Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia kwenye Kamati zetu hizi zote mbili. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wa Kamati hizi pamoja na Wenyeviti wote ambao wamewasilisha hoja iliyoko Mezani.

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge kuishukuru sana Kamati ya Miundombinu ambao wamekuwa wakitoa kila mara ushauri katika Wizara yetu hii ya Ujenzi na Uchukuzi na wamekuwa msaada mkubwa katika mambo mengi. Nataka nifafanue zaidi hususan katika reli yetu ya SGR ambayo imeelezewa humu ndani, nataka niweke kumbukumbu sawa.

Mheshimiwa Spika, reli yetu ya SGR tangu imeanza kujengwa tulitangaza lot ya kwanza kutoka Dar-es- Salaam mpaka Morogoro. Kwa bahati mbaya waliorudisha tenda walikuwa ni wawili na hatimaye mmoja akajitoa akabakia mmoja, kwa hiyo, ikabidi afanye kazi hiyo mkandarasi mmoja. Kutoka Morogoro mpaka Makutupora ilipotangazwa alitokea mmoja, ikabidi apewe huyo huyo mmoja, lakini baada ya ku- bargain naye ama baada ya kupunguziana bei na lot iliyofuata ya Tabora – Isaka alitokea mmoja na akapewa kazi huyo huyo mmoja. Isaka – Mwanza walitokea wakandarasi wawili, aliyeshinda ndiye aliyepewa hiyo kazi.

Mheshimiwa Spika, sasa trend hii inaonesha nini? Kwa maana nyingine katika tenda zote ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi zimeainishwa, kuna tenda za aina nyingi, kuna competitive tender, kuna single source tender na zote ni njia sahihi ya kupata wakandarasi. Kwa hiyo, hakuna njia iliyo bora zaidi ya nyingine. Kwa hiyo, single source na ndio maana alivyokuwa anatokea mmoja huku tulikuwa tunam-award kwa sababu alikuwa amekidhi vigezo na Serikali tukawa tuimeridhia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niweke kumbukumbu sawa katika gharama za Mradi wa kutoka Tabora kwenda Kigoma pamoja Mradi kutoka Isaka kwenda Mwanza. Kwanza Mradi wa Isaka – Mwanza ulisainiwa Januari, 2021 kabla hata vita ya Ukraine na Russia, kwa maana nyingine kabla ya gharama kubwa kuongezeka. Mradi wa kutoka Tabora kwenda Kigoma umesainiwa tukiwa ndani ya vita ya Ukraine na Russia ambapo gharama za vifaa zimekuwa gharama kubwa sana, kwa vyovyote vile gharama yake itakuwa iko tofauti na mradi ule ambao ulisainiwa kabla ya dunia kuingia katika changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi wa Mwanza – Isaka ulikuwa Dola za Kimarekani pamoja na VAT, Dola za Kimarekani 1,123,794,312 hii pasipo VAT. Mradi ukiwa na VAT ulikuwa Dola 1,326,077,288 na gharama ya kilometa moja pasipo VAT, exclusive VAT, ni Dola za Kimarekani 3,295,584 na senti 49 na pamoja na VAT inakuwa Dola za Kimarekani kwa maana ya gharama ya kilometa moja 3,888,789 na senti 70. Huu ni Mradi wa Mwanza – isaka.

Mheshimiwa Spika, ukija Mradi wa Tabora – Kigoma; wote gharama yake pamoja na VAT ni Dola za Kimarekani 2,743,748,828 pamoja na VAT, pasipo VAT Dola za Kimarekani 2,325,210,871. Gharama kwa kilometa kwa huu mradi ni Dola za Kimarekani 4,595,000, hiyo pasipo VAT, ikiwa na VAT inakwenda Dola za Kimarekani 5,422,000.

Mheshimiwa Spika, kwa nini kuna variation kidogo hapa? Kuna variation kwa sababu, mbalimbali; ya kwanza, kutoka Isaka kwenda Mwanza kule ni mteremko au terrain yake ni ndogo. Kutoka Tabora kwenda Kigoma kuna terrain ama kuna…

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, Sheria ya Manunuzi pamoja na Kanuni zake zimetoa exception ya kutumia njia ya manunuzi ya single source, ambapo hizo taratibu inatakiwa lazima uzikidhi ndiyo uende. Sasa kama ufafanuzi huo anaoutoa kwamba huku Mwanza - Isaka ilitangazwa competitive watu wakashindana, lakini ilipofika Tabora - Kigoma haikutangazwa, na Sheria ya Manunuzi imeweka utaratibu wa namna ya kushughulika na single source.

Mheshimiwa Spika, single source inatumika tu pale inapolazimu kutumika. Sasa ukieleza kwamba suala hili kwingine huko kote tulitangaza akawa mmoja, kwa nini Tabora – Kigoma haikutangazwa akawa mmoja? Kwa nini akachaguliwa mtu mmoja? (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, nakuongezea dakika moja. Kwanza taarifa hiyo ya Mheshimiwa Mpina unaipokea? Halafu umalizie mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwanza taarifa yake siipokei kwa sababu nimeshamwonesha trend yote, kwamba kuna sehemu ambako miradi hii ilitangazwa, lakini akatokea mtu mmoja. Kwa hiyo, hata maeneo ya lot No. 3, na Na. 4, kwa sababu trend ilikuwa kutokea mtu mmoja duniani wakati tunatangaza katika competitive tender ikabidi tuendelee kumchukua huyo huyo pasipo kujali kwamba wapo wengine, kwa kuwa walikuwa hawatokei. Kwa hiyo, taarifa yake siipokei.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, nataka niweke kumbukumbu sawa katika Bunge lako kwamba kuwepo kwa mikataba hii ambayo ni fixed contract, maana yake haitakuwa na variation tena, tofauti na miradi mingine yoyote. Kwa lugha nyingine, hii fedha ambayo tumeingia mkataba hapa, haitabadilika mpaka mradi ukamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, nataka nisisitize kwamba tenda ya kutoka Tabora kwenda Kigoma imekuwa ni tenda sahihi na aliyepata amepata kiusahihi na ameanza kazi kuusahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Sawa. Sasa katika kuweka sawasawa hizo kumbukumbu ulizosema, maana yake hivi vipande vingine, tenda zilitangazwa, wale waliojitokeza ninyi mkawatazama mkampa aliyestahili. Hata mlikotangaza halafu akajitokeza mmoja ndiye aliyepewa. Kwa hiyo, ni sehemu moja tu ya kutoka Tabora kuelekea Kigoma ndiyo ambayo amepewa yule wa mwendelezo. Nimeelewa sawa sawa?

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, umeelewa sawa sawa, kwa sababu yule alikuwa tayari yuko site na tukawa tunaendelea na kazi. Kwa hiyo, tukaona ni bora pia huyu aendelee na kazi. Kwa sababu maeneo mengi tukitangaza walikuwa hawajitokezi katika competitive tender.