Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii nami niweze kuchangia hoja iliyoko Mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanya. Nitumie fursa hii pia kuzipongeza Wizara zote mbili; ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niende moja kwa moja kwenye hoja, na ninapenda kuchangia katika Shirika letu la SIDO. Kwanza kabisa kama ambavyo sote tunafahamu kwamba shirika hili lilianzishwa mahususi kwa kuwezesha viwanda vidogovidogo pamoja na kuongeza rasilimali katika bidhaa zetu na kutumia teknolojia mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, tumekuwa na ubunifu mwingi na vijana wengi wamekuwa ni wabunifu. Na kama Kamati tulipata fursa ya kutembelea TIRDO na pale tuliona kuna vijana wengi ambao wamekuwa wakibuni teknolojia mbalimbali. Mfano, tuliona kuna vijana ambao wamebuni application ya taa ambapo kupitia application hiyo unaweza ukawasha taa ukiwa ndani ama nje ama umbali mrefu lakini changamoto kubwa ya uendelezaji wa ubunifu huu ni kwamba vijana wengi hawana mtaji wa kuendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Kamati, na mtaona hata kwenye taarifa yetu, tumeomba ama tumeshauri Serikali kuona uwezekano kupitia SIDO na wataalam wake waone namna ya kubuni vyanzo mbadala ambavyo wanaweza wakawasaidia vijana hawa ili waweze kuendeleza ubunifu wao. Lakini pamoja na hayo, Serikali ione namna ya kuandika maandiko mbalimbali kupitia miradi mbalimbali ambayo itawasaidia wao waweze kupata zile fedha zilizopo katika Global Innovation Fund kupitia washirika mbalimbali wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Serikali iweze kuona vijana hawa wanaendeleza ubunifu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba vijana wanajiajiri. Na katika eneo hili upande wa SIDO tunatambua kwamba kuna mikopo midogomidogo inatolewa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa NEDF na tunaona juhudi hizo kupitia kwamba wanatoa mikopo yenye riba ya asilimia tisa upande wa miradi ya uzalishaji na asilimia 12 upande wa miradi ya kibiashara. Na kiwango kikubwa ambacho wanatoa ni kiasi cha shilingi milioni tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninapenda kuishauri Serikali kwa mjasiriamali ambaye anaanzisha kiwanda kidogo, milioni tano bado ni ndogo. Na kama mnavyofahamu, kiwanda au kubuni teknolojia kunahitaji kiwango kikubwa cha fedha. Sasa milioni tano bado ni kiwango kidogo. Niiombe Serikali iongeze kiwango hiki walau ikiwa kama milioni kumi itaweza kuwasaidia wajasiriamali wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la kuwezesha bidhaa za wajasiriamali hawa kufikia masoko. Tunatambua kwamba Serikali imekuwa ikitoa mafunzo lakini bado kuna changamoto upande wa wajasiriamali wetu; wanahitaji elimu zaidi upande wa branding, labelling na packaging ya bidhaa zao ili ziweze kushindana na bidhaa zinazoenda nje. Sasa TBS wanalo jukumu la msingi kuhakikisha kwamba bidhaa za wajasiriamali wetu zinathibitishwa ili ziweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo tunafahamu online businesses (masoko ya kimtandao), watu wengi katika kipindi hiki wamekuwa wakitumia masoko ya kimtandao. Sasa upande wa SIDO nilikuwa nikiangalia hapa utendaji wao wa kazi upande wa digital marketing bado ni mdogo kwa sababu bado watu hawajawa na uelewa mpana kuhusiana na shughuli ambazo zinafanywa na SIDO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimeangalia upande wa Instagram kwenye page yao wana 35.8k followers na upande wa Facebook wana 8k followers. Bado hawajajitangaza vya kutosha. Kwa hiyo, ninapenda kushauri watumie mitandao ili waweze kufikia idadi kubwa ya watu na waweze kujua vitu ambavyo vinafanywa na SIDO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninapenda kuzungumza; EPZA walitwaa maeneo ya wananchi upande wa Bagamoyo na Bunda, yalitwaliwa kwa ajili ya kuendeleza viwanda na sasa imekuwa muda mrefu maeneo hayo bado wananchi hawajalipwa fidia. Kwa hiyo, ninapenda kuishauri Serikali, na kupitia Kamati yetu tumeiomba, kwamba wananchi hawa walipwe fidia zao ili fedha watakazopata ziweze kuwasaidia kuendeleza maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Ahsante. (Makofi)