Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa muda huu wa kuweza kuchangia maazimio ya Kamati zetu mbili zilizowasilishwa mahali hapa kwa ajili ya maendeleo na mustkabali wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mungu ambaye ametulinda na ametupa muda huu tukiendelea kupumua na kuwa wazima wa afya njema.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuingiza ruzuku na kuwapunguzia wananchi makali kwenye mbolea. Tumeona jitihada za mwaka huu, wananchi wengi wamelima, mazao yatakuwa mengi sana mwaka huu kwa sababu kila mwananchi amelima na kutumia mbolea.

Mheshimiwa Spika, changamoto kwenye mambo mazuri lazima ziwepo. Mbolea zile zilitakiwa zifike katika maeneo yetu ya vijiji, lakini ilishindikana ikafika kwenye maeneo yetu ya wilaya, na wananchi wameendelea kulima na kununua mbolea kwa wingi kwa ajili ya faida na mafanikio ya Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona ni kwa nini miradi mingi haiendi kwa haraka na kwa nini miradi mingi inachelewa? Kwa kipindi hiki cha miezi sita, Wizara ya Kilimo imepokea asilimia 17 tu. Wizara ya Kilimo ina miradi mingi ya umwagiliaji ambayo haikufikiwa vizuri kupitia Wakandarasi ambao wamewekwa katika maeneo ya miradi hiyo. Miradi mingi mpaka sasa hivi haijaenda vizuri kutokana na kwamba fedha hazijawafikia Wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa tumeliona Hazina. Hazina wanachelewesha fedha na kusababisha kutofikia yale malengo. Kwa sababu sasa hivi ni miezi sita, lakini ni asilimia 17 tu katika Wizara ya Kilimo, ina maana hayo maendeleo yatakuwepo? Tukiangalia ruzuku ya mbolea, ilipangiwa shilingi bilioni 150, mpaka sasa hivi Wizara imepokea shilingi bilioni 50. Ina Wakandarasi wale ambao wanaingiza mbolea nchini wamepokea robo ya zile fedha. Ndiyo maana umekuta mzunguko wa mbolea umekuwa shida katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kuna mbolea ambazo hazijafika, na kuna mazao ambayo yanahitaji mbolea, hususan wakulima wa tumbaku. Kama imechelewa kufika katika maeneo ya wakulima mpaka zao la mbolea likaanza kuharibika, ina maana hapo tunamwondoa mkulima katika hali ya kulima lile zao kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, vile vile naomba niishauri Serikali, ndani ya nchi yetu kuna maeneo ambayo yanajulikana kabisa; kama Mkoa wa Katavi, Kigoma na Kagera, mvua zinaanza mwezi wa Kumi, lakini mbolea zinakuja Januari. Huyu mkulima ameshalima. Leo hii anaichukua ile mbolea anaweka tu basi afanyaje lakini msimu wake wa kuweka mbole umeshapita. Nilikuwa naomba Serikali ijipange vizuri kupitia mbolea. Inatambua kabisa mikoa ya huku Rukwa, Katavi, Kigoma pamoja na Kagera wanaanza msimu wao wa kulima mwezi wa Kumi. Ina maana mbolea inatakiwa Mwezi wa Nane iwe imeshafika site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iboreshe kwenye masuala ya mbolea ili kuendelea kuhamasisha wananchi kulima kupitia Rais ambaye amewapa ruzuku ya mbolea na wananchi wamefurahi. Sasa zile jitihada za Rais zisiweze kupotea bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nipongeze Wizara ya Maji, wanafanya kazi kubwa sana. Tumeona Mheshimiwa hapa amesema, tulienda kukagua miradi ya Dar es Salaam, DAWASA. Jitihada zilizofanyika kwa kipindi cha ukame, maji Dar es Salaam ilikuwa shida, lakini Wizara ya Maji kupitia Shirika la DAWASA likafanya kazi kubwa na kuondoa kabisa ule upotevu wa maji. Sasa hivi wananchi wanapata maji kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naenda kwenye miundombinu. Naomba niungane kabisa na Kamati kuhusu masuala ya Shirika la TAA. Viwanja vya ndege sasa hivi vinatengenezwa na TANROADS. TANROADS wameshakuwa na majukumu mengi. Wana madaraja makubwa, barabara na sasa hivi tumeona nchi yetu barabara nyingi zinatakiwa kufanyiwa marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naunga mkono Kamati ya Miundombinu waliposema kuwa hii miradi ya viwanja vya ndege warudishiwe TAA ili waweze kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu mzuri ili yale mambo tunayotaka yafanyike yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi tunaona hata kwenye Wizara yetu ya Kilimo kuna wananchi mbali mbali, vikundi mbali mbali wanalima mboga mboga na maua, ambapo mwisho wa siku yanatakiwa yatoke katika nchi yetu yaende katika nchi nyingine. Ina maana tukiwaachia TAA watafanya kazi vizuri, viwanja vitajengwa kwa haraka na kupitia mapato yao ya ndani wataendeleza pale palipopungua kwenye fedha ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana niungane mkono na Kamati ya Miundombinu kuhusu miradi yote ya viwanja vya ndege virudishwe TAA.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Kamati yetu ya Kilimo, ahsante. (Makofi)