Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. MIRAJI J. MTATURU K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuhitimisha hoja yetu ambayo tuliiwasilisha pale asubuhi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii. Tulipata Waheshimiwa Wabunge 11 ambao walichangia kwenye hoja ambayo tuliiwasilisha hapa. Nawashukuru sana, sina sababu ya kuyarudia majina yao.

Mheshimiwa Spika, katika hoja ya jumla, ilionekana kuna tatizo la bajeti, kwamba Wabunge walikuwa na mashaka makubwa na sisi Kamati tulieleza, kwamba wakati tunawasilishiwa taarifa ilikuwa ni asilimia 23 tu hivi ya bajeti ambayo ilishafika kwenye Wizara zetu.

Mheshimiwa Spika, maelezo ambayo tumeendelea kuyapata ni kwamba kuna baadhi ya tenda ambazo zilikuwa kwenye utaratibu, ziko kwenye process. Bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasilioano na Teknolojia ya Habari alieleza kuna tenda kama ya minara ambayo tayari kama minara 700 hivi ambayo huenda ikafanyiwa kazi ndani ya miezi hii miwili. Kwa hiyo, maana yake ikikamilika ile ita shoot kwenda mbele zaidi tofauti na hii ya sasa. Kwa hiyo, nina amini kabisa maoni yetu ambayo tulisema yamechukuliwa na Serikali na sisi kama Kamati tunaendelea kusisitiza kwamba fedha zitolewe ili miradi iweze kutekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kumejitokeza hoja mahususi kama tatu na mojawapo ni hii ya SGR kipande cha Tabora- Kgoma ambacho kimeelezwa hapa na kimsingi ni kwamba umepata majibu ya Serikali kwa ufupi kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niseme tu kwamba sisi Kamati tumepokea maoni ya Wabunge ambao wameonesha concern hiyo kwamba ni vizuri kama kuna haja basi Mheshimiwa Spika kwa maelekezo yako, unaweza kuielekeza Serikali iweze kupitia kwa sababu haya ni maslahi mapana ya Taifa na ili iweze kuonekana kwamba Serikali inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,kama itakupendeza Kamati ya Katiba na Sheria ipo lakini pia sisi Miundo Mbinu tupo,ukielekeza upya wanaweza kutuletea kwa niaba ya Bunge tuweze kuitazama upya na kuona utaratibu mzima ulivyofikiwa. Lakini sisi kama Kamati tunaendelea kusema tena tutaendelea kusimamia Wizara hii katika kuhakikisha Miradi yote inatekelezwa kama ilivyopangwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja mahususi nyingine ambayo ilijitokeza ni hoja ambayo aliitoa Mheshimiwa Daktari Faustine Ndungulile ni hoja ya Vivuko. Na hili nieleze kwamba Mheshimiwa Ndungulile amekuwa ni mdau muhimu sana na eneo la Kigamboni kumekuwa na matatizo ya vivuko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakiri wote kwamba katika maeneo ambayo Serikali au Taifa liweze kuchukua hatua ni kuhakikisha kwamba vivuko vinafanyiwa ukarabati iwezekanavyo ili watu wetu waendelee kuwa salama. Lakini eneo lile la Kigamboni watu wengi sana wanavuka kutoka mjini kuja Kigamboni. Kwa hiyo, nakubaliana na yeye kabisa kwamba TEMESA, hata sisi ndani ya Kamati tumekuwa na wasiwasi mkubwa na namna ya utendaji wa TEMESA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,Kwa hiyo, niombe tu hili la kupeleka au kutangaza tenda na kupata mwingine baada ya ushindani, ninadhani iwe ni hoja ya sasa kama alivyosema Mheshimiwa Spika. Tuache ifanyiwe ukarabati kitengenezwe Kivuko ili wananchi wa Kigamboni wawe salama ili waweze kuishi salama na wasafiri salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu suala la maji hatuwezi kusubiri baadae kuja kuanza kutoa rambirambi kwa kitu ambacho kinakuja kuonekana wazi tungeweza kutengeneza. Kwa hiyo, niombe tu mchakato ambao ulitumika Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza na ninaamini kabisa umeenda sawa. Tunachotakiwa ni tusimamie Vivuko viwe salama, MV Magogoni itokee na iweze kuleta usalama wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, hoja mahususi ambayo ni ya mwisho ilikuwa ni ya Mheshimiwa Josephat Gwajima. Askofu alieleza suala la barabara ya kule Tegeta kwamba tuangalie barabara zenye uchumi mkubwa ziwe ni kipaumbele ziweze kutengenezwa ziweze kuzalisha mapato mengine ya kuweza kutengeneza barabara zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni sahihi kabisa na sisi kwenye Kamati tuliliona tulipokwenda kutembelea barabara ile ya kule Ludewa ambayo ina changamoto ya milima mikubwa sana. Tulienda kule tukashauri barabara ile iweze kutengenezwa ili chuma pamoja na mkaa ulioko kule utoke kwa haraka uende kule kwa ajili ya kwenda kuuzwa katika Bandari zetu na uweze kuleta pato kubwa la Taifa. Kwa hiyo, tunamkaa wa kutosha uko kule, kuna chuma ya kutosha kule lakini haitoki kwa sababu tatizo ni barabara haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru Serikali juzi tulivyoenda kukagua tumefanikiwa kupata Bilioni Tano imewekwa pale kwa ajili ya Milima fulani. Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa pale alikuwa ananiambia amefurahi kuona Serikali imewawekea fedha ya kutengeneza angalau sehemu ya Mlima kama Kilometa Saba. Kwa hiyo, nilitaka niseme kwamba hoja yako ni nzuri. Niombe Serikali ichukueni hii, barabara yenye uzalishaji na uchumi mkubwa zichukuliwe kipaumbele ili ziweze kuzalisha mapato ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hoja kubwa nyingine ilikuwa ni ile ya kuzima simu tarehe 13 Februari. Ninaomba nirudie tena kusema ili tuweze kuondokana na tatizo la Kimtandao, Serikali isirudi nyuma wale ambao hawajahakiki tarehe 13 tunamuunga Mkono Mheshimiwa Waziri simu zile zifungwe. Ili tujue nani hasa mwenye simu yake vinginevyo tukiendelea kufanya danadana tutaendeleza tatizo la kimtandao na hatutamaliza utapeli kwenye simu ambazo ziko kwenye mtaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya maneno hayo. Ninaomba nirudie tena kushukuru kwa hoja zote zilizotolewa, naomba nirudie tena sasa kwa heshima kabisa naomba kutoa hoja ili ipitishwe na Bunge ili yawe maazimio ya Bunge yakuweza kupitisha taarifa yetu, ahsante sana. (Makofi)

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, naafiki.