasa kwa bidhaa ambazo zinatokana na kilimo; pili, nitazungumzia kuhusiana na mashamba ya maua ambayo mengi yako kule Mkoani Arusha.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba hali ya kipato cha Mtanzania wa kawaida ni ngumu, tunafahamu kwamba kuna changamoto kubwa sana ya ajira katika nchi yetu, watu wengi wanamaliza vyuo vikuu, wanamaliza shule lakini hawapati ajira kiasi ambacho kinawasababisha kuwa na ugumu kwenye maisha.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba kuna changamoto pia kwenye masuala yanayohusiana na mishahara yetu. Tukiangalia kwa mfano kwenye sekta binafsi mishahara kwa kiwango cha chini imetoka kwenye shilingi 120,000 mpaka shilingi 140,000 kwa maana kuna ongezeka la kama shilingi 20,000; tumeona pia kwenye sekta ya umma tumetoka shilingi 300,000 mpaka shilingi 375,000 kwa maana ya kwamba tumeongezewa kwa shilingi 75,000.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nasema hayo ili nitakapozungumzia mfumuko wa bei tuangalie na athari tulizokuwa nazo kwenye maisha yetu ya kila siku kwenye mishahara pamoja na changamoto mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia website ya Wizara ya Kilimo ambayo imetoa data mbalimbali kuhusiana na bei za vyakula nchini, ukiangalia kwenye upande wa mchele inaonekana mwaka 2020 kilo moja ya mchele ilikuwa ni shilingi 1,486 lakini mwaka 2023 kilo moja ya mchele inaonekana ni shilingi 2,888. Hii kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo ni bei ya jumla, bei ya sokoni. Kwenye upande wa mahindi imetoka shilingi 570; mwaka 2020 mpaka shilingi 1,160 na mwaka 2023 na upande wa maharage imetoka shilingi 2,040 mpaka shilingi 2,916.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia hapa tu kwa mujibu wa maelezo ya Wizara ya Kilimo ambayo yanasema kwamba mfumuko wa bei umetokana na sababu nne; kwa maana ya UVIKO-19, vita ya Urusi na Ukraine, kupanda kwa bei za mafuta na mabadiliko ya tabianchi. Kwa maoni yangu, sababu zote za UVIKO, mabadiliko ya tabianchi, vita ya Ukraine zimeangaliwa kutoka shambani mpaka walivyosafirisha hadi zikafika sokoni ndiyo maana bei leo imeweza kuwa shilingi 2,888 kwa mchele; shilingi 1,160 kwa mahindi na shilingi 2,916 kwa maharage.
Mheshimiwa Spika, ukiacha hiyo bei ya jumla sasa ukienda kwenye soko lenyewe kwa maana ya bidhaa ya rejareja. Ukitembelea Soko letu la Majengo hapa Dodoma unakuta mchele unauzwa mpaka shilingi 3,400. Ukienda kule Arusha unakuta mchele unauzwa mpaka shilingi 3,500. Sasa ninajiuliza kwamba kutoka shilingi 2,888 kama wastani hadi kufika shilingi 3,500 sasa pale role ya Serikali ni nini?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu inavyoonekana sasa hivi wafanyabiashara kama wako huru sana kujiamulia kupanga bei wanavyotaka. Maana kutoka shilingi 2,888 mpaka shilingi 3,500 nadhani difference ni kubwa kwa sababu mzigo mkubwa tayari umeshabebwa; mzigo wa usafirishaji kutoka shambani mpaka kufika sokoni, mzigo wa pembejeo tayari mkulima alishaubeba kule.
Mheshimiwa Spika, huyu anayetoa Soko Kuu la Arusha au anayetoa Soko Kuu la Majengo anakwenda kupeleka dukani kuuza rejareja kwa nini gap limekuwa kubwa. Mimi naona hapa kuna kazi ya Serikali ya kufanya ya kusimamia mfumuko wa bei na siyo kuacha tu bei iwe ni ya kiholela kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ukiangalia hii taarifa yenyewe ambayo imetolewa kwenye website ya Wizara ya Kilimo unaona kabisa inawatia moyo wafanyabiashara kuendelea kuuza bidhaa kwa bei ya juu. Ukiangalia mfano taarifa yao hii ya tarehe 2 hadi 6 Januari, 2023, kwa upande wa Mkoa wa Dodoma wanatuambia kwamba mchele unauzwa shilingi 3,400 kwa maana ya rejareja lakini mhusika kule amenunua kwa shilingi 2,775, kwa hiyo kuna ongezeko kama la shilingi 625.
Mheshimiwa Spika, upande wa Arusha pia ukiangalia ni shilingi 4,000 lakini yeye amenunua bei ya jumla shilingi 2,900 kwa hiyo kuna ongezeko kama la shilingi 1,100. Lakini kibaya zaidi ukiangalia Mkoa wa Kilimanjaro, Wizara ya Kilimo yenyewe inatuambia kwamba bei ya mchele sasa hivi kwa bei ya jumla ni shilingi 3,500.
Mheshimiwa Spika, sasa nikawa najiuliza, kama pale Arusha naweza nikanunua mchele kwa bei ya jumla ya shilingi 2,775, inakuaje Kilimanjaro nanunua kwa shilingi 3,500? Ni rahisi sana kwa mwananchi kupanda daladala kutoka pale Kilimanjaro akalipa nauli shilingi 5,000 akafika Arusha akanunua mchele akarudi Kilimanjaro akatumia shilingi 10,000. Lakini ukiangalia gharama ambayo imeongezeka hapa siyo chini ya shilingi 500. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba japo kuwa Serikali imejificha kwenye vita vya Ukraine, UVIKO na mabadiliko ya tabianchi lakini bado kuna kazi ya kufanya ili kuondoa mfumuko wa bei kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu, naomba Serikali yetu iwaangalie wananchi hawa kwa jicho la huruma. Manung’uniko ni mengi, vilio ni vingi.
Mheshimiwa Spika, na kinachonisikitisha hii hela wala hapati mkulima. Kwa sababu kama katika hali ya kawaida nikienda kwenye bei ya jumla ni shilingi 2,950, sasa hebu niambie hii analipwa mfanyabiashara yule wa jumla, je, ndiyo fedha ambayo anapata kweli mkulima wa kawaida?
SPIKA: Mheshimiwa Gambo; Mheshimiwa Waziri amesimama.
T A A R I F A
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ninataka nimpe taarifa kwamba; moja, Serikali haijajificha kwenye anachosema Ukraine wala UVIKO, wala tabianchi. Nimpe taarifa kwamba haya mambo ya Ukraine na UVIKO ni halisia, yaani siyo kisingizio. Haya ni mambo halisia.
Mheshimiwa Spika, na Serikali imechukua hatua ambazo kwa East Africa na SADC hakuna nchi imezichukua, za kutoa shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kupunguza gharama. Ndiyo maana unaona hata nchi majirani wanakimbilia kuchukua hivi vitu kutoka katika nchi yetu; shilingi bilioni 100 kila mwezi.
Mheshimiwa Spika, na siyo hapo tu, Serikali ikaondoa kodi na tozo zote kwenye mafuta ya kula, kwenye wheat flour na ikachukua nusu ya bei ya kila mfuko wa mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitaka kufanya tathmini halisia, ondoa hii gharama ambayo imechangiwa, uone hizi bei zingekuwa wapi. Kwa sababu tusiongelee tu bei iliyopo tukaona hamna kilichofanyika, tunapofanya proximation hizo, weka kama isingekuwepo hiyo bei, uichukulie ile bei ambayo inge-trend. Ndiyo maana bei ya hizi bidhaa ndiyo ziko juu, lakini kwa sababu dunia nzima ziko juu kwa Tanzania iko chini ukilinganisha na nchi za East Africa na za SADC lakini hata maisha hayo fuatilieni kwa nchi zingine za Ulaya na Marekani kote kule kumebadilika kumeenda tofauti.
Mheshimiwa Spika, hivyo, nilitaka nitoe taarifa pamoja na kwamba kuna jitihada zingine tunaendelea kuchukua, ukiona jitihada ambazo zimechukuliwa na Kilimo na zilizochukuliwa na Viwanda na Biashara jitihada zinaendelea lakini lazima tu-recognize jitihada ambazo zimeshafanyika, Serikali iko macho sana kwenye haya mambo na inaendelea kuchukua hatua. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mrisho Gambo, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, mimi siipokei kwa sababu ni wajibu wake kuitetea Serikali kwa hiyo mimi naomba nisiipokee na nimpongeze kwa kazi yake nzuri ya kuitetea Serikali.
Mheshimiwa Spika, nitampa mfano mmoja tu, mwaka 2022 mwishoni kwa mjibu wa taarifa ya Serikali, ilikuwa inaonekana mchele ni shilingi 2,090 na nikisema shilingi 2,090 sizungumzii shambani, nazungumzia mkulima ameshalima Serikali ime-subsidize mbolea zote zimeshaingizwa, Mkulima ameshauza, dalali amechukua amepeleka sokoni Dar es Salaam, Arusha au Dodoma. Leo mtu ambaye amenunua kwa shilingi 2,090 anakuja kuuza kwa shilingi 3,500 sasa pale UVIKO unaingiaje? Pale vita ya Ukraine inaingiaje?
Mheshimiwa Spika, kuna mahali unaweza ukaona Serikali ime-subsidize ndio maana tukafikia Shilingi 2,090. Tunasema baada ya hapo sasa mbona huku hamuangalii kwa wananchi kunakoendelea, watu wanaamua tu kujiuzia tu wanavyotaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, hili jambo la mfumuko wa bei siyo jambo jepesi, sisi wote tunatokana na Serikali hii na Chama chenye Serikali hii, lakini tunao wajibu wa kuwasemea wananchi siyo kutetea kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Serikali kwa ujumla watusaidie kwenda kufanya utafiti na kuangalia kama kuna mahali popote wafanyabiashara wanaongeza gharama waende wakasimamie. Tumeona huko siku za nyuma, wafanyabiashara walikuwa wakisikia tu Mwezi Ramadhani unakaribia walikuwa wanapandisha Sukari. Serikali ilikuwa inaingia kila mahali kwenye masoko na maeneo yote, bei ilikuwa inakuwa stable, sasa hivi kigugumizi cha nini? Tunaacha watu wajifanyie wanavyotaka?
SPIKA: Sekunde thelathini, malizia.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia naona muda wa hoja yangu ya pili hautakuwepo lakini ombi langu kwa Serikali tuangalie uwezekano wa kutoa kipaumbele kwenye mfumuko wa bei, hili jambo ni kubwa na lina maslahi mapana kwa nchi yetu. (Makofi)