Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia taarifa yetu ya mwaka ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Nianze kusema kwamba naunga mkono hoja mapendekezo yote ambayo yamependekezwa kwa Serikali kwa ajili ya kuboresha Sekta zetu za ushalishaji.
Mheshimiwa Spika, nitaongelea mambo mawili au matatu kutegemeana na muda. Nianze kwa kusema kwamba athari za mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri sana kwa maana ya kwamba tumeshuhudia ukame mkubwa, vifo vya mifugo na wanyama na pia mvua kidogo, na hata zinaponyesha siyo kwa wakati na wakati mwingine zikinyesha, zinaleta mafuriko yote ambayo yameleta upungufu wa maji. Kwa jinsi hiyo, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, Serikali ikajielekeza katika ujenzi wa mabwawa ili kuhakikisha kwamba tunapata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, maji kwa ajili ya umwagiliaji na maji kwa ajili ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, sasa hoja yangu iko katika utekelezaji wa jambo hili. Tunachokiona ni kwamba kwa sababu ya msukumo, kila Wizara sasa inakwenda na kujenga bwawa. Ukifika Chamakweza utakuta Bwawa la Mheshimiwa Ndaki, ukienda upande huu unakuta Bwawa la Mheshimiwa Aweso, ukienda upande huu unakuta Bwawa la Mheshimiwa Bashe, yaani Wizara tatu au nne zote zinaenda kujenga mabwawa ambayo design ni tofauti. Life time, yaani bwawa litakaa muda gani, wakati mwingine haijulikani. Standard ni tofauti, fedha inayotumika na viwango ukiyalinganisha pia ni tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuishauri Serikali kwamba ili tuweze kupata tija katika msukumo wa jambo hili, Wizara zote ambazo zinadhani kwamba zinapaswa kuwa na mabwawa kwa ajili ya kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi ziwe coordinated ili tupate sehemu moja ambapo tunapata design, itakayotusaidia kuelewa kwamba bwawa letu litadumu kwa wakati gani?
Mheshimiwa Spika, kuna mabwawa ambayo tumeyatembelea, yamejengwa mwaka 2022 lakini mwaka huu 2023 ng’ombe wameshapasua uzio na wanaingia ndani ya bwawa. Hiyo haiwezi kuleta tija. Kwa hiyo haya mambo yaweze kuratibiwa mahali pamoja ili tuweze kupata tija inayotokana na ujenzi wa mabwawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine; katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo tumeishuhudia Serikali yetu ikiyatekeleza, mingi sana ya miradi hii ni kwamba inajengwa na Wakandarasi wa nje. Utakuta mjenzi ni Kandarasi wa nje lakini hata mshauri wa mradi ni kandarasi wa nje. Hali hii inawanyima wakandarasi wetu wa ndani uwezo na ujuzi ambao ni muhimu sana kwa wakati ujao. Kwa sababu hata sisi tunatamani hapo baadaye kampuni zetu, za Watanzania ziweze kuwa na uwezo wa kufanya hii miradi mikubwa na ikiwezekana na sisi tuweze kupata kandarasi katika nchi za nje. Sasa hili halitawezekana iwapo kandarasi zote wanachukua wale wa nje na hakuna sheria inayombana yule kandarasi wa nje kumtumia mtu wa hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, fedha nyingi tunayoipata kwa njia ya mikopo na fedha ya kodi za Watanzania utakuta zote zinatumika kwenda nje ya nchi na hapa ndani tunabakia na fedha za vibarua. Sasa hili jambo tunadhani ni kwamba Sera ya Uwezeshaji ya Kitaifa ipo ya local content, kinachoonekana ni kwamba haisimamiwi vizuri au haitumiki kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuiombe Serikali, tunaisihi sana Serikali katika hili iweze kuhimiza habari ya local content katika miradi mikubwa inayofanyika hapa nchini. Tungejikuta kwamba baada ya kumaliza ujenzi wote wa miradi hii kuna baadhi ya kampuni za Watanzania ambazo zimeshajijengea uwezo hata nao kuanza kuwa kampuni za Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja yangu hapa ni kwamba local content, Sera yetu ya Taifa iliyopo iweze kusimamiwa vizuri. Kwa sababu kwa jinsi ilivyo sasa hivi, haisimamiwi vizuri hata kidogo au haitumiki kabisa. Kwa hiyo, Watanzania na kampuni zao wanaendelea kuwa na kazi zile ndogo ndogo wakati zile zenye tija na faida kubwa zinaendelea kuwa ni zile za kandarasi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, tumeongea juu ya upungufu wa samaki Ziwa Victoria, na sababu zinaeleweka. Kuna uvuvi haramu wa kutumia matimba na wanaotumia matimba; matimba ni kitu kikubwa, siyo kitu ambacho kinafanyika kwa kificho. Pia, kwa sababu ya upungufu wa samaki ambao inasemekana Ziwa Victoria sasa samaki wazazi ni pungufu ya asilimia 0.4. Mazalia ya samaki kule ziwani yanajulikana yalipo, lakini yameshambuliwa, sasa haya yanafanya vile viwanda vya samaki pale katika Mwambao wa Ziwa Victoria yanakosa malighafi na kwa hiyo, hata ajira zinapotea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, itafikia wakati tulipokwa ni kinara wa kusafirisha minofu ya samaki nje ya nchi, hatimaye tutashindwa. Ninaloliona hapa ni kwamba kuna mambo mengine ambayo kunakosekana alertness (nakosa neno zuri la Kiswahili) upande wa Serikali. Kwa sababu kuna mambo ambayo huhitaji kujadili, unahitaji kuchukua hatua za haraka ili tuweze kuponyesha hali ya maziwa yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba alertness upande wa Serikali ichukue hatua za haraka na maamuzi ya haraka wakati mwingine ili tuweze kuokoa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, naona kengele yangu imegonga. Nakushukuru, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)