Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa fursa kuweza kuchangia katika Taarifa ya Kamati. La pili niishukuru Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji inayoongozwa na Dkt. Ishengoma kwa ushirikiano na support wanayotupa na wajumbe wote wa kamati kwa ushirikiano na support wanayotupa. Mapendekezo mengi waliyoleta mbele yako na sisi upande wa Serikali tunayaunga mkono na tutaenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kwanza umenitaka nitoe taarifa kuhusu TARI Ilonga. Ni kweli shamba letu la kuzalisha mbegu za msingi za awali za TARI Ilonga wafugaji waliingia na kuharibu eneo kubwa. Nataka kulitaarifu tu Bunge lako Tukufu ni kwamba kama Serikali tulichukua hatua za haraka. Kwanza kuhakikisha kwamba tunarudisha uzalishaji wa zile mbegu za msingi ambazo ni muhimu kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo, lakini hatua ya pili ambayo tumeamua kufanya kama Serikali ni kwamba mashamba yote ya uzalishaji wa mbegu sasa tunayawekea fence ili kuondokana na hili tatizo la kuvamiwa na mifugo na ambalo limekuwa ni chanagamoto kubwa katika maeneo ambayo tunapatikana na wafugaji; na kuhakikisha kwamba tunaondoa hii changamoto ya kuvamia mashamba na kuweza kuondoa tatizo la magugu kwenye mashamba ya uzalishaji wa mbegu. Kwahi yo nataka nikutaarifu tu na kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba hakuna athari yeyote itakayotokana na mpango tuliyokuwa tumeuweka katika mwaka huu wa fedha kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu kutokana na matatizo yaliyokuwepo.
Mheshimiwa Spika, nilitaka nichangie maeneo machache. Eneo la kwanza ni la ruzuku ya mbolea. Nikiri kwamba kuna changamoto, na changamoto inatokana kutokana na distribution network na kwanini kumekuwa na changamoto kubwa.
Mheshimiwa Spika, msimu wa kilimo wa 2021/2022 ambao mazao yake ndiyo tunatumia leo nchi yetu ililima jumla ya leo la kilimo hekta million 10.1, ndilo tulilolima kama nchi nzima. Baada ya Serikali kutangaza ruzuku mwaka huu tumelima jumla ya eneo la kilimo hekta million 15,890,362. Na ukiangalia Mikoa mikuu ya uzalishaji, kwa mfano Mkoa kama wa Ruvuma umeongeza eneo la kilimo kutoka eneo la hekta laki sita na elfu thelathini mpaka laki tisa na elfu sitini. Tafsiri yake nini? Tafsiri yake nikwamba distribution network itakuwa na mzigo mkubwa. Sisi kama Serikali hatua ya kwanza tuliyochukua tumehakikisha kuanza kuvisajili vyama vya ushirika. Maeneo ambayo kuna vyama vya ushirika tumevipa status ya kuwa distributor wa mbolea katika maeneo hayo; na hii inatupunguzia pressure na kutuondolea tatizo.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili tunayoichukua, sasa hivi tumeanza kusajili maghala yote yaliyoko vijijini na kuyapa status kama ni selling point kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo ili tutakapifika kuanzia mwezi wa saba, wa nane mbolea za kupandia na mbolea za kukuzia zote zinakuwepo katika vituo vya kuuzia mbolea na wakulima wanapouza mazao yao wanapata mbolea na kurudi. Hii itasaidia kuondoa huu utaratibu wa biashara ya mbolea ambayo waagizaji wote wanaagiza kuanzia mwezi wa tisa. Sasa tumewapa ruhusa, na hivi karibuni mtaona tangazo la pre-qualifications kwa ajili ya bulk procurement kwa mwaka ujao wa fedha. Naamini kwamba utaratibu huu utatuondolea pressure ya distributions network.
Mheshimiwa Spika, nitumie Bunge lako kuwashukuru Wabunge wote ambao wamekuwa wakipata changamoto, tukiwasiliana kwa ajili ya kutatua matatizo haya na wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika, mara mbili mara tatu uligeuka kuwa Afisa Kilimo kupita katika maduka na kuwa TFRA Officer na umetusaidia sana, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tutakumbana na changamoto, mfumo umeanza tarehe 15 Agosti. Naamini kwamba, maeneo mengi yamekuwa na upungufu, lakini upungufu huu utakwisha katika mwaka ujao wa fedha. Niwatoeni hofu, hatutakuwa na matumizi madogo kuliko ya msimu wa 2021/2022 ya mbolea katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nichangie eneo la pili, eneo la mfumuko wa bei. Ni kweli bei ya chakula imepanda na ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wote tukaelewa kwamba, chakula tunachokula leo ni kile kilichozalishwa msimu wa 2021/2022 ambapo wakulima walienda shambani wakiwa wamenunua pembejeo ghali, mara mbili ya bei iliyoko leo. Gharama za uzalishaji mwaka jana zilikuwa kubwa, pamoja na changamoto nyingine. Sasa hapa swali limeibuka miongoni mwa Wabunge; ruzuku hii inasaidia nini kwenye mfumuko wa bei? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hebu sote tufikiri leo, wakati unga ni shilingi 2,000 mkulima angekuwa anaenda dukani kununua mbolea kwa shilingi 140,000. Serikali imetoa ruzuku ili kumpunguzia ugumu wa maisha mwananchi huyu, leo badala ya kutumia shilingi 140,000, anatumia shilingi 70,000 anakuwa na disposable income ambayo anaweza kutumia kwenye shughuli nyingine. Serikali imempa ruzuku kwenye mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kunti ametolea mbegu aina moja ya Hysun, lakini mbegu ya alizeti ambayo sasa hivi inauzwa kupitia taasisi za Serikali inauzwa kwa shilingi 10,000 ambayo katika bei ya soko la kawaida angeinunua shilingi 20,000. Naamini kwamba, gharama hizi ambazo tunakabiliana nazo sasa na kote duniani, njia bora ya kuondoa mfumuko wa bei ni kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji. Serikali inachukua hatua hizo na matokeo yake tutayaona kwenye msimu ujao wa uvunaji ambao tunaanza kuvuna kuanzia mwezi wa Aprili, Mei na Juni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sekta yetu ya kilimo, historically, na bahati nzuri wengine wamo humu walimu wametufundisha, wamefundisha na sisi tumesoma nyaraka mbalimbali; toka tunapata uhuru mfumo wetu wa mawasiliano kwenye kilimo ni kilimo cha kujikimu. Ndio maana kilimo toka nchi hii inapata uhuru kimeshindwa kuwaondoa watu kwenye dimbwi la umaskini. Ni lazima tukiri zama zimebadilika, mahitaji yamebadilika, hakiwezi kuendelea kuwa kilimo cha kujikimu, ni lazima kiwe kilimo ambacho kinamwondoa mtu kwenye umaskini na kumpatia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kilimo kiwe cha namna hiyo ni lazima tuwekeze kwenye tija. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge watu-hold sisi responsible, Serikali kumsaidia mkulima kuongeza tija ya uzalishaji ili azalishe kwa tija na gharama za uzalishaji zitashuka na gharama za chakula zitashuka na wakulima watakuwa competitive ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho, bajeti. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu, limetupitishia bajeti ya zaidi ya bilioni 900, eneo la umwagiliaji ni eneo la procurement. Leo hii tunavyoongea kama Wizara, miradi yote ambayo tulitarajia kui-commission kwa ajili ya mwaka huu wa fedha tumesha-procure, wakandarasi wameshapatikana na sasa tumeshasaini mikataba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachotokea, tunakojenga wakulima wanalima. Hatuwezi kuwazuia wasilime, tumewapeleka wakandarasi wanasubiri wakulima wavune. Tutaanza kuziona certificates kuanzia mwezi Mei, Juni na Julai, ndio zitakwenda Wizara ya Fedha nyingi kwa ajili ya malipo. Miradi hii ni ya miezi 18, naamini hatuna problem kubwa sana na Wizara ya fedha. Mimi ni mkweli, nakuhakikishia, nikiona nina tatizo nitaenda kwenye mamlaka za juu, lakini as I stand today, sina big problem na Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu hela ya ruzuku ya mbolea; tumepokea bilioni 50…
SPIKA: Sekunde 30.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tumepokea bilioni 50. Ruzuku ya safari hii ni tofauti kabisa na ruzuku za zamani, hatuwezi kumlipa importer au distributer fedha kabla ya mkulima kuchukua mbolea. Imetuletea shida na wasambazaji, lakini huu ndio mwelekeo sahihi, tunalipa baada ya mbolea kununuliwa na mkulima na kui-verify na kuona DN, QR Code na namba ya mkulima, ndio importer analipwa fedha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, fedha zipo bilioni 150 na African Development Bank, dola milioni 41 ambazo zilikuwa kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na zenyewe zimepatikana, tutawalipa suppliers wote na tunaubadili mfumo wote wa usambazaji wa mbolea katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)